Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hawa watu wa kazi

Watu Kazi Hawa watu wa kazi

Thu, 30 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Soka la wanawake nchini limezidi kukua huku klabu zikisajili wachezaji wa kigeni na timu zetu zikifanya vyema katika michuano ya kimataifa.

Msimu uliopita Simba Queens ilifika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika kwa wanawake na msimu huu JKT Queens imefika makundi ya michuano hiyo mikubwa zaidi kwa ngazi ya klabu kwa wanawake Afrika.

Timu ya wasichana ya shule ya Fountain Gate ya Dodoma ilitwaa ubingwa wa Afrika wa Shule za Sekondari nchini Afrika Kusini wakati timu ya taifa ya U-17 ya wasichana Serengeti Girls ilifika robo fainali katika fainali za Kombe la Dunia 2022 lililofanyika India, hizi zikiwa ni baadhi tu ya timu za mabinti nchini zilizofanya makubwa.

Mwanaspoti linakuchambulia baadhi ya mastaa wa soka la wanawake nchini ambao uwanjani wanakiwasha ile mbaya.

Mwanahamis Omary ‘Gaucho’

Ni miongoni mwa wachezaji wakongwe katika kikosi cha Simba Queens ambaye ameupiga mwingi kwa miaka mingi akizitumikia klabu zake na timu za taifa.

Mkali huyo wa kutupia mabao aliwahi kufanya makubwa pia akiwa na klabu ya Shabab Atlas ya Ligi Kuu ya soka la wanawake ya Morocco.

2. Winifrida Gerald (Fountain Gate)

Achana na umbo lake dogo, Winifrida Gerald kwa sasa amekuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha timu za taifa.

Ukimuona unaweza kujua hapa kazi ipo kwani ni miongoni mwa wachezaji machachari anapokuwa uwanjani.

Mchezaji huyo alitisha zaidi kwenye michuano ya CAF ya ubingwa wa Shule za Sekondari Afrika huko Afrika Kusini alikoshinda tuzo mfungaji bora na mchezaji bora baada ya kufunga mabao 11 kwenye michuano hiyo ambayo Fountain ilibeba kombe hilo.

Ukiachana na hilo aliisaidia timu ya taifa U-18 kubeba ubingwa wa CECAFA kwa mara ya kwanza mashindano waliyokuwa yakifanyika kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamanzi, akibeba tuzo ya mchezaji bora baada ya kuifunga Uganda bao 1-0.

3. Amina Ally (JKT Queens)

Msimu uliopita alikuwa na wananchi wa kike, Yanga Princess na baada ya mkataba wake kuisha akajiunga na wanajeshi wa JKT Queens.

Tangu amejiunga na JKT, kiungo huyo ameanza kuonyesha kiwango bora kwenye michuano ya CECAFA na Ligi ya Mabingwa kwenye eneo la kati.

Ni miongoni mwa viungo ambao wanacheza na kufurahia kabumbu na kwa namna anavyocheza unajua ni mtu wa kazi.

4. Donisia Minja (JKT Queens)

Tangu ajiunge na JKT msimu wa mwaka 2016 akitokea Evergreen kiungo huyo amekuwa na kiwango bora.

Donisia ambaye safari yake ya soka aliianza mwaka 2004 katika shule ya msingi ya Airwing hadi sasa amekuwa mchezaji muhimu katika kikosi hicho na kuweka ufalme kwenye eneo la kiungo.

Licha ya kuwa kiungo mkabaji lakini ana uwezo wa kufumania nyavu na kuwa tishio kwenye tuzo za wafungaji bora.

Msimu uliopita ambapo timu yake ilibeba ubingwa alimaliza Ligi na mabao 17 nyuma ya aliyekuwa mfungaji bora, Jentrix Shikangwa ambaye alimaliza na mabao 19 akiwa na Simba Queens.

5. Fatuma Issa ‘Fetty Densa’ (Simba Queens)

Fetty Densa anajiweka tofauti na wachezaji wengine hasa staili yake ya kuvaa hijabu ambayo inamfanya kujulikana akiwa uwanjani.

Beki huyo ambaye unakuwa msimu wake wa tano akiwa na Wekundu wa Msimbazi tangu atue mwaka 2019 na kubeba mataji matatu ya Ligi Kuu na kufika nusu fainali Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ukiachana na kufanya vizuri kwenye Ligi pia amekuwa msaada kwenye kikosi cha timu ya taifa ‘Twiga Stars’ na ukimuona tu uwanjani kazi ipo.

6. Naijat Abas (JKT Queens)

Mara nyingi makipa wamekuwa hawazungumzwi sana lakini Naijat Abas amekuwa muhimu kwenye kikosi cha JKT na timu ya taifa.

Alifanya vizuri kwenye michuano ya CECAFA, JKT ikibeba ubingwa huo baada ya dakika 90 kuisha kwa sare ya bila kufungana dhidi ya C.B.E ya Ethiopia kisha kuokoa mkwaju wa penalti mmoja wakishinda 4-5.

Aliivusha pia Tanzania hatua inayofuata kwenye fainali za kufuzu mataifa ya Afrika kwa wanawake (WAFCON) yatakayofanyika mwakani nchini Morocco baada ya kufuta mkwaju mmoja wa penalti dhidi ya Ivory Coast.

Matokeo ya kwanza nchini Abdijan aliruhusu mabao 2-0 na mchezo uliofuata Azam Complex Chamazi, Stars ilishinda mabao 2-0 na kuruhusu mikwaju ya penalti ambayo aliokoa 2-4 na kutinga hatua ya pili ambayo wanakutana na Togo.

7. Asha Djafar (Simba Queens)

Msimu wa mwaka juzi aliibuka kinara wa mabao akiweka nyavuni mabao 27 kwenye mechi 22 za Ligi Kuu lakini msimu uliopita alishindwa kutetea kiatu hicho baada ya kumaliza na mabao manane kwenye mechi 18.

Ukiachana na msimu uliopita kusuasua kwenye uhakika wa kukosa namba lakini winga huyu ni kitasa kweli kweli namna anavyozunguka uwanjani na kupeleka mashambulizi lango la mpinzani.

Asha ambaye ni raia wa Burundi amekuwa akifanya vizuri kwenye kikosi cha timu yake ya taifa.

8. Noela Luhala(Yanga Princess)

Beki wa Yanga na timu za taifa za U-17, U-20 na U-18 amekuwa akikitendea haki kitambaa cha unahodha kwenye timu hiyo.

Michuano ya CECAFA U-18 aliisaidia timu hiyo kutoruhusu bao lolote na licha ya kuwa beki lakini alimaliza mashindano kwa kufunga mabao mawili kwenye mechi tano.

8. Stumai Abdallah (JKT Queens)

Achana na utanashati na urembo anaoendelea kuonyesha nje ya uwanja lakini ni miongoni mwa washambuliaji makini uwanjani.

Msimu uliopita alimaliza Ligi na mabao 13 na kuweka rekodi ya wachezaji wawili yeye pamoja na Donisia kufunga mabao matatu (hat-trick) katika michezo miwili tofauti.

Chanzo: Mwanaspoti