Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hawatoki salama leo!

Yanga Vs Simba FT Yanga vs Simba utapigwa saa 11

Sun, 23 Oct 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Mwisho wa ubishi. Mashabiki wa Simba na Yanga, leo hakuna wanachokisubiri ila pambano la timu hizo zinazokutana kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara msimu huu utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku wakitambiana salama ya timu mojawapo ni kutoenda uwanjani tu.

Kuingia uwanjani kwenye mchezo huo utakaoanza saa 11:00 jioni, ina maana moja tu, mmoja lazima alie, kwani hata vigogo wa klabu hizo hawaamini kutakuwa na droo leo Kwa Mkapa. Licha ya viongozi na mashabiki wa klabu hizo kuamini mechi hiyo lazima izae mabao, ila rekodi baina ya timu hizo inaonyesha mechi ya watani ngumu, kwani katika vikosi vya sasa vya timu hizo ni wachezaji watatu tu ndio waliofunga katika dabi ya ligi, huku katika mechi 10 zilizopita hakuna mbabe.

Wachezaji hao waliofunga kwenye dabi na wapo kwenye vikosi vya leo ni Erasto Nyoni na Joash Onyango kwa upande wa Simba, huku Yanga akiwa ni Zawadi Mauya, wakati Bernard Morrison ambaye amefunga pia katika dabi ya ligi akiwa anatumikia adhabu ya kifungo cha utovu wa nidhamu.

Rekodi zinaonyesha kwenye mechi 10 za dabi katika ligi tangu msimu wa 2017 hadi mwaka huu kila timu imeshinda mara mbili tu na michezo sita kumalizika kwa sare na yakifungwa jumla ya mabao 12, kila timu ikifunga sita na mshindi wa leo anaweza kuboresha zaidi rekodi dhidi ya mwenzie.

Licha ya kuwa mchezaji pekee wa Yanga katika kikosi cha sasa aliyewahi kufunga dabi ya ligi, Mauya huenda asiwepo kwenye kikosi cha kwanza ila anaweza kuwapo benchi la wachezaji wa akiba, kwani eneo hilo la kiungo lina mafundi kama Yannick Bangala, Khalid Aucho, Feisal Salum, Gael Bigirimana na Salumu Abubakar ‘Sure Boy’ aliyerejea baada ya kuugua ghafla wiki iliyopita.

Onyango aliyefunga bao la kusawazisha katika mechi ya Nov 7, 2020 ana nafasi kubwa ya kuanza leo, wakati Nyoni aliyefunga katika mechi ya April 29, 2018 kwenye mechi ambayo Yanga ililala 1-0, uwezekano wa kucheza ni mdogo kutokana na ubora wa Enock Inonga na Mkenya huyo, japo maamuzi yapo kwa Kocha Juma Mgunda.

REKODI TAMU

Rekodi zinaonyesha tangu msimu 2017-2018 miamba hiyo imekutana mechi 10 za Ligi Kuu Bara na kushindwa kutambiana kwani kila timu imeshinda mechi mbili tu, huku zilizosalia zikiisha kwa sare kuonyesha leo kutakuwa na kazi kwelikweli.

Mara ya mwisho Simba kupata ushindi mbele ya Yanga ilikuwa Feb 16, 2019 kwa bao lililofungwa na Meddie Kagere na baada ya hapo timu hiyo imekuwa ikisaka ushindi bila mafanikio. Kagere kwa sasa yupo Singida Big Stars.

Mechi zilizofuata za 2019-2020 timu hizo zilishindwa kutambiana kwa kufunga 2-2, kisha BM33 akiwa Yanga kufunga bao pekee katika mchezo wa marudiano na Msimu 2020-21, mechi ya kwanza iliisha kwa sare ya bao 1-1, wakati ile ya pili Simba ilifungwa 1-0 kwa bao la Mauya.

Michezo ya msimu uliopita yote iliisha kwa suluhu na mchezo wa leo utaamua nani awe mnyonge au mbabe mbele ya mwenzake.

WACHEZAJI WA KUCHUNGWA

Kulingana na ubora wa vikosi vya timu zote mbili kuna wachezaji wanatakiwa kuchungwa kwenye mchezo wa leo utakaochezeshwa na mwamuzi Ramadhan Kayoko ambao wanaweza kuamua matokeo Kwa Mkapa. Kwa kikosi cha Yanga, Fiston Mayele mwenye mabao matatu hadi sasa ndio tishio kwa Simba kutokana na rekodi yake ya mechi za Ngao ya Jamii kwa misimu miwili mfululizo akiitungua Simba kwa mabao matatu na kuwapa kazi kubwa kwa mabeki Henock Inonga na Joash Onyango.

Muda wote wa mchezo Inonga, Onyango wanatakiwa kuwa makini dhidi yake, kwani tofauti na hivyo anaweza kuwapelekea kilio kama ilivyokuwa kwenye mechi ya Ngao ya Jamii.

Pia kuna Feisal Salum ambaye ameiliza Simba mara mbili za nusu fainali kwenye Ngao ya Jamii, ikiwamo ile ya Simba iliyoshinda 4-1 naye kufunga la kufutia machozi na lile la msimu uliopita wakati akiipeleka Yanga fainali na kwenda kubeba taji mbele ya Coastal Union iliyokuwa chini ya Mgunda.

Wengine ni Stephane Aziz Ki, Farid Mussa na Tuisili Kisinda, lakini kwa Simba nyota tishio kwa beki ya Yanga ni Moses Phiri aliyeweka kambani mabao manne kwenye ligi huku akiwa na muendelezo mzuri wa kufunga mabao katika michezo mfululizo ikiwamo ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Phiri hana mambo mengine, lakini ana akili ya kutupia nyavuni kutokana na kupenyezewa pasi za kutokea upande wa kushoto wenye beki Mohammed Hussein na Augustine Okrah na Clatous Chama.

Chama naye hakuna mechi yoyote ya ligi dhidi ya Yanga aliyowahi kucheza kwenye kiwango bora ni mchezaji wa kuchungwa kutokana na uwezo wake mkubwa wa kufanya jambo la hatari haswa mpira unapokuwa mguuni kwake kwani kwa sasa anaonekana yupo moto kwelikweli kwa pasi zake matata. Wachezaji wengine kutoka Simba hatari kwa sasa na wanatakiwa kuchungwa, Pape Sakho, Augustine Okrah, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Mzamiru Yassin.

KUREJEA/KUKOSEKANA

Kwenye mechi ya mwisho Yanga ilicheza ugenini na Al Hilal ya Sudan iliwakosa nyota wake wawili, Sure Boy na Denis Nkane ambao wamerejea kikosini kama ilivyokuwa kwa Bigirimana ambaye hivi karibuni alikuwa ni majeruhi.

Kurejea kwa nyota hao watatu kikosini kutaongeza nguvu ndani ya Yanga hasa eneo la kiungo linaloweza kwenda kuamua mechi kutokana na uimara wa Simba upo katika eneo hilo, wakati huo huo itamkosa Morrison kutokana na kufungiwa.

Simba huenda ikawakosa nyota wake wawili kwa sababu ya majeruhi, Shomary Kapombe na Jimsonu Mwanuke wakati huo huo kuna urejeo wa Pater Banda ambaye hivi karibuni alikosekana kwa sababu ya majeruhi.

WANAWEZA KUANZA

Kulingana na michezo ya Yanga msimu huu kikosi chao huenda kikaanza na mfumo (4-3-3 au 4-2-3-1), utakuwa na wachezaji, Djigui Diarra, Djuma Shaban, Kibwana Shomary, Dickson Job na Bakar Mwamnyeto. Eneo la kiungo kuwakuwa na wawili chini wa kukaba, Khalid Aucho, Yannick Bangala wakati juu yao kutakuwa na mtaalam Feisal Salum na watatu wa juu watakuwa Jesus Moloko, Farid na Mayele.

Kikosi cha Simba huenda akitaanza tafauti na mifumo miwili ya Yanga na kipa atakuwa, Aishi Manula, Israel Mwenda, Tshabalala, Inonga, Onyango, Mzamiru Yasin, Sadio Kanoute, Chama, Phiri, Okrah na Pape Ousmane Sakho.

Kulingana na vikosi vilivyo ushindani mkubwa utakuwa katikati mwa uwanja kwa timu zote mbili kwani zina wachezaji wabunifu pindi wanapomiliki mpira na wenye uwezo wa kukaba wanapokuwa hawana mpira. Viungo wa timu moja kati ya Simba na Yanga watakaokuwa imara kwenye kutimiza majukumu yao itakuwa silaha kwa timu yao kupata ushindi.

MBINU KALI

Kocha wa Yanga, Nassredine Nabi anahitaji kupata ushindi kwenye mchezo huo mkubwa ili kupunguza presha iliyopo nyuma yake baada ya kushindwa kuivusha timu hiyo hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika.

Nabi ataingia kwenye mechi hiyo kwa nidhamu kubwa kulingana na ubora wa Simba ulivyo sasa pamoja na timu yake kushindwa kufunga mabao kwenye kipindi cha kwanza haswa michezo ya hivi karibuni. Miongoni mwa silaha aliyokuwa nayo Nabi ni kufanya vizuri na kupata matokeo bora kwenye michezo aliyokutana na Simba na uwezo wa kubadilika kimbinu hasa kipindi cha pili.

Kwa upande wa Mgunda ataingia na matumaini makubwa ya kupata ushindi kutokana na muendelezo mzuri aliyokuwa nao wa kupata matokeo bora pamoja na viwango vizuri wanavyoonyesha wachezaji wake tangu alipoichukua timu hiyo kutoka kwa Zoran Maki.

Mgunda kikosi chake hakitakuwa na mabadiliko makubwa na atacheza zaidi katikati mwa uwanja huku akimtumia, Okrah na Phiri kwenye kutoa pasi za mwisho kwa washambuliaji akiwemo Phiri kufunga mabao. Kama Simba itapata ushindi chini ya Mgunda inaweza kuwafanya viongozi wa timu hiyo kuacha kufikilia suala la kumleta kocha mpya na ikabaki nae kwenye nafasi hiyo hadi mwisho wa msimu.

WASIKIE MAKOCHA

Kocha wa Yanga, Nabi ameelezea hali ya kikosi chake na aliwaomba radhi mashabiki wa timu hiyo baada ya kuondoshwa Ligi ya Mabingwa Afrika na Al Hilal ya Sudan kwa kufungwa jumla ya mabao 2-1 na kuwataka kusahau yote yaliyopita.

“Tumesahau yote yaliyopita na akili zetu tumezielekeza kwa Simba, ni mchezo mgumu kutokana na kiwango ambacho kimeonyeshwa na wapinzani wetu kwa siku za karibuni lakini tupo tayari ili kushinda,” alisema Nabi.

Nabi aliongeza katika mchezo huo atamkosa nyota wake, Bernard Morrison ambaye anatumikia adhabu ya kukosa mechi tatu baada ya kumkanyaga kwa makusudi beki wa Azam, Lusajo Mwaikenda wakati kiungo, Salum Aboubakar ‘Sure Boy’ yupo hatihati pia ya kutocheza kutokana na majeraha yanayomkabili ingawa atafanyiwa tathimini ya mwisho.

Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake kiungo wa timu hiyo, Zawadi Mauya alisema “Mechi ya Dabi siku zote ina presha kubwa ila hilo halipo kwetu kwani tupo tayari kupambana kwa ajili ya mashabiki zetu, hivyo nawaomba waje kwa wingi kutupa sapoti kwa sababu naamini hatutawaangusha.”

Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Simba, Juma Mgunda alisema anawaheshimu wapinzani wao kwani wana wachezaji na benchi bora la ufundi hivyo watacheza kwa kuwaheshimu ingawa malengo yao ni kuhakikisha wanashinda mchezo huo.

“Shomari Kapombe ameanza mazoezi mepesi ila hatokuwa sehemu ya kikosi cha leo sambamba na Jimmyson Mwanuke anayeuguza majeraha ila waliobaki wote wako tayari kwa ajili ya kuipambania timu kupata ushindi,” alisema.

Nahodha wa Simba, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake alisema licha ya kutokuwa na matokeo mazuri dhidi ya Yanga kwa miaka ya karibuni ila wamejifunza kutokana na makosa na hawapo tayari kuona hilo likiendelea.

Yanga ambaye ni bingwa mtetezi anaingia katika mchezo huo akiwa na kumbukumbu nzuri ya kushinda mchezo wa mwisho waliokutana kwenye Kombe la Ngao la Jamii Agosti 13, mwaka huu baada ya kuifunga Simba mabao 2-1.

MASTAA NA MAMILIONI

Kambi za timu zote zimeongezewa mzuka kwa mabosi wa klabu hiyo kutoa ahadi ya mamilioni ya fedha kama watahakikisha timu hizo zinatoka na ushindi.

Simba mambo yamekuwa moto zaidi kutokana na bilionea Mohammed Dewji sambamba na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Salim Abdallah ‘Try Again’ kusema imetosha kuwa wanyonge kwa Yanga tangu 2019, huku matajiri wa Yanga wakisisitiza kazi iendele ili kupoza machungu ya kung’olewa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Hata hivyo, kambi zote zimekuwa wasiri kuanika kiasi hicho cha fedha, lakini habari kutoka ndani ya timu ni kwamba mkwanja waliowekea sambamba na zile fedha walizojazwa mapema kulipa malimbikizo ya fedha waliozkuwa wakidai kwa timu zote umekoleza utamu wa mchezo huo wa leo.

Chanzo: Mwanaspoti