Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Haya hapa Maajabu ya Simba kimataifa

Simba Rekodi CAF Simba SC

Sun, 30 Oct 2022 Chanzo: Mwanaspoti

WANACHAMA, mashabiki na wapenzi wa Simba kwa sasa wanahesabu siku kabla ya kujua timu yao itangukia kundi gani kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba iliyozaliwa mwaka 1936 ndio timu pekee kati ya tatu za Tanzania zilizoshiriki mechi za mchujo za Ligi ya Mabingwa, ikiiacha Yanga ikiangukia kwenye play-off ya Kombe la Shirikisho Afrika, huku KMKM iking’olewa kabisa.Hii sio mara ya kwanza kwa Simba kuibeba nchi, kwani timu hiyo ndio tishio kwenye michuano ya CAF kutoka Tanzania, ikiwa imeandika rekodi kadhaa za kusisimua zinazoibeba na kuifanya istahili kuitwa jina la Taifa Kubwa, jina iliyobatizwa miaka ya 1990.

Klabu hiyo yenye maskani yake jijini Dar es Salaam imekuwa na rekodi nzuri katika michuano ya CAF bila kujali kama ni Klabu Bingwa Afrika (sasa Ligi ya Mabingwa Afrika) ama Kombe la Washindi na CAF (sasa Kombe la Shirikisho Afrika). Also Read

SIMBA YA MAKUNDI CAF: Rekodi, jina vyawabeba Kolamu 1 hour ago

Hapo chini ni dondoo chache za umwamba wa Simba kwenye mechi za kimataifa, ikiwa ndiye kinara kwa timu za Tanzania tangu nchi ilipoanza kushiriki michuano hiyo mwaka 1969.

SUNDERLAND HADI SIMBA

Mwaka 1971, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Tanzania, Abeid Amaan Karume alizitaka klabu kuachana na majina ya kigeni na Rais huyo wa kwanza wa Zanzibar aliyejulikana kama Simba katika harakati za kudai Uhuru wa nchi za Afrika, jina ilo aliLIpendekeza litumike kutokana na sifa zake.

SIMBA NUSU FAINALI 1974

Hii ndio rekodi kubwa kuwekwa na klabu hiyo kimataifa baada ya kutinga hatua ya nusu fainali katika Klabu Bingwa Afrika (sasa Ligi ya Mabingwa Afrika). Klabu hiyo ilianza mchezo wa raundi ya kwanza ugenini dhidi ya Linare ya Lesotho na kushinda mabao 3-1.

Katika mchezo wa marudiano, Simba ilishinda 5-1 na kuitoa timu hiyo kwa jumla ya mabao 8-2.

Raundi ya pili, Simba iliitoa Green Buffaloes ya Zambia ugenini mchezo uliisha kwa sare tasa na nyumbani Simba ikashinda 9-0. Hapo Simba ilifuzu robo fainali na kukipiga dhidi ya Accra Hearts of Oak ya Ghana. Katika mchezo wa kwanza ugenini Simba ilishinda 2-1 na nyumbani ikatoa sare tasa.

Nusu fainali Simba ilicheza dhidi ya Ghazl El Mahalla Sporting Club au El Mahalla, maarufu kama Mahalla El Kubra.

Mchezo wa kwanza, Simba ilishinda bao1-0 nyumbani na ugenini ikafungwa 1-0. Ikatolewa kwa penalti 3-0 na wapinzani wao hao walienda kubeba taji hilo.

YAWEKA REKODI AFIKA 1979

Mwaka 1979, Simba ilicheza mchezo wa kwanza nyumbani dhidi Mufulira Wanderers na kufungwa 4-0. Kila mtu aliamini Simba ilikuwa imetoka kwenye michuano hiyo. Ikiongozwa na Kocha wa Timu ya Taifa, Taifa Stars ambaye ni mwanachama mtiifu wa Yanga, Joel Nkya Bendera (kwa sasa ni marehemu), Simba ilipindua meza ugenini na kushinda 5-0 na kufuzu hatua inayofuata.

Raundi ya pili, Simba ilienda kutoa sare tasa Nigeria dhidi ya Rocca Rovers lakini ikafungwa 2-0 nyumbani.

FAINALI ZA CAF

Mwaka ambao Simba iliweka heshima ni kufika fainali za Kombe la CAF 1993 ilifika fainali baada ya kutoka sare ugenini na Stella Abidjan ya Ivory Coast.

Safari ya michuano hiyo iliyounganishwa na ile ya Kombe la Washindi na kuzaliwa kwa Kombe la Shirikisho Afrika, Simba iliitoa Ferroviario de Maputo ya Msumbiji kwa faida ya bao la ugenini baada ya suluhu nyumbani katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza na kutoka sare ya 1-1 ugenini kisha ikaivaa Manzini Wanderers ya Swaziland (Eswatini ya sasa) na kuipiga nje ndani kwa bao 1-0 kila mchezo katika raundi ya pili na kutinga robo fainali.

Simba iliitoa USM El Harrach ya Algeria kwa mabao 3-2, ikishinda 3-0 na kupasuka ugenini 2-0. Nusu fainali ilivaana na Waangola, Atletico Sport Aviacao na kuing’oa kwa jumla ya mabao 3-1.

Simba ilishinda nyumbani mabao hayo kisha kutoka suluhu ugenini. Ndipo Simba ikatinga fainali za michuano ya Afrika, lakini ikakatiliwa nyumbani na mabao ya Boli Zozo, aliyefunga kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru) na wageni kuondoka na taji wakikabishiwa na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Pili kipindi hicho, Mzee Ali Mwinyi.

ROBO FAINALI

Ikitoka kuaibika nyumbani kwenye fainali za CAF, msimu uliofuata wa michuano ya CAF, Simba ilishiriki Klabu Bingwa Afrika na kufanikiwa kufika robo fainali mwaka 1994 ikitolewa na Nkana Red Devils. Raundi ya kwanza iliifunga Al Merrikh ya Sudan kwa jumla ya mabao 2-0, ikishinda nje ndani bao 1-0 Raundi ya pili ikaitoa BTM Antananarivo ya Madagascar kwa bao 1-0, ilipoenda ugenini ilipata suluhu.

Ikakutana na Nkana kwenye robo fainali na safari ikaishia hapo kwa kufungwa ugenini 4-1 japo ilijitutumua na kushinda nyumbani 2-0.

HESHIMA AFRIKA

Mwaka 2003 Simba ilirudi na kishindo. Iliifikia rekodi ya Yanga ya kucheza makundi, imng’oa bingwa mtetezi Zamalek ya Misri kwa penalti baada ya kila mmoja kushinda kwake 1-0 kwake.

Simba ilianzia kuitoa BDF XI ya Botswana 1-0 nyumbani kisha 3-1 ugenini na kufuzu kwa jumla ya mabao 4-1.

Raundi ya kwanza iliing’oa kwa penalti 9-8 Santos ya Afrika Kusini baada ya suluhu ya mechi zote mbili na Simba ikatinga raundi ya pili dhidi ya Zamalek na kuoing’oa kwa penalti 3-2.

WAARABU WANAIJUA

Ukiacha kufanya kweli kwenye mechi za CAF, lakini rekodi tamu ya kuzitetemesha vigogo kutoka Afrika Kaskazini iliifanya Simba iwe na heshima kubwa Afrika, kwani katika michuano hiyo imekuwa ikikutana na Waarabu na bado ikawatoa jasho. Simba haijawahi kufungwa na timu yoyote kutoka Afrika Kaskazini uwanja wa nyumbani, na imezipasua Al Ahly, Mehalla Kubra, Zamalek, Ismaily, El Mokawloon, El Merrikh, El Harach.

Hata hivyo, udhaifu wa Simba ukiondoa rekodi ya kuing’oa Zamalek, Simba imekuwa ikitaabika ugenini dhidi ya timu za Kiarabu, kwani ni mara chache imewahi kulazimisha sare, isipokuwa mechi nyingi imekuwa ikipasuka, rekodi ya karibuni ni kupigwa mabao 5-0 na Al Ahly msimu wa 2018.

Chanzo: Mwanaspoti