Nilicheka pale niliposikia kiongozi mmoja wa Simba akidai Henock Inonga hauzwi. Umekuja uvumi huenda anatakiwa Morocco. Haitashangaza kama kutakuwa na uvumi mwingi kuhusu hatima yake.
Tuanzie wapi kabla hatujarudi huko? Tuanzie katika kiwango chake kwenye michuano hii ya Afcon. Kesho anatarajiwa kuiongoza tena DR Congo katika pambano dhidi wenyeji Ivory Coast hatua ya nusu fainali. Inonga na wenzake hawashikiki pale Ivory Coast.
Inonga ameendelea kuwa na kiwango kilekile ambacho huwa anacho nyumbani. Kesi yake itakuwa tofauti kidogo na ile ya kipa wa Yanga, Djigui Diarra. Jana niliandika mahala safari hii tutajua kama kinachomponza Diarra ni kimo. Tutajua kama ambacho hakikumpeleka Diarra Ulaya akitokea klabu ya kwao Stade Mallen ni kimo.
Naamini achilia mbali kimo chake alikuwa hana sifa ya kukosa hata timu ya Ligi Kuu pale Ubelgiji. Labda kimo ndicho ambacho kilisababisha aje huku. Kama akibaki basi tutajua kweli Wazungu wamegoma kumchukua.
Kwa nini kesi ya Inonga ipo tofauti? Tuanzie na ukweli ambao pia niligusia jana. Katika michuano hii ya Afcon wachezaji ambao wapo sokoni zaidi ni wachezaji wanaocheza soka la ndani la Afrika. Wanaocheza Ulaya tayari wana timu na wameshafahamika Ulaya. Wanaocheza ndani ya Afrika ni wachache, lakini wengi wamepatikana Taifa Stars. Wengine Zambia. Wengine wengi wapo Afrika Kusini na wengine ni hawa kina Inonga.
Kuna masoko mawili kwa Inonga kama ilivyo kwa Diarra. Kuna soko la ndani ya Afrika halafu kuna lile soko la nje ambalo linajumuisha Ulaya na Asia. Kwa soko la nje kwa kweli Inonga umri umekwenda. Miaka 30. Kwa soko la ndani Inonga bado wamo.
Inonga yupo sokoni kwa sababu moja kubwa ya msingi. Ni namna gani amefanikiwa kupenya katika kikosi cha DR Congo ambacho mara nyingi kinasheheni wachezaji kutoka Ulaya na kwingineko? Ni namna gani amefanikiwa kucheza mechi zote?
Zaidi ya kucheza Congo imekwenda mbali katika michuano hii. Sawa amezungukwa na mastaa wakubwa wanaocheza Ulaya lakini yeye pia amekuwa mhimili mkubwa katika timu. Yumo katika mastaa walioifikisha DR Congo nusu fainali ya
michuano hii na hauwezi kujua DR Congo itakwenda wapi zaidi.
Inonga ni tofauti na Fiston Mayele ambaye ingawa ana mchango wake katika kikosi cha DR Congo, lakini mara nyingi amekuwa akikaa benchi akimpisha Cedric Bukambu acheze katika nafasi yake. Ni wazi moja kwa moja jicho la mawakala na klabu kubwa za ndani ya Afrika limekwenda kwa Inonga.
Tofauti yake na Diarra ambaye tunaamini labda kimo kinamdhibiti katika nafasi yake, Inonga ni beki wa kati ambaye ni mrefu, ana nguvu na ana kasi. Kifupi, ana sifa zote za kucheza katika zile klabu za Afrika Kaskazini. Angeweza kuwa na sifa zote za kucheza hata Ulaya kama angekuwa na miaka 20. Katika hili soko la ndani kuna wababe wenye pesa chafu ambao wanaweza kufanya lolote na muda wowote. Nimecheka kusikia kauli ya kiongozi wa Simba, Inonga hauzwi. Rais wa Real Madrid, Florentino Perez aliwahi kutuambia hakuna mchezaji asiyeuzwa duniani. Inategemea tu una kiasi gani cha pesa.
Hawa rafiki zetu matajiri wa Afrika kina Pyramids, Al Ahly, Waydad, Zamalek, Berkane, FAR Rabat na wengineo wana pesa chafu. Wenyewe kwa wenyewe wanaweza kutunishiana misuli lakini sio klabu ya Afrika Mashariki ikitunishiana nao misuli.
Wanaweza kuweka Dola 500,000 lakini Simba wakaguna na kuweka kifua. Baadaye wakubwa wanakutana tena katika kikosi cha kahawa wanaweka mezani Dola 800,000 bado Simba wanatunisha misuli. Wakirudi na ofa ya Dola 1 milioni sioni kama Simba wanaweza kuzuia. Ukiandika kwa Dola kuna watu wanaweza wasielewe lakini Dola 1 milioni ni zaidi ya Sh2.2 bilioni.
Kudai Inonga hauzwi ni kujichonganisha na mashabiki tu. Leo unaweza kusema hauzwi halafu kesho ukatangaza kumuuza. Mashabiki watakuona hauna msimamo kumbe ni pesa ndio ambayo imeshawishi. Mara nyingi wanachofanya wenzetu huku kwa masikini ni kutangaza tu dau ambalo linaweza kumuondoa.
Hata kauli ambayo Perez aliitoa katika mauzo ya wachezaji ilitokana na kukerwa na kauli ya rais wa zamani wa Juventus, Luciano Moggi ambaye alitangaza staa wa timu hiyo wakati huo, Zinedine Zidane alikuwa hauzwi. Alidhani Perez angekuja na pesa ya kitoto. Akaja na pesa ambayo ilikata mzizi wa fitina.
Kitu kingine ambacho kinaweza kusababisha kuuzwa kwa Inonga nasikia ni namna mkataba wake ulivyokaa.
Nasikia amebakiza miezi michache katika mkataba wake wa sasa. Sina uhakika. Lakini kama kweli amebakiza miezi michache basi kinachopaswa kufanyika ni kupambana asaini mkataba mpya.
Asiposaini mkataba mpya basi kama ofa inatokea anaweza kuuzwa kuepuka hasara inayoweza kutokea endapo akiondoka bure. Mwishowe tujifunze kuwaambia ukweli mashabiki wetu wachezaji wote hawa wanaotamba katika klabu zetu wapo sokoni.
Unadhani Yanga walitamani kuachana na Mayele? Unadhani Simba walitamani kuachana na Clatous Chama na Luis Miquissone wakati ule? Ukweli, wachezaji wetu wote wanauzwa. Ni suala la kufika bei fulani tu.
Kitu kizuri hata mashabiki wa siku hizi ni waelewa. Wanajua soka ni biashara na kuna bei huwa haikataliki. Tuendelee tu kuwaandaa kisaikolojia wachezaji wetu wote wapo sokoni isipokuwa kwa bei sahihi.