Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hawa ndiyo nyota watano Yanga waliowalaza na viatu Belouizdad

Yanga 4 WA0024 Hawa ndiyo nyota watano Yanga waliowalaza na viatu Belouizdad

Mon, 26 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Klabu ya Yanga ndio timu ya kwanza ya Tanzania kucheza robo fainali (au Top 8) ya Ligi ya Mabingwa Afrika ilipofanya hivyo mwaka mara mbili mfululizo 1969 na 1970 lakini hiyo ni kabla ya michuano hiyo kubadilishwa mfumo na kuanza kutumika huu wa sasa mwaka 1997.

Katika mfumo wa sasa, Yanga imeingia kwenye vitabu vya historia juzi baada ya kutinga robo fainali ya michuano hiyo kwa mara ya kwanza baada ya kuwafunga mabingwa mara nne mfululizo wa Ligi Kuu ya Algeria klabu ya CR Belouizdad kwa mabao 4-0 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Mchezo huo nje ya uwanja ulitangazwa kuwa ni Pacome Day (Kitaalamu Zaidi) ikiwa ni kuenzi au kutambua mchango wa nyota wao wa kimataifa kutoka Ivory Coast, Pacome Zouzoua.

Ndani ya mchezo Yanga walionekana kuwa bora katika kila idara uwanjani na pongezi nyingi ziende kwa kocha mkuu wa kikosi hicho, Miguel Gamondi ambaye amekiandaa vyema kikosini.

Wachezaji takribani wote walikuwa katika viwango vyao vya hali ya juu lakini kwa Mwanaspoti, linakuletea mastaa watano waliokuwa mwiba zaidi kwa CR Belouizdad kutokana na namna walivyowapa shida wapinzani wao.

PACOME ZOUZOUA Ni kiungo ambaye alikabidhiwa mchezo huu na hakika hakuwaangusha mashabiki na watu wote walioamua kumpa heshima hiyo.

Baada ya mchezo huo, bila ya shaka jina la Zouzoua litaendelea kusalia kwenye vinywa vya timu ya CR Belouizdad kwa muda mrefu kutokana na kile ambacho alikuwa anawafanyia uwanjani.

Profesa wa Boli, Pacome alikuwepo kila mahali uwanjani. Kulia ama kushoto, popote ambapo alikuwa anaamua kucheza Zouzoua alikuwa anawapa matatizo mengi wapinzani na alitengenezaa nafasi nzuri za kufunga.

Bao la tatu alilofunga Kennedy Musonda lilikuwa ni mfano wa kazi nzuri ya Zouzoua katika mchezo huo maalumu uliotolewa kwa ajili yake.

Kabla ya kutoa asisti hiyo kwa Musonda, alimlambisha nyasi beki mmoja, kisha akamlaza sakafuni mara mbili kipa wa Belouizdad, Alexis Guendouz halafu akaupitisha mpira katikati ya mabeki kadhaa ukamkuta mfungaji akiwa peke yake na kuweka wavuni mpira katika lango tupu. Katika mechi tano za michuano hii, Pacome amehusika katika mabao matano, akifunga matatu na kutoa asisti mbili.

Kiungo mshambuliaji wa Yanga  Pacome Zouzoua akikabwa na wachezaji wa Belouizdad Uwanja wa Mkapa. Picha na Loveness Bernard

IBRAHIM ABDALLAH 'BACCA' Beki kisiki au chuma ni baadhi ya majina waliyompa mashabiki wa Yanga kutokana na ubora alionao sasa na kwenye mchezo huo alikuwa imara akimlinda kipa wake Djigui Diarra.

Yanga walitakiwa wasiruhusu bao na kweli walifanikiwa lakini isingekuwa rahisi kama si kazi kubwa aliyofanya Bacca katika eneo la ulinzi. Bacca alijitoa bila kuchoka kwa ajili ya kuhakikisha kipa Diarra anakuwa salama na nyavu zake haziguswi.

Unaweza ukasikia 4-0 ukahisi pengine ilikuwa mechi ya upande mmoja lakini si hivyo kuna muda iliwalazimu Yanga kushikilia bomba kwelikweli kwani kuruhusu walau bao moja tu kwenye mchezo ule kungebadili taswira nzima iwe tofauti kabisa.

KHALID AUCHO Mashabiki wa Yanga wanamuita Daktari wa Mpira ndiye muhimili wa kiungo cha timu hiyo, ndio mtu anayeamua mapigo yote ya uchezaji ndani ya kikosi cha Yanga na namna ya kuwakabili wapinzani wao.

Aucho alikuwa kila sehemu ya uwanja aliyohitajika ili kutoa msaada na kazi hiyo aliifanya kwa ustadi wa hali ya juu mno kwa kuanzia kukaba na kutoa pasi za uhakika.

Alianzisha mashambulizi kwa haraka na pale alipohijika kupooza mpira alifanya hivyo ambapo Yanga ilianza kuwatafuta Waarabu kwa bao la kipidi cha kwanza la Mudathir Yahya na kuwasababishia kocha wao atake kupigana na wachezaji kwenye benchi lao kwa bao la nne lililowasambaratisha kabisa lililowekwa nyavuni na mtokeabenchini, Joseph Guede.

MUDATHIR YAHYA Apewe maua yake hiyo ni moja ya kauli zinazozungumzwa sana kwa sasa kwa wale wanaotazama anachokifanya uwanjani staa kutoka Zanzibar, Mudathir Yahya.

Kwa siku za hivi karibuni Mudathir amekuwa sio tu mpambanaji kama wengi walivyomzoea bali amekuwa ni mfungaji wa mabao muhimu kwenye mechi muhimu kwa timu yake.

Licha ya kuwa Yanga ilifunga mabao manne kwenye mchezo huo, lakini bila shaka bao la Mudathir linaweza kuwa ndio lilikuwa muhimu zaidi katika kuamsha morali ya mchezo huu.

Yanga haikupaswa kufika mapumziko bila bao baada ya kushambulia mfululizo huku nyota wake wakipoteza nafasi baada ya nafasi ya kuwafunga CRB. Shukrani kwa kiungo aliye katika ubora wa juu, Mudathir, ambaye alifunga bao lake la tano katika mechi zake tano alizocheza katika michuano yote.

Hakika bao hilo ndio lilikuwa funguo ya mabao mengine katika mchezo huo na ndio maana hadi sasa tukiwa tunajadili haya, Yanga ipo robo fainali.

STEPHAN AZIZ KI Ni mfungaji wa bao moja katika mchezo na 'asisti' moja safi kwenda kwa Guede ambaye alifunga bao la nne. Aziz Ki amekuwa akifanya hivyo kwenye ligi na hata kwenye michuano ya kimataifa kama hivi.

Ni mchezaji ambaye anaweza kucheza mechi za aina hii ambazo zinavuta hisia za watu wengi ama unaweza kusema ni mchezaji wa mechi kubwa. Kama angetulia, siku ile alikuwa na 'hat-trick' yake dhidi ya Belouizdad.

Mbali na wachezaji hao watano lakini pia wapewe maua yao nyota wote waliocheza mechi ile ambao walivuja jasho kikwelikweli ili kuanzika historia kama Kouassi Yao, Dickson Job, Maxi Nzengeli na Kennedy Musonda na Guede ambaye bao lake limeifanya Yanga kufuzu robo fainali na kuandika historia mpya kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: