Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Heri Lamine Yamal hajamkuta Lionel Messi

Yamla X Messi Heri Lamine Yamal hajamkuta Lionel Messi

Sat, 20 Jul 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kwa sasa moja ya majina yanayotamba duniani ni la Lamine Yamal. Ndio. Kile alichokionyesha kwenye michuano ya Euro 2024 Ujerumani, ilikuwa lazima aimbwe kila kona.

Kipaji chake alichonacho tangu aanze kucheza soka kwenye akademi ya vijana ya Barcelona na hadi kupanda timu ya wakubwa, imekuwa gumzo.

Hata hivyo, kuna wanaoamini, endapo staa huyo angekuwa timu moja na Lionel Messi supastaa wa zamani wa Barcelona, asingefika au kufika huko anakotaka miaka mingine ijayo.

Kwa nini? Niliwahi kusikiliza mahojiano ya mshambuliaji wa zamani wa AC Milan, Barcelona na timu ya taifa ya Ghana, Kevin Prince Boateng na Rio Ferdinand akimzungumzia Messi.

Kevin, kaka wa Jerome Boateng aliyechagua kuichezea Ghana wakati mdogo wake akiitumikia Ujerumani, anasema alipojiunga na Barcelona mwaka 2019 kwa mkopo akitokea Sassuolo moja ya mambo yaliyomchanganya ilikuwa ni mtindo wa maisha ya Messi.

Anasimulia muda ambao wachezaji wote walikwa Gym kwa ajili ya kuweka miili sawa, hakuwa anamwona Messi katika eneo hilo na hata akija ni kwa ajili ya kuchuliwa tu misuli na muda mwingi ne alikuwa akicheza mpira wa kikapu (basket ball) au kuongea na simu.

Hii ni tofauti na kanuni iliyopo ama iliyojengeka kwa wachezaji wengi, ili ufanikiwe inabidi ufanye mazoezi sana ili mwili wako uwe sawa muda wote.

Hiyo imeonekana sana kwa Cristiano Ronaldo ambaye mara kadhaa katika mahojiano yake aliwahi kusema yeye ni binadamu aliyefikia kiwango cha mwisho cha kuutumikia mwili wake kwa jinsi anavyokula, anavyofanya mazoezi na mtindo wake wa maisha kwa jumla.

Messi hana maisha hayo. Kevin anasimulia hata walipokuwa wakienda katika vyumba vya kubadilishia nguo wakati wa mapumziko baada ya kipindi cha kwanza cha mechi kumalizika, pindi kocha alipokuwa anatoa maelekezo, Messi muda wote alikuwa bize na simu.

Baada ya maelekezo angenyanyuka na kuanza kujinyoosha kujiandaa kwa ajili ya mechi, alikuwa akifanya hivyo pia pindi mchezo unakaribia kuanza.

Messi angeonekana kuongea na watoto wake kwa simu kupitia video na ikibakia dakika kadhaa ndio ungemwona anaanza kujiandaa kwa ajili ya mechi. Messi hakuwa anajali hata kama ni mechi kubwa, alifanya hivyo mara zote na alipoingia uwanjani alionyesha kiwango bora.

Kwa mujibu wa Kevin, mtindo wa maisha wa Messi uliwaharibu wachezaji wengi waliokuwa wanachipukia. Wakati staa huyu wa kimataifa wa Argentina yupo katika timu hiyo aliwahi kuibuka Ansu Fati na aliwahi kusajili pia Ousmane Dembele.

Mastaa hawa walionekana huenda wangefuata nyayo za Messi kwa viwango lakini hawakufikia huko na moja kati ya sababu alizozieleza ilikuwa ni kuiga mtindo wa maisha wa Messi.

Hawakuwa wanataka kufanya mazoezi wakiamini wangeweza kuishi kama staa huyo na matokeo yake majeraha yakawa ndio sehemu ya maisha yao ya soka na matokeo yake Dembele akauzwa wakati Ansu Fati akiwa hapati nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza.

Wachezaji hawa ni wale wanaojulikana lakini kuna kundi kubwa la wachezaji wadogo walioibuka kipindi cha Messi na mwisho wakaishia pabaya kwa kumuiga staa huyo.

Imekuwa ni jambo zuri kwa Lamine hajamkuta Messi, inawezekana naye angeingia katika mkumbo huo. Bahati kwa Lamine anaingia katika Barcelona ambayo mshambuliaji ni Roberto Lewandowski ambaye licha ya umri wake amekuwa mmoja kati ya mastaa wanaoishi sana katika mazoezi.

Kwa mujibu wa Kevin licha ya Messi kuwa hafanyi mazoezi inavyotakiwa, usingeweza kuona pengo awapo uwanjani, alikuwa akikimbia vya kutosha na hata ukikutana naye alikuwa anakupa changamoto kama mtu mwenye mazoezi.

Ni heri Lamine hajamkuta binadamu huyu aliyetengenezwa kwa ajili ya mpira na mpira ukatengenezwa kwa ajili yake.

Licha ya watu wengi kuamini huenda Messi alimwachia maufundi staa huyo kutokana na kumuogesha katika picha za kalenda ya Barcelona, lakini kuna asilimia zaidi ya 50 angeishia pabaya kama angemkuta fundi huyo.

Chanzo: Mwanaspoti