Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hawana kazi! Makocha hawa wanazurura tu mtaani

Tuchel Thomas Tt.jpeg Thomas Tuchel

Mon, 13 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Tottenham Hotspur imeripotiwa kuwa kwenye vita kali ya kumshawishi Kocha Thomas Tuchel aende kuwa kocha wao mpya baada ya kuona Antonio Conte akiwa na changamoto kadhaa. Sambamba na Tuchel, kocha mwingine ambaye yupo kwenye rada za Spurs ni Mauricio Pochettino, ambaye anahusishwa na mpango wa kurudi klabuni hapo.

Hata hivyo, makocha hao wawili, Tuchel na Pochettino ni miongoni tu mwa mabosi maarufu ambao kwa sasa hawana kazi, wakiwa karibu na simu zao muda wote kusikilizia mchongo mpya wa kurudi mzigoni.

9) Andre Villas-Boas

AVB hana kazi kwa sasa. Anataka kazi au hataki hicho ni kitu ambacho bado hakijawekwa wazi. Lakini, kocha huyo hajawahi kuficha mpango wa kustaafu ukocha mapema. Alipita Chelsea mwaka 2011 na amekuwa kwenye ukocha tangu 2009. Kazi yake ya mwisho ilikuwa Marseille, ambako aliondoka baada ya kushindwana na viongozi juu ya sera yao ya usajili. Kwa sasa AVB anasubiria tu kazi.

8) Marcelino Toral

Mhispaniola huyo alichukua uamuzi wa kuachana na Athletic Bilbao katika kipindi cha majira ya kiangazi ya mwaka jana baada ya kukosa imani na aliyekuwa akigombea urais kwenye klabu hiyo. Marcelino ni maarufu mno kwenye soka la Hispania, akiwahi kuzinoa pia Valencia, Villarreal na Sevilla. Lakini, kwa sasa hana kazi na anapatikana tu sokoni, akisubiri mchongo mpya jambo ambalo linamfanya simu yake muda wote iwe imejaa chaji.

7) Rafael Benitez

Ni kocha mkubwa, lakini maisha ya Rafa Benitez huko Everton hayakuwa mazuri kabisa. Rekodi zake kwenye ukocha ni tamu akipita kwa mafanikio katika klabu nyingi ikiwamo ya Valencia, Liverpool na Chelsea. Lakini, Benitez hana kazi kwa sasa, huku mara kadhaa jina lake likihusishwa na klabu za Leeds United na Southampton. Benitez ni kocha mkubwa ambaye simu yake imejaa chaji akisikilizia mchongo mpya.

6) Joachim Low

Mjerumani huyo ni mmoja kati ya makocha 21 walioshinda ubingwa wa Kombe la Dunia. Lakini, tangu ang’atuke kwenye Timu ya Taifa ya Ujerumani, Low hajapata mchongo wa kwenda kuinoa timu ya klabu, hasa ukizingatia alidumu na timu hiyo ya taifa kwa takribani miaka 15. Kuna nyakati alihusishwa sana na Fenerbahce, lakini tangu alipoachana na Ujerumani mwaka 2021, hana mchongo mwingine anasubiri tu simu iite kupewa dili la mchongo mpya.

5) Marcelo Bielsa

Kufukuzwa Leeds United kutokana na timu hiyo kuwa kwenye hali mbaya ni moja ya mambo yaliyotibua rekodi zake. Maisha ya Bielsa huko Elland Road yalikuwa matamu kabla ya mambo kutibuka. Bielsa ni mmoja kati ya makocha wenye hadhi kubwa kwenye soka, akihusudiwa pia na makocha wengine kama Pep Guardiola – lakini ukweli ndio huo, hana kazi, anasubiri ajira mpya baada ya kuachana na Leeds United.

4) Zinedine Zidane

Zidane ni kocha mahiri au alikuwa na zali na timu ya Real Madrid? Ni swali linaloulizwa, kwa sababu Mfaransa huyo hajawahi kufanya kazi kwingine zaidi ya Bernabeu, mahali ambapo alikuwa kocha kwa awamu mbili. Zidane alipochana na Real Madrid kwa mara ya pili, iliripotiwa atakwenda kuchukua mikoba ya Didier Deschamps kwenye kikosi cha Ufaransa, lakini mpango huo umekwama na Zidane hana na kazi hadi sasa.

3) Luis Enrique

Klabu kubwa na timu za taifa zimeripotiwa kufikiria mpango wa kumwajiri Luis Enrique kufuatia kuachana na Hispania kabla ya Kombe la Dunia. Chelsea ilitajwa kuhitaji huduma ya kocha huyo wa zamani wa Barcelona kabla ya kumpa kazi Graham Potter. Timu ya Taifa ya Brazil nayo iliwahi kutajwa kumtaka Mhispaniola huyo. Lakini, hadi sasa, Enrique hana kazi jambo linalomfanya simu yake muda wote ijae chaji kusikilia mchongo mpya.

2) Mauricio Pochettino

Muargentina, Mauricio Pochettino hakauki kwenye ishu za kuhusishwa na ajira mpya kwa kipindi hiki ambacho amekuwa hana kazi tangu alipoachana na Paris Saint-Germain. Mara kadhaa, Pochettino alihusishwa na kibarua cha Manchester United kabla ya kukubali kazi ya kwenda kuinoa PSG huko Parc des Princes. Kwa sasa, Pochettino anahusishwa na mpango wa kurudi Tottenham. Anangoja simu iite.

1) Thomas Tuchel

Kocha wa zamani wa Chelsea, Thomas Tuchel yupo tu kwa sasa hana kazi tangu alitoswa kibarua Stamford Bridge. Mjerumani huyo aliondoshwa PSG na kupewa kibarua cha kuinoa Chelsea, ambako aliipa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kocha huyo hana kazi kwa sasa na siku za karibuni amekuwa akihusishwa na mpango wa kutua Tottenham Hotspur.

Tangu ameondoka Chelsea klabu hiyo haijakaa sawa,Tuchel yupo karibu na simu yake, akisubiri mchongo mpya.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live