Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hawa wakikutana kwani itakuwaje?

Pacome Zouzoua Nov.jpeg Hawa wakikutana kwani itakuwaje?

Tue, 14 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ligi Kuu Tanzania Bara imesimama kwa muda kupisha timu ya taifa ‘Taifa Stars’ kucheza mechi za kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2026 ambapo itaanza kucheza na Niger Novemba 18 huko Morocco (ambako Niger wanakutumia kama uwanja wa nyumbani) kisha kucheza na Morocco kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Novemba 21.

Ligi imesimama baada ya timu 14 kucheza mechi tisa kila moja isipokuwa Simba na Mashujaa ambazo zina kiporo cha mchezo moja ambao utazikutanisha zenyewe.

Wakati ligi ikisimama, Yanga ambayo ni bingwa mtetezi inaongoza msimamo ikiwa kwa imekusanya pointi 24 kwenye mechi tisa ilizocheza, ikishinda mechi nane na kufungwa moja.

Baada ya ligi kusimama, Spoti Mikiki inakuletea tathmini ya kikosi cha wachezaji wa kigeni waliofanya vizuri zaidi katika mechi tisa za Ligi Kuu dhidi ya kile cha wazawa ambavyo kama vingekutana, mechi ingekuwa na uhondo wa aina yake.

KIKOSI CHA WAGENI DJIGUI DIARRA

Ni kipa anayeshikilia tuzo ya kipa bora kwa misimu miwili mfululizo iliyopita. Msimu wa 2022-23 alicheza mechi 17 bila kuruhusu bao. Ameendeleza ubora huo msimu huu akicheza dakika 630 kwenye mechi saba ambazo amekaa golini kwa dakika 90 mechi mbili amezikosa akicheza Metacha Mnata na Abutwalib Mshery.

Diarra kwenye dakika hizo alizochezea Yanga msimu huu ameisaidia kutokufungwa bao kwenye mechi nne huku ikipata ushindi dhidi ya JKT Tanzania, Namungo FC, Geita Gold na Singida Big Stars.

Diarra ametajwa kwenye orodha ya makipa kumi wanaowania tuzo ya kipa bora wa mwaka wa Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) akiungana na kipa namba moja wa Manchester United, Andre Onana.

KOUASSI YAO

Ni usajili mpya ndani ya Yanga aliyenaswa baada ya timu hiyo kumuacha Djuma Shabani ambaye aliomba kuondoka ndani ya timu hiyo akiwa tayari ameipa mataji mawili ya Ligi Kuu Bara na kutaka kwenda kujaribu maisha kwingineko.

Dirisha kubwa Yanga ikainasa saini ya Yao kutoka ASEC Mimosas na ujio wake umekuwa na manufaa kwa timu ukimweka nje Kibwana Shomari ambaye alikuwa panga pangua chini ya kocha Nasreddine Nabi ambaye pia ametimka ndani ya timu hiyo.

Yao ndani ya kikosi cha Yanga tayari amecheza dakika 655 akicheza mechi nane kati ya tisa walizocheza kabla ya kuivaa Coastal Union ameifungia timu yake bao moja na kutoa asisti tano.

CHEIKH SIDIBE

Ni nyota wa timu ya taifa ya Senegal ambaye anakipiga Azam FC katika msimu wake wa kwanza nchini na ameingia moja kwa moja katika kikosi cha kwanza akisaidiana na Pascal Msindo au Edward Manyama ambao ndio wanabadilishana kwenye nafasi hiyo.

Beki huyo tayari amepachika bao moja kwenye ligi katika mchezo dhidi ya Singida Big Stars na uwepo wake ndani ya kikosi hicho umewafanya mashabiki wa timu hiyo kumsahau Mzimbabwe Bruce Kangwa ambaye aliachwa baada ya mkataba wake kuisha.

CARNO BIEMES

Ni beki panga pangua wa kikosi cha kwanza cha SBS akimkimbiza Pascal Wawa ambaye alitua kikosini hapo akitokea Simba ambaye sasa amerudi nchini kwao Ivory Coast.

Sasa yeye ni beki ambaye anaongezewa mchezaji wa kucheza naye kati ya Abdulmajid Mangalo na Joash Onyango (majeruhi) ambao wote hawana uhakika wa kucheza mara kwa mara katika kikosi cha kwanza.

HENOCK INONGA

Ni beki kisiki kwelikweli ambaye anaunda safu ya beki wa kati na Che Fondon Malone ambaye amesajiliwa msimu huu.

Kama ambavyo ilikuwa msimu uliopita ambapo aliingia kwenye kikosi bora cha msimu cha TFF hakuna shaka kuwa anaweza kuendelea kuwa sehemu ya kikosi hicho kwa msimu mwingine tena kutokana na ubora wake licha ya timu yake kuruhusu mabao, amekuwa imara zaidi eneo hilo ambalo amejihakikishia namba kikosi cha kwanza.

MAROUF TCHAKEI

Ni kiungo aliyevunja utawala wa Bruno Gomes ndani ya Singida Big Stars kutokana na ufundi wake ambapo katika msimu wake wa kwanza tu kucheza Ligi Kuu tayari ameifungia timu yake mabao manne.

Tchakei anacheza nafasi ya kiungo mshambuliaji anaweza kutokea pembeni pia lakini tangu ametua SBS amekuwa akitumika zaidi namba 10 na kutoa mchango mkubwa kwenye timu yake.

MAXI NZENGELI

Mtambo wa mabao ndani ya kikosi cha Yanga hadi sasa amehusika moja kwa moja katika mabao tisa katika mechi tisa alizocheza akifunga saba na kutoa asisti mbili.

Maxi ambaye amecheza dakika 668 amejiunga na Yanga msimu huu na kujihakikishia namba kikosi cha kwanza akimtupa nje Jesus Moloko ambaye alikuwa panga pangua msimu uliopita.

CLATOUS CHAMA

Ukiongelea wapishi wa mabao basi lazima umtaje Mwamba wa Lusaka, Clatous Chama ambaye hadi sasa ametoa asisti mbili za mabao.

 Fundi huyo ambaye kwa sasa ameongezea nguvu kwenye nafasi yake akipambana sambamba na Saido Ntibazonkiza ni kati ya wachezaji bora wa kigeni waliopata kutokea kwenye soka la Tanzania.

PACOME ZOUZOUA

Ni usajili mpya ndani ya Yanga lakini tayari ameingia kwenye mfumo akiwa ni nyota panga pangua kikosi cha kwanza licha ya kukutana na Stephane Aziz Ki ambaye ni msimu wake wa pili.

Pacome ambaye anacheza nafasi ya kiungo mshambuliaji ndani ya timu hiyo tayari ameifungia mabao manne timu yake kwenye mechi nane walizocheza hadi sasa.

PRINCE DUBE

Ni msimu wake wa tatu ndani ya Azam FC. Pamoja na changamoto yake ya kukaa nje kwa muda kutokana na majeraha ya mara kwa mara, amekuwa na mchango mkubwa kwenye timu anaweza asimalize msimu lakini akawa ameshatupia mabao kambani.

Msimu huu timu yake ikiwa imecheza mechi tisa tayari amepachika mabao matatu, ni mchezaji namba mbili ndani ya timu yake akiongozwa na kiungo Fei Toto.

STEPHANE AZIZ KI

Ni kinara wa upachikaji wa mabao Ligi Kuu hadi sasa sambamba na Maxi Nzengeli wa Yanga na Jean Baleke wa Simba baada ya kufunga mabao saba kila mmoja. Ki pia ametoa asisti tatu akiisaidia timu yake kuongoza msimamo baada ya kukusanya pointi 24.

Ki ni msimu wake wa mwisho Yanga baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili msimu uliopita na ni kiungo ambaye amejihakikishia namba kikosi cha kwanza chini ya Miguel Gamondi.

Sub: Abdulai Iddrisu, Nicholaus Wadada, Joyce Lomalisa, Joash Onyango, Khalid Aucho, Jean Baleke, Fabrice Ngoma, Idris Mbombo, Elvis Rupia na Mabrouck Amza,

Kocha: Miguel Gamondi (Yanga), Melis Medo (Dodoma Jiji)

KIKOSI CHA WAZAWA ARON KALAMBO

Ni zao la timu ya vijana ya Tanzania Prisons kabla ya kwenda kuchezea Polisi Morogoro mwaka 2015. Alirejea Prisons mwaka 2016 akacheza hadi mwaka 2020 alipohamia Mbeya City, kabla ya kujiunga na Dodoma Jiji FC msimu uliopita na anaendelea kukipiga huko.

Kalambo ni kipa ambaye alijijengea ufalme ndani ya timu ya Dodoma Jiji kutokana na ubora wake akiisaidia timu yake kuwa nafasi ya nne kwenye msimamo baada ya kucheza mechi tisa na kukusanya pointi 15 wakishinda mechi nne, sare tatu na kufungwa mechi mbili.

DICKSON JOB

Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi amekuwa na mabadiliko mengi kwenye kikosi chake kuna kipindi alimweka nje Bakari Mwamnyeto kabla ya kurejea kwenye kiwango chake lakini Job aliendelea kutumika kwenye kikosi cha kwanza hata kwenye nafasi ambazo hakuzoeleka kucheza kutokana na mahitaji ya timu.

Job ndiye beki bora kwa Yanga mbali kuibuka kwa Ibrahim Bacca mwishoni mwa msimu ambapo alionyesha kiwango cha juu, jamaa amekuwa akiupiga mwingi kiasi cha kuwa msaada upande wa beki ya kulia ambayo ilionekana kulegalega.

Kiasi Job sio beki wa pembeni eneo ambalo huwa anatumika Yao Yao lakini amekuwa msaada hasa kwenye michezo ambayo Gamondi alitaka kuwa na ukuta imara huku upande wa kushoto akicheza Joyce Lomalisa.

IBRAHIM ABDALLAH ‘BACCA’

Ni zao la KMKM visiwani Zanzibar alionwa na Yanga kwenye mashindano ya Mapinduzi na kuiwezesha timu hiyo kutwaa taji la Ligi Kuu, Kombe la ASFC na kuifikisha Yanga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, kiwango ambacho kilifanya aongezwe mkataba fasta.

Beki huyo kisiki amekuwa bora eneo hilo akimuweka nje nahodha Bakari Mwamnyeto ambaye sasa hana namba ya kudumu nafasi hiyo imekuwa ikichezwa mara kwa mara na Job na Bacca ambaye amekuwa na muendelezo wa ubora.

NATHANIEL CHILAMBO

Beki huyu wa kulia amekuwa kwenye kiwango kizuri msimu huu akiwa na kikosi cha Azam, jambo lililowashawishi viongozi wa timu hiyo kumuongezea mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia.

Licha ya ushindani wa nafasi kutokana na ubora wa mastaa mbalimbali, Chilambo amekuwa mzuri kutokana na uhodari wake wa kuzuia na kutengeneza mashambulizi.

Nyota huyu aliyejiunga na Azam akitokea Ruvu Shooting iliyoshuka daraja, ni miongoni mwa mabeki wa kulia wenye bao moja katika Ligi Kuu Bara msimu huu.

MOHAMMED HUSSEIN ‘TSHABALALA’

Anaweza kuwa miongoni mwa wachezaji ambao wamecheza michezo mingi zaidi kwenye ligi, ni mzuri kwenye kushambulia na kuzuia kama ilivyo kwa Kapombe.

Zimbwe Jr ni mchezaji kiongozi ambaye licha ya kuwa nahodha msaidizi amekuwa akitekeleza majukumu hayo kwa kiasi kutokana na John Bocco kutopata nafasi ya kutosha kwenye kikosi cha kwanza cha Simba.

Beki huyo wa kushoto amekuwa bora tangu kipindi kile ambacho Simba ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara misimu minne mfululizo hadi sasa. 

MZAMIRU YASSIN

Msimu huu Mzamiru Yassin anaonekana kupata changamoto kubwa kutoka kwa Fabrice Ngoma aliyesajiliwa msimu huu na Sadio Kanoute. Lakini hiyo haiondoi ukweli kwamba jamaa ni mwamba kwelikweli kwenye kiungo cha ulinzi akichapa kazi hadi kupachikwa jina moja maarufu la utani.

MUDATHIR YAHYA

Ni kiungo mchapakazi wa Yanga amesajiliwa dirisha dogo msimu uliopita akitokea KMKM ya Zanzibar tayari ametwaa taji moja la Ligi Kuu Bara na amejihakikishia namba katika kikosi cha kwanza.

Mudathir amecheza mechi tisa, ameifungia timu yake mabao mawili na kutoa asisti moja akicheza sambamba na kiungo fundi Khalid Aucho.

WAZIRI JUNIOR

Ni mshambuliaji mzawa ambaye amekuwa akiibuka na kupotea msimu huu akiichezea KMC ameifungia mabao matatu na aliibuka mchezaji bora wa mwezi Septemba.

Junior ambaye ni zao la Mbao amewahi kukipiga Yanga, Azam na sasa ni mshambuliaji wa kuaminiwa chini ya kocha Morin.

FEISAL SALUM

Kiungo fundi wa Azam FC msimu wake wa kwanza ndani ya timu hiyo akitokea Yanga amefunga mabao matano akianza na hat-trick dhidi ya Tabora United na alifunga bao moja dhidi ya Mashujaa timu yake ikiibuka na ushindi wa mabao 3-1.

Kiungo huyo ambaye amenunuliwa kwa dau nono kutoka Yanga amekuwa bora ndani ya kikosi cha Azam FC amejihakikishia namba kikosi cha kwanza akimfanya James Akaminko asubiri nje.

IDDI SELEMAN ‘NADO’

Winga wa Azam FC zao la Ndondo Cup amekuwa imara ndani ya timu hiyo licha ya wingi wa mastaa wa kigeni na tayari msimu huu ametupia mabao mawili.

Nado sasa amekosa uhakika wa namba kikosi cha kwanza tangu aliposajiliwa Djibril Sillah kutoka Raja Athletic ambaye pia wamefungana mabao na winga huyo mzawa akipachika mabao mawili dhidi ya Yanga na Mashujaa.

Sub: Metacha, Kijiri, Kibabage, Job, Lenny, Bajana, Kaseke, Andambwile, Maguri, Ajibu na Balua.

Kocha: Mohammed Abdallah ‘Baresi’ (Mashujaa), Zuberi Katwila (Mtibwa Sugar)

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: