Mchezaji wa zamani wa Leeds United na Manchester City, Danny Mills amesema kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp sio fundi kihivyo ni watu tu wanampa sifa asizostahili.
Klopp ambaye amedumu Liverpool kwa miaka tisa baada ya kuchukuwa nafasi ya Brendan Rodgers Oktoba 2015, ameiwezesha timu hiyo kushinda karibia mataji yote makubwa kuanzia ya ndani na nje ya England.
Malejendi na makocha wa zamani wa Liverpool kama Bob Paisley na Bill Shankly, walimtaja kama ndio kocha bora wa muda wote kuwahi kutokea kwenye timu hiyo.
Hata hivyo, Mills hakubaliani na hili akiamini mafanikio aliyoyapata hayafikii baadhi ya makocha waliopita kwenye timu hiyo.
Akiwa kwenye moja ya vipindi vya televisheni vya talkSPORT, Mills alisema: “Ameshinda Ligi Kuu England mara moja kwenye miaka tisa.”
Mills aliongeza kwamba haoni kama alifanya kitu kikubwa ukizingatia alikaa kwa misimu mitano kabla ya kuchukua ubingwa wake wa kwanza wa ligi jambo ambalo makocha mbalimbali walilifanya kwenye misimu yao miwili au mmoja wa kwanza.
“Claudio Ranieri amewahi kushinda ligi, makocha wanaenda Chelsea na kushinda taji la EPL kwenye msimu wao wa kwanza na wengine wamekuwa wakishinda kwenye misimu yao ya pili.”
Mtangazaji alimwambia Klopp aliikuta Liverpool kwenye hali mbaya ikiwa haijawahi kuchukuwa ubingwa kwa miaka 30, na Mills akasema: “Blackburn hawakuwahi kuchukua, wakachukua, Chelsea haikuwa imechukuwa ubingwa katika miaka 50 wakati Jose Mourinho anachukuwa mikoba ya kuifundisha (akatwaa EPL katika msimu wake wa kwanza tena kwa pointi 95).”
Gwiji huyu pia akadai kwamba yeye kwake Klopp ni bora lakini hawezi kabisa kufikia levo za Pep Guardiola na akasisitiza mbali ya watu kuona Liverpool haitumii pesa nyingi kwenye kipindi ambacho Klopp amehudumu ni uongo, kocha huyu anatumia pesa.
“Wameuza wachezaji kwa pesa nyingi, ukiangalia mfano kwa Philippe Coutinho walipokea karibia Pauni 120 milioni, wanalipa mishabara mikubwa mfano kwa Mohamed Salah anayepokea kati ya Pauni 400,000 hadi Pauni 500,000 kwa wiki, Thiago Alcantara naye amesajiliwa.”