Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Haya Trossard atakiwa fasta huko Saudi Arabia

Leandro Trossard Leandro Trossard

Mon, 2 Sep 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Miamba ya soka ya Saudi Pro League, Al Ittihad imeripotiwa kuishtua Arsenal baada ya kupeleka ofa ya kumtaka winga, Leandro Trossard.

Licha ya kwamba dirisha la usajili limefunga England, klabu za soka za Saudi Arabia bado zinasajili wachezaji, usajili wao bado haujafungwa.

Kinachoelezwa ni kwamba Al Ittihad imeweka mezani Pauni 29.5 milioni kama ofa ya kupata huduma ya mkali huyo wa kimataifa wa Ubelgiji. Na sasa Arsenal itakuwa na kazi ya kuamua kama inataka kumpiga bei winga huyo au itagoma na kubaki na huduma yake.

Na kama Arsenal itachukua uamuzi wa kumuuza Trossard, basi itapata faida ndogo sana. Trossard, 29, alijiunga na Arsenal akitokea Brighton kwa ada ya Pauni 20 milioni pamoja na bonasi ya Pauni 7 milioni kwenye dirisha la Januari.

Na sasa kocha wa Arsenal, Mikel Arteta anamchukulia winga huyo kuwa mchezaji wake muhimu kwenye kikosi cha kwanza.

Trossard alifunga mabao 19 na asisti 12 katika mechi 71 alizocheza tangu alipojiunga na miamba hiyo ya Emirates.

Arsenal ilihitimisha dirisha la usajili wa majira ya kiangazi huko Ulaya kwa kumnasa kwa mkopo winga Raheem Sterling kutoka Chelsea. Mastaa wengine iliyowasajili Arsenal kwenye dirisha hilo ni makipa David Raya na Neto, kiungo Mikel Merino na beki Riccardo Calafiori.

Chanzo: Mwanaspoti