Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hawa ndio kiboko ya Benchikha

Benchikha Mapinduzi.jpeg Hawa ndio kiboko ya Benchikha

Fri, 8 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kocha Mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha ameondoka nchini kwenda Algeria kubrashi taaluma aliyonayo, akiwa ameiongoza timu hiyo katika mechi 15 za michuano yote kuanzia Ligi Kuu Bara, Kombe la ASFC na Ligi ya Mabingwa Afrika alikotinga robo fainali, lakini imebainika kuwa mastaa wawili wa timu pinzani wamemtibulia na kuonekana ndio kiboko ya kocha huyo.

Kocha huyo aliyeajiriwa na kutambulishwa na Simba Novemba 28 mwaka jana, ameiongoza kwenye mechi nane za Ligi Kuu Bara akipoteza mchezo mmoja tu, kama ilivyo kwenye Ligi ya Mabingwa aliyoiongoza katika michezo mitano huku katika Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) Wekundu hao wakiwa chini yake wameshuka uwanjani mara mbili tu.

Katika mechi hizo nane za Ligi Kuu rekodi zinaonyesha Simba imeshinda mechi tano, kutoka sare mbili na kupoteza mchezo mmoja ambao ni wa juzi mbele ya Tanzania Prisons iliyowalaza kwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Jamhuri, mjini Morogoro yote yakiwekwa kambani na nyota wa maafande hao Samson Mbangula.

Kwenye michezo ya CAF ambayo Simba imetinga robo fainali kwa kishindo kupitia Kundi B, ilipoteza mechi moja tu mbele ya Wydad CA ya Morocco, huku ikitoka sare mbili na kushinda mbili mbele ya Wydad na Jwaneng Galaxy ya Botswana waliyoifumua kwa mabao 6-0 na kufuzu robo fainali ikiwa ni mara ya nne katika misimu sita ya michuano ya CAF.

Mechi mbili za ASFC, Benchikha ameiongoza timu hiyo kushinda zote ikianza kuinyoosha Tembo FC kwa mabao 4-0 katika hatua ya 64 Bora na kufuzu 32 Bora ambapo iliicharaza TRA Kilimanjaro kwa mabao 6-0 na kufuzu 16 Bora sasa ikisubiri kukabiliana na Mashujaa ambayo inatarajiwa kuvaana nayo Machi 15 kwenye Ligi Kuu Bara.

Sasa kama hujui ni kwamba kuna wachezaji wawili tu kupitia mechi hizo ndizo walizoweza kumtungua Benchikha kwa mabao mawili ndani ya mchezo mmoja, ikiwa ni sawa na ilivyomtokea pia mtangulizi wake, Roberto Oliveira 'Robertinho' aliyefutwa kazi Novemba 6 saa chache baada ya Simba kufumuliwa mabao 5-1 na Yanga katika Derby ya Kariakoo.

ALIANZIA HAPA

Kidume cha kwanza kumkaribisha Benchikha nchini kwa kugusa nyavu za Simba mara mbili alikuwa ni Wazir Junior wa KMC katika pambano lililokuwa la pili kwa kocha huyo tangu aanze kuinoa timu hiyo ambalo liliisha kwa sare ya 2-2 lililopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex siku ya Desemba 23 mwaka jana.

Kabla ya hapo, Benchikha alianza na mguu mzuri kwa kupata ushindi wa mabao 3-0 mbele ya Kagera Sugar katika mechi ya kwanza kuiongoza timu hiyo katika Ligi Kuu Bara, iliyopigwa Desemba 15 kwenye Uwanja wa Uhuru kwa mabao ya Saido Ntibazonkiza, Sadio Kanoute na nahodha John Bocco.

Ndipo siku chache kabla ya sherehe za Krismasi, Wazir Junior alipofanya yake na kuandika historia ya kuwa mchezaji wa kwanza kuifunga Simba ya Benchikha mabao mawili katika mechi moja katika mchezo ulioisha kwa sare ya 2-2, huku wenyeji KMC wakiupiga mpira mwingi pale Chamazi.

Wazir alianza kwa kufunga bao dakika 31 kabla ya Simba kulichomoa kwa penalti dakika ya 57 kisha Jean Baleke ambaye ameondoka klabuni hapo kupitia dirisha dogo la usajili aliongeza chuma cha pili dakika mbili baadaye na kuonekana kama wamepoteza tena mchezo mbele ya Simba ambayo haijawahi kuifunga tangu ipande daraja.

Hata hivyo, wakati mashabiki wa Simba wakiamini wamemaliza kazi, Wazir Junior aliwakata stimu kwa kutupia bao la pili na lililokuwa la kusawazisha katika dakika ya 88 na hadi filimbi ya mwisho inalia matokeo yalikuwa ni sare ya 2-2.

AFANDE AMMALIZA

Simba ikiwa imetoka kufanya mauaji ya kimbari mbele ya Jwaneng katika mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika wikiendi iliyopita, ilirejea kupiga mzigo wa Ligi Kuu Bara juzi jioni kwenye Uwanja wa Jamhuri kwa kuialika Tanzania Prisons na afande Samson Mbangula akamtibulia tena baada ya matokeo mazuri ikiwa chini ya Benchikha.

Mbangula alifunga bao la kwanza katika dakika ya 45 kutokana na kuwahi mpira na kukimbia nao kwa umbali mrefu kabla ya kumtungua Aishi Manula aliyechelewa kutoka langoni kumkabili na bao hilo lilidumu hadi mapumziko.

Kipindi cha pili Mbangula aliingia kwenye rekodi ya kuwa mchezaji wa pili kukifunga kikosi cha Simba mabao mawili ndani ya mechi moja kwa kuongeza bao la pili dakika ya 62 akiwalamba chenga na kuwagaragaza mabeki wa kati, Henock Inonga na Kennedy Juma kabla ya kumpiga tobo kipa Manula kuiandikia Prisons bao la pili.

Simba ilijitutumua na kupata bao la kufutia machozi lililowekwa kimiani na kiungo Fabrice Ngoma dakika ya 88.

BAO LA TANO

Mabao hayo mawili ya Mbangula yalimfanya afikishe jumla ya mabao matano ambayo Simba ya Benchikha imeyaruhusu katika mechi nane za Ligi Kuu Bara, lakini yakimfanya nyota huyo wa Prisons kufikisha mabao sita katika mechi tano mfululizo zilizopita.

Mbangula hakufunga katika mechi ya kwanza tangu kurejea kwa ligi hiyo iliyosimama kwa miezi miwili kupisha Kombe la Mapinduzi 2024 na Fainali za Afcon 2023, lakini mechi tano zilizofuata amefunga mabao sita, likiwamo moja moja alitupia dhidi ya Namungo, Singida FG, Azam FC na Tabora United na kisha juzi akafunga mawili kufikisha jumla ya mabao saba kwa msimu huu akichuana na mastaa wa klabu nyingine kubwa.

Kasi ya ufungaji wa mabao imemfanya Mbangula kuwafunika hadi kinara wa orodha ya wafungaji, Feisal Salum wa Azam, Mudathir Yahya wa Yanga na nyota wa Simba, Clatous Chama ambao kwenye mechi sita za timu zao zilizopita licha ya kufunga mabao, lakini hawajamfikia afande huyo wa Prisons.

Muda amefunga jumla ya mabao manne kwenye mechi hizo sita zilizopita, huku Fei anayeongoza orodha ya wafungaji akiwa mabao 12, ametupia matatu tu wakati Chama aliye na mabao matano hadi sasa akifunga mawili tu ndani ya mechi sita zilizopita za ligi.

Mudathir alifunga dhidi ya KMC (mawili) na Mashujaa alipotupia moja sawa na Dodoma Jiji, huku Feisal akiweka mawili dhidi ya Dodoma Jiji na moja kwa Prisons, wakati Chama, kipenzi cha mashabiki wa Wekundu katika michezo sita zilizopita alifunga bao moja dhidi ya JKT Tanzania sawa na alivyofanya dhidi ya Azam zilizotoka sare ya 1-1.

Kwa upande wa mechi za kimataifa, Benchikha amefungwa bao moja tu walipolala 1-0 mbele ya Wydad, kwani ilitoka suluhu dhidi ya Jwaneng ugenini kisha kushinda 6-0 nyumbani mbele ya wapinzani hao na kutoka pia suluhu nyingine ugenini waliporudiana na Asec Mimosas, lakini wakiinyuka Wydad mabao 2-0 ziliporudiana jijini Dar es Salaam.

Katika mechi za Kombe la Shirikisho (ASFC) Simba ya Benchikha haijaruhusu bao hata moja katika mechi mbili ilizocheza hadi sasa.

HATA ROBERTINHO

Rekodi ya Benchikha kufungwa mabao mawili msimu huu katika mechi moja pia ilimkumba mtangulizi wake, Roberto Oliveira 'Robertinho' ambaye naye alitunguliwa na wachezaji wawili tofauti kabla ya kibarua chake kuota nyasi baada ya Kariakoo Derby.

Mchezaji wa kwanza kumzingua Robertinho msimu huu alikuwa ni Matteo Antony wakati akiwa Mtibwa Sugar katika pambano la kufungulia msimu uliopigwa Agosti 18, mwaka jana kwenye Uwanja wa Manungu Complex, Morogoro na Simba kushinda mabao 4-2.

Matteo alifunga mabao yote mawili ya Manungu yakiwa ni ya kuchomoa kwani wageni walianza kutupia kambani katika mchezo huo uliokuwa mkali. Nyota huyo ambaye kwa sasa anakipiga JKT Tanzania, alitumia dakika mbili tu kuchomoa mabao ya Jean Baleke na Willy Onana waliofunga katika dakika ya 5 na 9, akiyatupia katika dakika ya 20 na 22, kisha Fabrice Ngoma akifunga bao la tatu dakika 45 na Clatous Chama kuongeza la nne dakika ya 81.

Kisha, Maxi Nzengeli wa Yanga naye akafanya yake kwenye Kariakoo Derby iliyomfukuzisha kazi Robertinho wakati Simba ikilala kwa mabao 5-1. Kennedy Musonda aliitanguliza Yanga kwa bao la mapema la dakika ya tatu tu, kabla ya Kibu Denis kuchomoa katika dakika ya tisa na kufanya pambano hilo liende mapumziko matokeo yakiwa ni sare ya 1-1, ndipo katika kipindi cha pili mvua ya mabao ilinyesha kwa Mnyama kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Maxi alifunga bao la tatu na la kwanza kwake kwenye mchezo huo katika dakika ya 64 kabla ya Stephane Aziz KI kuongeza la tatu katika dakika ya 73 na wakati Simba ikijiuliza jinsi ya kuyarejesha mabao hayo, kiungo mshambuliaji huyo anayemudu pia kucheza kama winga akaongeza la nne na lililokuwa la pili kwake na bao la tano likawekwa kimiani na Pacome Zouzoua kwa mkwaju wa penalti.

Kipigo hicho kiliwachefua mabosi wa Simba na saa chache baadaye wakatangaza kumuachisha kazi kocha Robertinho ambaye juzi alikaririwa na Mwanaspoti akisema kama kuna mtu aliyemtibulia wala sio Maxi, bali ni Pacome aliyemtaja kama nyota aliyewavuruga akishirikiana wenzake katika pambano hilo na Simba kuchapwa mabao hayo matano.

Hicho kilikuwa kipigo cha kwanza kizito zaidi kwa Simba kutoka kwa Yanga tangu ilipofumuliwa mabao 5-0 mwaka 1968 na kulipa kisasi kwa watani wa jadi hao katika mechi ya mwaka 1977 waliifumua timu ya Wananchi mabao 6-0 na kuongeza kipigo kingine Mei 6 mwaka 2012 Yanga iliponyooshwa mabao 5-0 Kwa Mkapa

Chanzo: Mwanaspoti