Thierry Henry amethibitisha kwamba staa anayesakwa na Bayern Munich, ambaye anakipiga kwenye kikosi cha Crystal Palace, Michael Olise anataka kuichezea Ufaransa kwenye soka la kimataifa na si England.
Kocha wa England, Gareth Southgate alisema mwezi uliopita kwamba FA inamfuatilia winga huyo wa miaka 22, Olise baada ya kocha wa Ufaransa, Didier Deschamps kuamua kumweka kando kwenye kikosi cha mastaa wake aliowachagua kukipiga Euro 2024.
Fowadi huyo wa Palace, ambaye yupo kwenye hatua za mwisho kujiunga na Bayern kwa ada ya Pauni 51 milioni, alizaliwa Hammersmith, London na wazazi wake baba ni Mnigeria na mama yake ni Mfaransa aliyechanganya na Mualgeria.
Hivyo, Olise anaweza kucheza nchi nne tofauti kwenye soka la kimataifa, lakini kwa mujibu wa Henry, staa huyo anataka kuitumikia Les Bleus.
Gwiji hilo la Arsenal, ambaye kwa sasa ni kocha wa timu ya vijana ya Ufaransa chini ya miaka 21, Henry, ataongoza timu ya taifa hilo kwenye michezo ya Olimpiki itakayofanyika Paris baadaye katika kipindi hiki cha majira ya kiangazi.
Henry alimteua Olise katika sehemu ya kikosi chake cha awali cha wachezaji 25 na kusema: "Tunafahamu uwezekano wake wa kucheza sehemu nyingi, lakini mwenyewe anataka kuichezea Ufaransa. Lazima uonyeshe utayari ili uwepo kwenye timu ya Ufaransa.
"Kama angekuwa Mwingereza, angekuwa ameshaichezea England. Angeshafanya uamuzi wa kucheza kwenye michuano ya Ulaya na timu ya England kama ambavyo amefanya mchezaji mwenzake wa Palace, Eberechi Eze, lakini yeye anataka kuichezea Ufaransa na alijua hatakuwapo Euro 2024."
Olise tayari ameshaichezea Ufaransa kwenye timu za vijana chini ya miaka 18 na miaka 21, lakini ukizungumzia michuano ya Euro 2024 inayofanyika huko Ujerumani, kocha Southgate alisema wazi timu hiyo ilimhitaji sana Olise, licha ya kuwapo na ugumu wa kupata huduma yake.
Olise anahusishwa na mpango wa kutua Bayern, jambo ambalo atakuwa amezitosa Chelsea, Manchester United na Manchester City zilizokuwa zikihitaji huduma yake kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi.