Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

He! Bosi wa Forest amchenjia refa

Tajiri Nottingham He! Bosi wa Forest amchenjia refa

Mon, 4 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Tajiri mmiliki wa Nottingham Forest, Evangelos Marinakis ameripotiwa kwamba alilazimika kuondolewa na walinzi baada ya kumfukuzia mwamuzi Paul Tierney hadi kwenye korido za kuelekea vyumbani kwenye Uwanja wa City Ground baada ya mechi ya Liverpool kwenye Ligi Kuu England juzi Jumatatu.

Shuhuda, ambaye ni mfanyakazi wa BBC 5 Live, alidai kwamba tukio hilo limetokea baada ya Forest kupoteza mechi kwa bao la utata katika kipigo cha 1-0 dhidi ya Liverpool, ambapo mfungaji Darwin Nunez, alifunga kwenye dakika ya 99.

Tajiri Marinakis, kocha wa kikosi cha kwanza Steven Reid na maofisa wengine walikwenda kumvaa mwamuzi Tierney baada ya filimbi ya mwisho ya kumaliza mpira. Refa Tierney alimtoa kwa kadi nyekundu Reid.

Shuhuda alisema: “Ni mara chache sana kuona tukio kama lile kwenye korido. Mmiliki wa timu Marinakis ilibidi aondolewe kwenye eneo la tukio la walinzi. Kocha Reid alikasirishwa, hivyo yeye na bosi wake Marinakis walimfuata Tierney na Graham Scott kwenye korido wakati wanaelekea kwenye vyumba vya marefa.

“Walikuwa wakiwapigia kelele, 'Heshimu wachezaji, heshimu wachezaji. Hivi vitu vinatokea kila wiki. Heshimu wachezaji'."

Shida ilianzia baada ya mwamuzi Tierney kumpa mpira kipa wa Liverpool, Caoimhin Kelleher baada ya kusimamisha mchezo kufuatia beki Ibrahima Konate kuumia.

Kimsingi mwamuzi alichopaswa kufanya baada ya kusimamisha mpira na kisha kuendelea, basi alipaswa kumpa staa wa Forest, Callum Hudson-Odoi, kwa sababu ndiye aliyekuwa mtu wa mwisho kumiliki mpira kabla ya filimbi ya kusimamisha mechi.

Mechi hiyo iliongezwa dakika nane, lakini Nunez alifunga kwa kichwa kwenye dakika 99, hiyo ina maana muda uliokuwa umeongezwa ulipita jambo ambalo liliwakasirisha sana Forest.

Akizungumza baada ya mechi, kocha mkuu wa Forest, Nuno Espirito Santo alisema: "Sitaki kuzungumza kitu kuhusu waamuzi. Naomba msinisukume kwenye hilo."

Mshauri wa waamuzi wa klabu hiyo, ambaye alikuwa refa wa zamani, Mark Clattenburg alisema: "Ni dhahiri mmiliki alichukia kwa sababu aliona uamuzi umeenda kinyume cha klabu yake. Forest ilipaswa kurudishiwa mpira wake. Lakini, walipewa Liverpool, wakaenda kufunga."

Chanzo: Mwanaspoti