Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

He! Bocco siku 111 buana!

Bocco2 660x400.jpeg He! Bocco siku 111 buana!

Sun, 7 Nov 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

JOHN Bocco ‘Adebayor’ ndiye anayeshikilia rekodi ya kuwa mchezaji aliyefunga bao kwa misimu 13 mfululizo tangu 2008, lakini huwezi kuamini kwamba hadi leo straika huyo wa Simba ametimiza siku 111 bila kucheka na nyavu.

Hadi kufikia sasa Ligi Kuu Bara msimu huu ikiwa raundi ya tano, Bocco bado hajafunga bao lake kuboresha rekodi yake ya kutupia ndani ya misimu 14 mfululizo, kwani alipata nafasi ya kuandika historia walipovaaa na Biashara United mjini Musoma, lakini alipoteza mkwaju wake wa penalti.

Kama hujui ni kwamba mara ya mwisho kwa Bocco kufunga bao lake katika Ligi Kuu Bara ilikuwa Julai 18 mwaka huu wakati ligi ya msimu uliopita ikihitimishwa kwa kufunga bao la penalti dakika za jioni wakati wakiifumua Namungo kwa mabao 4-0 na bao hilo kumfanya awe Mfungaji Bora.

Bao hilo lilimfanya Bocco afikishe mabao 16 na kumpiku nyota mwenzake wa Simba, Chriss Mugalu aliyekuwa na mabao 15 na kwenye mchezo huo dhidi ya Namungo alitupia mawili, lakini dakika nne za nyongeza ilitokea penalti na Bocco kwenda kuipiga na kufunga.

Ukihesabu tangu alipofunga bao hilo la mwisho lililompa tuzo ya ufungaji bora wa msimu uliopita hadi leo wakati ligi ikiwa imesimama kwa wiki mbili ni sawa na siku 111, ingawa kwa namna ligi ilivyo mbichi bado mkali huyo anayo nafasi ya kutupia na kuboresha rekodi yake.

Katika misimu 13 ya kufunga mfululizo akiitumia Azam kwa misimu tisa na minne akiwa na Simba, Bocco amefunga jumla ya mabao 139 na kumfanya awe kinara wa mabao wa muda wote kwa sasa katika ligi ndani ya misimu hiyo.

Aliyekuwa Kocha Mkuu wa Geita Gold, Etienne Ndayiragije alisema jambo la straika wa kiwango cha Bocco humtokea yeyote yule hivyo ni suala la muda kwa straika Bocco kurejea kwenye makali yake.

“Tangu msimu kuanza timu nzima haijatulia, ingawa rekodi zake ndizo zinazomuhukumu ila binafsi nadhani atakapopata bao moja ndipo atazidi kujiamini na kufunga zaidi, sina shaka naye kwenye hilo,” alisema Ndayiragije.

Mchezaji wa zamani wa Simba,Nicholas Gyan anayekipiga kwa sasa DTB iliyopo Ligi ya Championship alisema ukame wa mabao kwa mshambuliaji yeyote hutokea, lakini kwa ubora alionao mbele ya lango ni suala la muda tu kufunga.

“Hata wachezaji wakubwa kwenye ligi zilizoendelea humtokea yeyote kwa hiyo mimi sishangai kwa sababu bado ni mapema hivyo tuendelee kuwa na subira,” alisema Gyan.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz