Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hawa ndio Power Dynamos, wapinzani wa Simba SC Agosti 6

Power Dynamos August Kikosi cha Power Dynamos

Fri, 4 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Simba imetangaza rasmi itacheza na Power Dynamos ya Zambia katika kilele cha tamasha lao la ‘Simba Day’ litakalofanyika Jumapili hii ya Agosti 6, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Mwanaspoti linakuletea Makala ya historia fupi juu ya wapinzani hao watakaonogesha tamasha hilo na kuwapa raha mashabiki watakaohudhuria siku hiyo.

HISTORIA YAO

Power Dynamos ambao ndio mabingwa wa Ligi Kuu Zambia msimu uliopita, ilianzishwa rasmi Januari Mosi mwaka 1971 hivyo imetimiza miaka 52 tangu kuanzishwa kwake tofauti na wapinzani wao Simba wenye miaka 87.

Timu hiyo yenye maskani yake huko Kitwe hucheza Ligi ya MTN/FAZ Super Division ikijizolea umaarufu mkubwa kwa mashabiki kutokana na aina nzuri ya uchezaji wake wa soka safi la kuweka chini mpira ambao huvutia sana.

Mwaka 1991 ilikuwa ni klabu ya kwanza kutokea Kusini mwa Afrika kushinda ubingwa wa mabara baada ya kushinda Kombe la Washindi.

UWANJA WANAOTUMIA

Timu hii inatumia Uwanja wa Arthur Davies uliopo huko Kitwe Zambia ambao una uwezo wa kuingiza mashabiki 12,000.

Uwanja huu uliitwa jina la Arthur Davies ambaye alikuwa Mwamuzi wa FIFA na Mwanachama wa Chama cha Soka cha Zambia.

MATAJI SABA

Kwenye Ligi ya Zambia, Power Dynamos imetwaa mataji saba kuanzia 1984, 1991, 1994, 1997, 2000, 2011 na 2023 huku Kombe la Ligi (Zambia Cup) ikitwaa pia mara saba ikianzia 1979, 1980, 1982, 1990, 1997, 2001 na 2003.

Ngao ya Jamii (Zambian Charity Shield) imechukua mara sita ikianza 1998, 2004, 2009, 2012, 2013, 2016 wakati Kombe la Zambia Challenge imechukua mataji mawili tu kuanzia mwaka 1990 huku mara ya mwisho ikiwa ni 2001.

ABSA imelichukua mara mbili 2009, 2011, Kombe la Coca-Cola moja 2003 na Kombe la Zambia Barclays mwaka 2009 na 2011.

SIO MARA YA KWANZA

Hii sio mara ya kwanza kwa miamba hii kucheza na Simba kwenye tamasha la Simba Day kwani ilishawahi kukutana mwaka 2019.

Mwaka huo Simba ilishinda mabao 3-1 yaliyofungwa yote na aliyekuwa nyota wa timu hiyo, Meddie Kagere dakika ya 3, 58 na 73 na kuweka rekodi ya mchezaji wa kwanza kwenye tamasha hilo kufunga mabao matatu ‘Hat-Trick’.

WAPINZANI WAKE

Wakati mpinzani wa Simba nchini akiwa ni Yanga kwa upande wa Power Dynamos wapinzani wao wakubwa ni Nkana FC na Zesco United FC.

KOCHA MKUU

Timu hii inanolewa na Kocha Mkuu, Mwenya Chipepo aliyeipatia ubingwa wa nchi hiyo msimu ulioisha kwa mara ya kwanza tangu 2011.

Chipepo aliichukua timu hiyo Oktoba 7, 2021 baada ya Masautso Tembo kutimuliwa kutokana na mwenendo mbaya wa matokeo.

REKODI YA CAF

Kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, Power Dynamos imeshiriki mara tatu tu na mwaka 1998 na 2012 iliishia hatua ya pili huku 2001 ikishindwa kufanya vizuri zaidi baada ya kutolewa mapema katika mzunguko wa kwanza.

Kombe la Washindi Afrika kabla ya kuunganishwa na kuitwa Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2004, iliishia pia hatua ya pili mwaka 1985 na iliposhi-riki tena kwa mara nyingine mwaka 1995 haikufua dafu na kutolewa raundi ya kwanza.

Rekodi zinawabeba zaidi katika michuano hii ya Kombe la Washindi kwani ilifika robo fainali mara nne mwaka 1981, 1986, 1999 na 2003 huku ikiishia kutolewa hatua ya pili mara tatu ikianza 1988, 1989 na 1992. Mwaka wa kihistoria kwao ni ilipotwaa ubingwa wa michuano hiyo 1991 ilipoifunga BCC Lions ya Nigeria kwa jumla ya mabao 5-4.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live