Hakuna namna. Supastaa, Thierry Henry amesema kuna kitu kocha Mauricio Pochettino anapaswa kukifanya Paris Saint-Germain ili kufaidi mambo matamu ya staa wa mpira, Lionel Messi.
Henry ambaye alicheza kwa mafanikio makubwa Arsenal, Barcelona na timu ya taifa ya Ufaransa, anaamini Messi ‘anatengwa’ PSG.
Messi, 34 alitua PSG huko Parc des Princes bure akitokea Barcelona dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi baada ya miamba ya Nou Camp kushindwa kuendana na sera za La Liga juu ya mishahara ya mastaa.
Baada ya kutua PSG, kocha Pochettino amekuwa akimtumia pembeni huku akimchezesha Kylian Mbappe katikati.
Baada ya kuwa na maisha yenye mafanikio makubwa kwenye soka huko Nou Camp, Messi ameanza maisha Ufaransa kwa kasi hafifu uwanjani akiwa hajafunga bao lolote Ligue 1.
Na gwiji wa Arsenal, Henry – ambaye alicheza na Messi kwa miaka mitatu Barcelona, alisema anaamini Muargentina huyo kushindwa kufunga mabao PSG ni jambo linalopaswa kupatiwa ufumbuzi, atafutiwe nafasi nzuri ya kucheza sambamba na Neymar na Kylian Mbappe.
Henry aliambia RMC Sport: “Messi ametengwa, hapewi mpira sana. Siwezi kusema anahuzunika, ila ametengwa. Nadhani anapaswa kucheza katikati. Nina tatizo na Messi kucheza kulia. Pale katikati ataweza kutuliza kasi ya mchezo. Kuna kitu kinapaswa kufanywa ili kuwa na wachezaji Mbappe, Neymar na Messi wote wacheze kwa pamoja kwenye mechi.”
Hata hivyo, Henry anadhani Messi anapaswa pia kubadili staili ya kiuchezaji kwenye timu ambayo hajaandaliwa kucheza kuanzia kwake na kwamba kikosi cha PSG mashambulizi yote yamelengwa zaidi kwa Mbappe. Staa huyo Mfaransa aliongeza: “Messi si mzungumzaji sana. Yeye anazungumza akiwa na mpira tu.
“Kwa wakati huu, PSG ni timu ya Kylian. Kylian yeye ndiye anayeamua namna ya mchezo kwenye kikosi hicho, timu imejengwa kupitia yeye. Mipira yote inakwenda kwake.”
Kocha Pochettino amekuwa akimpanga Messi kulia katika safu ya washambuliaji watatu, huku Mbappe katikati na Neymar kushoto. Lakini, Henry anadhani eneo analochezeshwa Messi linambana, anashindwa kuonyesha makali yake ipasavyo.
“Sidhani kama anaweza kufanya kitu tofauti kwenye eneo hilo la kulia, lakini ndio hivyo siwezi kuzungumza sana kwa sababu sifahamu sababu za kiufundi za kocha,” alisema.
“Ni wazi, unapokuwa mbele kisha unawekwa pembeni na njia ya mpira, huwezi kuwa na madhara. Mipira michache sana itakufikia.”