Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hawa watano watamsahaulisha Gomez pengo la Chama na Miquiisone

Luis Chama Wachezaji wa Simba walioondoka dirisha lililopita

Fri, 1 Oct 2021 Chanzo: Mwanaspoti

Simba haijafunga bao katika mechi tatu mfululizo dhidi ya TP Mazembe, Yanga na kisha Biashara United na leo watashuka uwanjani dhidi ya Dodoma Jiji, huku mashabiki wa klabu hiyo wakiwa hawana furaha kwa vile hawakuzoea kukutana na hali hiyo, lakini koch Didier Gomes akapewa akili ya maana.

Kocha huyo na benchi lake la ufundi limepewa majina ya wachezaji watano ambao inaelezwa kama wataamua kuwapa nafasi basi watambeba katika mechi ya leo na nyingine zikiwamo za kimataifa na kuondoa jinamizi baya linaloikabili timu hiyo.

Wachezaji hao ambao Gomes ameshauriwa kuwatumia ni viungo Jonas Mkude, Mzamiru Yassin, Pape Sakho, pamoja na Duncan Nyoni na Yusuph Mhilu.

Kocha na Mratibu wa Friends Rangers, Heri Mzozo alisema kama Gomes atawapa nafasi wachezaji hao timu inaweza kurudi kwenye mstari na ikaanza kupata matokeo mazuri

“Shida ya Simba ipo katikati ya uwanja na aina ya mfumo ambao kocha amekuwa akiutumia. Yule Rally Bwalya bado hawapi Simba kile wanachokitarajia katika nafasi anayocheza hivyo ni bora wajaribu kumtumia Pape Sakho katika nafasi ile maana anaonekana ni mbunifu na mwenye maamuzi ya haraka,” alisema Mzozo aliyewaibua nyota kadhaa wanaotamba nchini na nje ya nchi na kuongeza;

“Pia katika kiungo, Taddeo Lwanga akirejea apewe nafasi kwa kucheza ama na Jonas Mkude au Mzamiru Yassin. Mkude nampendekeza zaidi maana ana uwezo mkubwa wa kuhamisha mipira kutoka upande mmoja kwenda mwingine, pia Yusuph Mhilu na yule Duncan Nyoni walionyesha kiwango kizuri mechi na Biashara nao wapewe nafasi wataisaidia timu.”

Mzozo alisema kinachoifanya Simba ishindwe kufunga na kutengeneza nafasi za mabao, sio ubutu wa washambuliaji bali ukosefu wa huduma nzuri kutokea eneo la katakati.

“Kuchezesha washambuliaji wawili haimaanishi ndio timu itafunga bao. Timu inapaswa iwe imara zaidi katikati na iwe na kiungo anayeweza kutengeneza nafasi kwa straika lakini unapochezesha washambuliaji wawili huku ukiwa na Bwalya asiyesaidia kukaba, timu inakuwa na mzigo mkubwa,” amesema Mzozo,

Beki wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa amesema Gomes anapaswa kuwa makini na upangaji wa kikosi hasa katika eneo la kiungo, kwani ndio kinachomuangusha kwa sasa tangu waondoke Clatous Chama na Luis Miquissone waliyekuwa tegemeo.

“Jambo la msingi kwa sasa, mwalimu akazane kujenga timu kwani Simba imeachana na nyota waliokuwa na ufanisi mkubwa kikosini, Luis na Chama na wamekuja wapya wanaotakiwa kuzoea falsafa ya timu na ya kocha,” amesema Pawasa, kocha wa timu ya taifa ya soka la ufukweni na kuongeza;

“Naamini Simba imesajili wachezaji wazuri na wanachokihitaji ni ile maelewano ya kitimu. Bahati mbaya wanakabiliwa na presha ya kupata matokeo mazuri, huku kocha akiwa na kundi kubwa la wachezaji na kuwa na kibarua cha kujua nani anaendana na falsafa na mbinu zake. Katika nafasi ya kiungo kwa mfano ana wachezaji takribani saba.”

“Kwa mchezo mmoja anatakiwa kuwatumia viungo wasiozidi watano, hivyo sio kazi rahisi. Wapo wachezaji ambao wanaonekana wana kitu kama akiwapa nafasi zaidi Simba itafanya vizuri,” amesisitiza Pawasa, huku

Kiungo wa zamani wa Nazareth ya Njombe, Tigana Lukinja alisema Gomes asisite kuwapa nafasi wachezaji wengine ikiwa wanaocheza mara kwa mara wanashindwa kufanyia kazi mbinu.

“Simba ipo katika mabadiliko ya kiuchezaji. Kocha afanyie kazi zaidi uchezaji wa kitimu, wakati mwingine kuruhusu wachezaji watumie uwezo binafsi, ikishindikana tunashauriwa kutumia baadhi ya wachezaji wasiopata nafasi ya kucheza ili kupindua meza,” alisema.

Chanzo: Mwanaspoti