Wakati wadau na mashabiki wa soka wakijiuliza hatima ya beki Mamadou Doumbia ndani ya Yanga kutokana na kutoonekana kikosini pia akiwa hajapewa ‘Thank You’.
Taarifa za kuaminika kuwa hawajamalizana. Yanga ilimsaini Doumbia katika dirisha dogo la msimu uliopita sambamba na kiungo Mudathir Yahya na mshambuliaji Kennedy Musonda ambao wanaendelea kukiwasha, lakini beki huyo raia wa Mali haonekani kikosini.
Baada ya Yanga kufanya siri na baadhi ya viongozi kuulizwa na kushindwa kuweka wazi juu ya Doumbia aliyesaini mkataba wa miaka miwili, mmoja ya vigogo wa timu hiyo (jina tunalo), amefunguka kuwa bado hawajamalizana, lakini wapo kwenye hatua nzuri.
Chanzo hicho cha kuaminika kilisema hatua iliyopo ni kumtafutia timu ili kumuuza ingawa timu nyingi zimeoyesha kutotaka huduma yake ikishindikana watamtoa kwa mkopo na wako mbioni kukamilisha hilo.
Kilichotokea kwa Doumbia ni kama kilichotokea kwa Gael Bigirimana aliyesajiliwa na Yanga msimu uliopita, lakini akatemwa dirisha dogo na kushindwa kuafikiana kiasi cha hivi karibuni kurejea kikosini kimyakimya au ilivyo kwa Peter Banda wa Simba inayeelezwa amempisha kipa Ayoub Lakred, huku akiwa bado yupo kikosini akisikilizia hatima ya kutafutiwa timu iwe kwa mkopo au kuuzwa.