Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hawa jamaa ni watu wa kazi kweli

Ngoma Baleke.png Hawa jamaa ni watu wa kazi kweli

Wed, 4 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Hakuna siri, kuna wakati usajili unaofanywa na baadhi ya timu unatia mashaka. Fikiria tu usajili kama uliofanywa msimu uliopita na Simba na Yanga kwa wachezaji kama Ismael Sawadogo, Victor Akpan, Nelson Okwa, Mamadou Doumbia, Gael Bigirimana na hata kumrejesha Heritier Makambo na Tuisila Kisinda ulivyokuwa wa mashaka.

Wapo baadhi ya wachezaji wanasajili wakiwa tayari wamezeeka na nguvu zimeanza kupungua au wanasajili wakiwa ni majeruhi wa kudumu au huwa hawajacheza kwa muda mrefu, kiasi wanakuja kuonekana kama wafanyakazi hewa kwenye vikosi vya timu zinazowasajili kwa mikataba minono.

Usajili makini hautakiwi kuwa wa mashaka. Mchezaji anatakiwa asajiliwe wakati uwezo wake unaonekana wazi na hata akishindwa awe ameshindwa mwenyewe, isiwe kwa sababu kulikuwa na mashaka fulani ndani yake.

Kibaya zaidi ni kwamba mashabiki na hata mabosi wa klabu huwa hawana muda wa kumvumilia mtu, wanataka mchezaji akisajiliwa gari liwake mara moja na sio kusubiri achanganye huko mbele.

Hata katika usajili wa nyota wa kigeni uliofanyika msimu huu kuna ambao tayari wanatia mashaka na wengine huwezi kushawishika kuwa watafanya vizuri huko mbele, japo watu wanawavutia pumzi, lakini kuna wengine wameanza na moto kuonyesha ni sajili bomba zilizofanywa kwa umakini. Makala hii inakuletea orodha ya baadhi ya nyota wa kigeni ambao usajili wao hauna mashaka yoyote na unaweza hata kusema kwa kinywa kipana kwamba jamaa wamenoga na ni watamu kinoma.

Che Fondoh Malone - Simba

Ni bonge la beki kutoka Cameroon, ana nguvu, ana kasi na uwezo mzuri wa kukaba sambamba na kumiliki mpira kwa kujiamini. Mchezaji mzuri anahitaji kitu gani zaidi ya hivyo? Huyu jamaa kwa sasa ameshikilia roho na ukuta wa Simba akiwa sambamba na Henock Inonga.

Huwezi kuwaambia kitu wanasimba juu ya beki huyo aliyesajiliwa kutoka Cottonsport kwa sababu ametua kikosini na kuonyesha uimara wake, japo ana udhaifu wake wa kujiamini kupita kiasi ambapo kama atakutana na washambuliaji wajanja anaweza kuiponza timu uwanjani.

Fabrice Ngoma - Simba

Kiungo mmoja matata anayejua kukaba na kukata umeme pale anapoisi kuna hitilafu inataka kutokea. Ndiye namba sita aliyewachanganya mashabiki wa Yanga waliokuwa wakimvizia kisha kuibua Msimbazi.

Ngoma aliyesajiliwa kutoka Al Hilal ya Sudan ni mchezaji ambaye huna shaka naye kwa aina ya uchezaji na umahiri alionao uwanjani akicheza kama kiungo mkabaji kwa sababu ya uimara alionao na kusambaza mipira kwa haraka mbali na kusogea eneo la mbele kuongeza idadi ya washambuliaji.

Aubin Kramo - Simba

Kama sio kupata majeraha ya kila mara, kiasi cha kuwachanganya hata mabosi wa klabu ya Simba, lakini jamaa ni fundi hasa na mchezaji mwenye faida kubwa kwa timu hiyo kutokana na kumudu kucheza zaidi ya nafasi moja uwanjani.

Anaweza kutumika kama winga wa kulia, mshambuliaji namba mbili na winga wa kushoto kwa ufasaha, ndio maana Simba ilimng'oa Asec Mimosas ya Ivory Coast wakiizidi Yanga iliyokuwa pia ikimvizia kama ilivyokuwa kwa Ngoma.

Kramo uweo wake hauna mashaka, kilichobaki ni kuomba Mungu majeraha yasiendelee kumuandama ili awape raha mashabiki kwani jamaa ni fundi kwelikweli na Simba haikukosea kumbeba msimu huu.

Cheikh Sidibe - Azam FC

Beki huyo wa kushoto anayeichezea pia timu ya taifa ya Senegal ni bonge la mcherzaji ambaye Azam haina sababu ya kuwaza fedha ilizotoa kumng'oa katika timu ya Teungueth ya nchini kwao.

Sidibe ana uwezo mkubwa wa kukaba pamoja na kucheza na akili za washambuliaji, mbali na kutengeneza mashambulizi kutokana na kasi kubwa aliyonayo na uwezo wa kumwaga maji kila mara.

Mbali na kumudu kama beki wa kushoto, Sidibe mwenye bao kwa sasa katika Ligi Kuu na asisti mbili anachezapia kama wingi wa kushoto na hiyo ndio faida ambayo Azam inaipata kwa sasa kwa tabia yake ya kupandisha mashambulizi makali kila mara kwa wapinzani. Pia ni mahiri wa mpira ya friikikii, hivyo usajili wake kutua Azam hauna shaka yoyote, kwani uwezo umeonekana mapema!

Marouf Tchakei - Singida BS

Anacheza soka la kimataifa nchini Tanzania kwa mara ya kwanza, lakini tayari amethibitisha kuwa, mabosi wa Singida hawakujichanganya kumsajili kutoka AS Vita ya DR Congo.

Kiungo mshambuliaji huyo kutoka Togo anayemudu kucheza pia kama kiungo wa kati na winga wa kulia usajili wake hauna shaka kwani tangu atue Singida kazi imeonekana.

Tchakei ana uwezo mkubwa wa kupiga chenga, kasi, kumiliki mpira na uwezo wa kuwatoka mabeki kwa akili akijua pia kufunga kwa miguu sambamba na kuruka mipira ya vichwa.

Elvis Rupia - Singida BS

Mshambuliaji huyo kutoka Kenya ni bonge la usajili ambao Singida haiwezi kujilaumu kwani ni kati ya wachezaji waliozaliwa na vipaji vya kufunga mabao.

Ana nguvu, ana kasi na uwezo anao pia. Ana uwezo wa kumiliki na kukokota mpira kwa kadri anavyosikia. Mchezaji mzuri anahitaji kitu gani zaidi ya hivyo? Huyu jamaa amejiunga Singida akitokea Polisi Kenya Gor Mahia ana vitu vingi uwanjani, lakini kikubwa zaidi ni kwamba anajua kufunga. Pale Kenya msimu uliopita aliandika rekodi ya kufunga jumla ya mabao 27 akivunja rekodi ya iliyodumu miaka 47 iliyowekwa na Maurice Ochieng mwaka 1976 aliyekuwa Gor Mahia kwa kufunga mabao 26 mwaka 1976. Usajili wake kwa Singida hauna mashaka kabisa.

Gibril Sillah - Azam FC

Mgambia huyo naye hana maswali mengi, tatizo lake ni kwamba hajafunga bao lolote hadi sasa katika Ligi Kuu Bara, lakini kwa uwezo alioonyesha uwanjani ni dhahiri kuwa usajili wake hauna mashaka. Azam ilimng'oa kutoka Raja Casablanca ya Morocco, hivyo huenda mashabiki wa Azam kwa sasa wanataka waone thamani yake halisi.

Ila ni ukweli ulioko wazi kuwa jamaa ana uwezo mkubwa wa kumiliki mpira, ana kasi na uwezo wa kupunguza mabeki pia. Anamudu kucheza winga zote mbili, mbali na akitumika kama kiungo mshambuliaji, mtu wa kuwarahisishia wenzake kazi atakuwa na msaada mkubwa kwa timu hiyo ambayo msimu huu inaonekana imepania kwa usajili iliyofanya.

Maxi Nzengeli - Yanga

Kiungo mshambuliaji huyo kutoka DR Congo, amegeuka lulu ndani ya Yanga kutokana na uweoz mkubwa aliouonyesha hadi sasa.

Maxi anayemudu winga zote mbili ana uwezo mkubwa wa kukokota mpira, kupunguza mabeki na kufunga pia, mbali na kasi inayowachanganya mabeki wengi wa timu pinzani.

Moto alioanza nao tangu atue Jangwani kutoka AS Maniema Union ya DR Congo imefanya mashabiki kutokuwa na shaka naye, kwani anajua kufunga na kuasisti vile vile akiwasha moto kwenye mechi za Ligi Kuu Bara na zile za kimataifa na kama ataendelea na kasi aliyonayo itawatesa timu pinzani.

Pacome Zouzoua - Yanga

Kiungo mshambuliaji mwingine anayeweza kutumika kwenye nafasi zaidi moja uwanjani ni hazina nyingine ya Yanga iliyovuna kwenye usajili wa msimu huu.

Pacome aliyesajiliwa kutoka Asec Mimosas ya Ivory Coast ana vitu vingine vinavyokaribiana na Maxi au Stephane Aziz KI na kubwa ni umahiri wa kupiga chenga za maudhi, kutoa pasi zenye macho na pia kufunga hata kwenye nafasi ngumu.

Nyota huyo ni kati ya sajili bora zilizowahi kufanywa na Yanga kwa miaka ya karibuni, kutokana na kuwasha moto mapema na kuwatoa hofu mashabiki wa klabu hiyo walioingiwa na ubaridi baada ya baadhi ya nyota waliokuwa msimu uliopita kutimka kikosini akiwamo Fiston Mayele.

John Noble - Tabora United

Kipa huyo wa zamani wa Enyimba, aliyewahi kuidakia pia timu ya taifa ya Nigeria, ametua Tabora United (zamani Kitayosce) na tayari ameonyesha uwezo kwenye mechi chache ambazo timu hiyo imecheza na kuanz akuwatoa udenda vigogo wa Azam Fc wanampigia hesabu wamvute ili kuondokana na jinamizi linalowaandana eneo la kipa tangu alipoondoka Aishi Manula na muda flani Razack Abarola.

Noble amekuwa kivutio kikubwa kutokana na uwezo wake mkubwa wa kupangua mashuti na kuziba njia. Ni mzuri kwa mipira ya juu na chini na anaruka vizuri kwenda pande zote, hivyo msimu huu tutarajie kupata uhondo kutoka kwake, kwani usajili wake hauna mashaka yoyote.

Fabrice Ngoy wa Ngoy - Namungo

Hakuna shaka kwamba usajili wa mshambuliaji huyo wa zamani wa Kitayosce (sasa Tabora United), raia wa DR Congo hauna shaka kwani jamaa anajua sana kufunga mabao.

Akiwa ametoka kufunga jumla ya mabao 15 katika Ligi ya Championship, Fabrice ametua Namungo akiwa ni kati ya sajili nzuri, iwapo ataendeleza ule moto aliokuwa nao Kitayosce alipoipandisha daraja.

Ana uwezo mkubwa wa kutoka mabeki, kumiliki mipira na kupiga mashuti makali yanayolenga lango, huku akimudu kucheza nafasi zote za mbele za ushambuliaji kitu kinachoweza kuipa faida timu yake ya sasa inayonolewa na Kocha Cedric Kaze.

WENGINE

Mbali na wakali hao, lakini msimu huu wamesajiliwa wachezaji kibao wa kigeni ambao wana uwezo wa kuzibeba timu zao, akiwamo John Ben na Jackson Mbombo waliopo Tabora United, Yanick Bangala aliyekuwa Yanga na kutua Azam FC, Willy Onana mfungaji bora wa Ligi Kuu Rwanda msimu uliopita aliyetua Msimbazi, kama ilivyo kwa Luis Miquissone aliyerejea Simba kutoka Al Alhy ya Misri, sambamba na kipa Mmorocco, Ayoub Lakred aliyeanza kupewa nafasi Simba kwa sasa, huku beki Gift Fred na Hafiz Konkoni wakiendelea kujitafuta taratibu kama Allasane Diao wa Azam.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live