Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hawa ndio Azam bana

Novatus+pic Novatus Dismas akisaini Azam FC (picha na maktaba)

Sat, 1 Apr 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Achana na matokeo yaliyoiweka pabaya Taifa Stars kwenye mbio za kwenda fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon), zitakazofanyika mwakani nchini Ivory Coast, mabosi wa Azam wamejivunia namna akademia yao ilivochangia wachezaji kibao kwenye kikosi hicho cha taifa.

Stars ilicharazwa bao 1-0 na Uganda The Cranes katika mechi ya Kundi F iliyopigwa Jumanne Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku asilimia kubwa ya wachezaji walioitumikia timu hiyo wakiwa ni zao la Akademi ya Vijana ya Azam FC na Kocha wa timu hiyo, Kally Ongala alisema ni heshima kwa klabu yao na kwamba anaamini matunda ya kile kilichowekezwa na matajiri hao kinaendelea kulipa.

Katika kikosi cha Stars kinachoongozwa na kocha Adel Amrouche kilianza na takribani wachezaji watano walioibuliwa na kukuzwa au kuitumia Azam akiwamo Simon Msuva, kipa Aishi Manula na kiungo Mudathir Yahya ambao walipita akademi hiyo kati ya 2009-2011, Novatus Dismas aliyejiunga mwaka 2016-2020 kisha kwenda Israel na baadae kucheza Ubelgiji hadi sasa, Mohamed Hussein aliyeitumikia 2010 kisha kwenda Simba na nyota Himid Mao aliyejiunga mwaka 2008 kabla ya kutimkia Misri mwaka 2018.

Kocha Kally akilizungumzia hilo alisema kama mmoja wa makocha wa Azam aliyewanoa wachezaji hao anajivunia kuona vipaji walivyovikuza vikileta matokeo chanya sio tu kwa klabu hiyo bali hata kwa taifa. Msuva ndiye aliyefunga bao pekee kwenye mechi ya kwanza dhidi ya Uganda iliyochezwa nchini Misri wikiendi iliyopita.

Kally alisema uwepo wa akademi hiyo unasaidia kulitangaza taifa kwa upande wa soka kwani kuna wachezaji wamepita hapo na wanafanya vizuri nje ya nchi huku akisisitiza jambo hilo ni endelevu.

"Ukweli haudanganyi, hii  inaonyesha wazi kabisa waliopita hapa wameenda kutuwakilisha vyema na kuonesha vipaji vyao kimataifa na kama timu itaendelea kuwepo basi tutahakikisha tunawakuza vijana kwa namna hiyo," alisema Kally   

Kocha huyo aliyewahi kuzichezea Abajalo, Yanga na Azam kabla ya kugeukia ukocha, kwa sasa ni kocha msaidizi akiwa pia ndiye kocha wa washambuliaji wa timu hiyo inayoshika nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu Bara na ikitinga robo fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC).

Chanzo: www.tanzaniaweb.live