Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hawa nao kuliamsha Ligi Kuu Bara 2024/25

Dstrfyugg Hawa nao kuliamsha Ligi Kuu Bara 2024/25

Thu, 15 Aug 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Msimu mpya wa Ligi Kuu Bara unaanza rasmi leo kila timu ikianza hesabu mpya ikiwania pointi 90 za michezo 30 inayopatikana ndani ya msimu mmoja.

Kila timu ilikuwa na muda wa zaidi ya siku 30 za kujipanga kwa kusajili vikosi vyao pamoja na kuboresha mabenchi yao ya ufundi tayari kwa msimu mpya ambao rasmi utafunguliwa leo.

Kwenye maboresho hayo, kila timu imefanya yake na wafuatao ni makocha wapya tisa kwenye timu zao mpya zitakazoshiriki ligi msimu huu.

Fadlu Davids-Simba

Simba itakuwa chini ya kocha wao mpya, Msauzi Fadlu Davids ambaye ametua klabuni hapo akitokea kwa mabingwa wa Morocco, Raja Athletic aliyokuwa anaitumikia kama kocha msaidizi.

Kocha huyo aliyezaliwa miaka 43 iliyopita, mara ya mwisho kufanya kazi kama kocha mkuu ni akiwa Maritzburg United ya Afrika Kusini na aliiongoza kwenye michezo 85 lakini hakuwahi kuchukua ubingwa wowote mkubwa.

Fadlu anatua Simba yenye kiu na presha kubwa ya mataji akitakiwa kurudisha hadhi yake akiwa ameshapoteza taji la kwanza la ngao ya jamii alilolikuta linashikiliwa na wekundu hao.

Francis Kimanzi-Tabora United

Kocha huyu mkongwe Mkenya amepewa mkataba wa mwaka mmoja na Tabora United iliyonusurika kushuka daraja msimu uliopita, ikiponea kwenye Playoff.

Kimanzi sio kocha mdogo, ana leseni kubwa ya Uefa Pro, akiwa pia mkufunzi wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) atakuja kuanza maisha mapya na 'nyuki' hao wa Tabora.

Kocha huyo atakayesaidiwa na Mkenya mwenzake, Yusuf Chipo, amewahi kuzifundisha klabu kadhaa za Kenya zikiwemo Wazito, Mathare United na Sofapaka, pia kaifundisha timu ya Taifa hilo kwa nyakati tofauti.

Paul Nkata-Kagera Sugar

Baada ya kuachana na kocha mzawa Fred Minziro, Kagera Sugar imerejea tena Uganda safari hii ikimchukua kocha mkongwe Paul Nkata.

Nkata (64) ni kocha mzoefu Afrika Mashariki akija kuifundisha timu hiyo iliyowahi kufundishwa na Mganda mwenzake Jackson Mayanja.

Rekodi kubwa kwa Nkata amewahi kufundisha Tusker ya Kenya kwa mafanikio akiwapa ubingwa wa Ligi Kuu humo na sasa atakuwa na kibarua cha kurudisha makali ya wakata miwa hao wa Kagera.

Patrick Aussems-Singida Black Stars

Baada ya kuipa mafanikio makubwa Simba kisha kutimka nchini, Kocha Aussems anarejea Tanzania safari hii akitua Singida Black Stars.

Aussems (59) raia wa Ubelgiji inawezekana akawa ndiye kocha kinara mwenye rekodi kubwa ya mafanikio akiwahi kuchukua taji la Ligi Kuu Bara pamoja na kuifikisha Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika Simba na sasa anatua Singida kuibadilisha historia ya mafanikio yao ikiwa haijawahi kuchukua ubingwa wowote.

Mohammed Muya- Fountain Gate FC

Baada ya kujibadilisha jina kwa iliyokuwa Singida Fountain Gate na sasa kuitwa Fountain Gate FC wanaingia msimu mpya ikiwa chini ya kocha mzawa Mohammed Muya atakayesaidiwa na mzawa mwingine Mohammed Laizer.

Muya amewahi kuwa ligi kuu bara lakini akifanya kazi kama kocha msaidizi, anatua Fountain Gate kuja kusaka mafanikio akiwa kocha mkuu wa timu hiyo akiwahi kupita Dodoma Jiji kama kocha msaidizi.

Hamady Ally-JKT Tanzania

Baada ya kuibadili Tanzania Prisons na kuitoa kwenye eneo la kushuka daraja mpaka kumaliza nafasi ya tisa kwenye msimamo wa ligi msimu uliopita, Ally safari hii anahama kambi moja ya Jeshi la Magereza na kutua Jeshi la Kujenga Taifa JKT.

Mabadiliko ya Prisons msimu uliopita yalimjengea heshima kubwa kocha huyo na JKT Tanzania kuamua kumsomba baada ya kumtema aliyekuwa kocha wao Malale Hamsini.

JKT baada ya kunusurika kushuka daraja akili ya kurudisha makali yao, itahitaji ufundi mkubwa wa Ally ambaye hajawahi kuchukua taji lolote ndani na hata nje ya nchi.

Mecky Maxime-Dodoma Jiji

Kocha Mecky Maxime sio kocha mgeni kwenye soka la Tanzania lakini msimu ujao tutamuangalia akiwa na Dodoma Jiji ya makao makuu ya nchi.

Maxime anatua Dodoma akitokea Singida Black Stars iliyokuwa inatumia jina la Ihefu msimu uliopita akiwa na kazi maalumu ya kuitafutia nafasi kubwa timu hiyo ambayo haijawahi kumaliza kwenye nafasi nne za juu ya ligi.

Maxime hajawahi kuchukua taji lolote la ligi akiwa kama kocha na atakuwa na kibarua kipya kwa Dodoma ambayo nayo haina taji lolote nchini.

Fikiri Elias-KenGold

Ken Gold iliyopanda Ligi Kuu Bara imempa ajira kocha mzawa Fikiri kuwa kocha wao mkuu kwa msimu huu.

Kocha huyo ambaye amewahi kufanya kazi Coastal Union ya Tanga, hana jina kubwa sana kwa kuwa hakuwahi kufanya makubwa sana ndani ya ardhi ya Tanzania akiwa hajawahi kuchukua taji lolote.

Goran Kopunovic-Pamba

Pamba ya Mwanza imerejea Ligi kuu na kujipanga kwao ikamchukua kocha Mserbia Goran Kopunovic ambaye sio mgeni sana kwenye soka la Tanzania kwani msimu uliopita aliifundisha Tabora United.

Goran hajawahi kuchukua taji lolote nchini lakini amewahi kuifundisha Simba kwa miezi sita iliyomaliza nafasi nne za juu.

Chanzo: Mwanaspoti