Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hawa ni makocha wenye cv kubwa na hawana timu

Mgunda Pic Tanga Juma Mgunda.

Tue, 7 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wapo makocha wenye majina makubwa nchini yaliyotokana na CV zao, wengine walicheza soka kwa mafanikio makubwa, pamoja na hayo yote hawana timu wanazofundisha kama ilivyozoeleka.

Hapa tunakuchambulia makocha ambao wengi wamesoma na kupata madaraja ya juu lakini hivi sasa hawana timu za kufundisha.

Wapo wenye Leseni A ambapo awali walikuwa wachache, jambo hilo limekuwa rahisi chini ya uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia aliyetoa nafasi nyingi za makocha wazawa kujiendeleza.

ABDUL MINGANGE

Abdul Mingange ni meja mstaafu wa jeshi, ana Leseni A amewahi kuzinoa Ndanda FC, Njombe, Mbeya City na ameipandisha Ligi Kuu Bara, Mashujaa ya Kigoma.

Mbali na CV yake ni kocha mwenye misimamo wa kile anachokiamini.  Mingange anasema kwa sasa hajapata timu ambayo anahihitaji kutokana na levo yake ambayo ameifikia kwa sasa katika ufundishaji.

“Sijapata timu kubwa zinazokuja zote ni wa timu za chini, ikija ya Ligi Kuu sitakuwa na kikwazo, lakini kwa sasa nafanya shughuli zangu,” anasema.

JUMA MGUNDA

Wanamuita ‘Pep Guardiola Mnene’ ni mmoja kati ya makocha wazawa wenye Leseni A na mwenye uwezo wa kufundisha.

Mgunda amecheza na kuufundisha mpira kwa weledi mkubwa akiifundisha Coastal Union kwa muda mrefu hadi Simba ilipomnasa kusaidia benchi la ufundi.

Ujio wake Simba ulirejesha matumaini kwa wanachama na wapenzi wa wekundu hao kutokana na namna ambavyo alikirejesha kikosi katika hali ya kuridhisha.

Kwa sasa hana timu ya kuitumikia kama ilivyokuwa Simba na Coastal Union ambapo alikuwa na mmlaka makubwa katika benchi la ufundi kwa sasa ni mkurugenzi wa timu za vijana za Simba.

CHARLES BONIFACE MKWASA

Mkwasa ameupiga mwingi akiwa na Tumbaku ya Morogoro, Yanga na Timu ya Taifa.

Amezinoa timu mbalimbali ikiwemo Yanga na Ruvu Shooting, Tanzania Prisons.

Mkwasa anasema licha ya kupumzika kwa muda mrefu mpaka sasa hajaacha fani yake hiyo ambayo ameitumikia muda mrefu na anaipenda.

“Napenda kufundisha lakini sasa hivi sina timu nikiipata hakuna shida nitafundisha tu mimi ni kocha siwezi kuchagua timu yoyote nafundisha,”anasema.

JUMA MWAMBUSI

Kocha mwenye kipaji cha hali ya juu na uwezo wa kubaini na kukuza vipaji akizifundisha timu mbalimbali za ligi kama Mbeya City, Yanga, Azam, Ihefu na hata Timu ya Taifa ya Tanzania.

Mwambusi ana uwezo mkubwa lakini kwa sasa hauwezi kuamini kama hana timu ya kuifundisha.

Kwa sasa anasema ameamua kupumzika na kufanya majukumu mengine hususan kilimo lakini kukaa kimya huko sio kwamba kaacha kufundisha.

“Timu ikinihitaji na tukakubaliana sina shaka narejea kuifundisha maana hii ni fani yangu ambayo nimeisomea haiwezi kufa tu, nimepumzika sasa sio kwamba nimeacha,” anasema.

ABDALLAH KIBADENI

Umri nao unaweza kuwa kikwazo katika kuendelea na majukumu yake ya kufundisha kutokana na hekaheka za kuwafundisha vijana wa Kitanzania.

Kibadeni alicheza soka Simba na kuwa kocha mchezaji wa Majimaji miaka ya 70’ kwa nyakati tofauti amekinoa kikosi cha Simba na Timu ya Taifa. Ametoa mchango  mkubwa katika soka la Tanzania.

Kwa sasa hatumiki licha ya cv na uwezo mkubwa alionao ameamua kujikita katika majukumu mengine ikiwemo kusimamia kituo chake cha soka cha kukuza na kuibua vipaji kilichopo Chamazi ambacho anaamini kitawaibua kina Kibadeni wengine siku zijazo.

Anabainisha kuwa kwa sasa hana timu lakini ikitokea akapata ofa nzuri hatasita kutoa ujuzi wake kwa vijana.

“Timu ikija nafundisha bila ya kujali ikoje cha muhimu tukubaliane vizuri tu hakuna shida lakini kwa sasa nipo tu na majukumu yangu katika academy,”anasema.

JAMHURI KIHWELO ‘JULIO’

Mchezaji wa zamani wa Simba na ameifundisha katika nyakati tofauti, pia amewahi kuzifundisha Mwadui, Namungo, KMC na nyinginezo zinazoshiriki Ligi Kuu. Julio ni miongoni mwa makocha wazawa wenye cv kubwa na nzuri kutokana na wachezaji wengi kupita katika mikono yake. Ni kocha ambaye haoni shida kumchana mchezaji au kiongozi endapo atazingua au kuingilia majukumu yake sio mtu wa kukwepesha. Kwa sasa hana timu na yeye pia yuko na mambo yake mengine licha ya ukocha kuwa taaluma yake ambayo ameikalia darasani.

Julio anasema ameamua kupumzika tu na kufanya majukumu yake mengine yanayomuingizia kipato, ikitokea timu inayomuhitaji wakakubaliana hana shida ataendelea kufundisha.

MOHAMMED 'ADOLF’ RISHARD

Ni miongoni mwa makocha wazawa wenye uwezo mkubwa lakini cha kushangaza hana timu katika ligi zote zinazosimamiwa na TFF. Ni kocha asiyekuwa na mambo mengi lakini wachezaji hupenda kumwita Father kutokana na namna ambavyo anaishi nao awapo katika majukumu yake,

Mwanaspoti limemtafuta kutaka kujua sababu zilizomfanya kutoonekana kwenye soka kwa muda sasa licha ya ubora wake aliokuwa nao na alama aliyoiweka katika baadhi ya timu alizowahi kuzinoa ikiwemo Tanzania Prisons, Polisi Morogoro. Anasema hataki timu zenye presha.

“Unajua kuna timu ukijiunga nayo kila kitu kinakuangalia wewe wakati unazisaidia, zinakuja lakini sijaona za kufanya nazo kazi ikitokea nikaiona nitafanya tu,”anasema.

Hachagua daraja la kufundisha lakini za Ligi Kuu na Championship ni nzuri zaidi kwake.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live