Siku hazigandi. Aliwahi kuimba mwanadada Komandoo Lady Jaydee. Kuanzia kesho, Alhamisi ule uhondo wa michuano ya Kombe la Mapinduzi unarudi upya. Ndio, msimu wa 18 wa michuano hiyo inayoanza rasmi kwenye Uwanja wa Amaan wenye mwonekano mpya wa kisasa wakati klabu 12 zitakapowania taji la 2024.
Michuano ya msimu huu inayokwenda sambamba na miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyofanyika Januari 12, 1964 ilikuwa ishirikishe timu 12 zikiwamo nne kutoka nje ya nchi, nne za Bara na nne za Zanzibar, lakini mambo yamebadilika kwa timu za kigeni kusalia tatu baada ya Bandari ya Kenya na URA ya Uganda kujitoa kutokana na sababu mbalimbali, huku nafasi zao zikichukuliwa na Jamus ya Sudan Kusini na JKU ya Zanzibar.
Huu utakuwa ni msimu wa 18 tangu michuano hiyo ilipoanzishwa 2007 na Mlandege ya Zanzibar ndio watetezi wa taji baada ya msimu uliopita kuifunga Singida Big Stars (sasa Singida Fountain Gate) kwa mabao 2-1.
Mashabiki wa soka visiwani Pemba na Unguja, hukaa mguu sawa kwa ajili ya kutaka kuanza kwa michuano hiyo kwani hupata burudani ambayo huikosa muda mrefu, kuzishuhudia timu maarufu za Simba na Yanga zikiumana.
Mbali na wakongwe hao, pia mialiko kwa timu za kigeni kutoka nje ya Tanzania ni sababu nyingine inayowasisimua wengi na kuwapa fursa ya kuwaona nyota ambao ni nadra kwenda visiwani kucheza mechi ya yoyote.
Katika michuano ya msimu huu kuna klabu 12 zitachuana zikiwa zimepangwa katika makundi matatu yenye timu tatu kila moja - Kundi A likiwa na watetezi, Mlandege na Jamhuri za Zanzibar, Azam FC na Vital’O ya Burundi, huku Kundi B likiwa na JKU, Simba, APR ya Rwanda na Singida FG, wakati Kundi C litakuwa na Jamus ya Sudan Kusini, Yanga, KVZ na Jamhuri.
Timu hizo zitakuwa zikiwania zawadi ya Sh100 milioni, huku itakayomaliza ya pili itabeba Sh70 milioni, ikiwa ni mara mbili ya zawadi za msimu uliopita ambao bingwa alitwaa Sh50 milioni na wa pili Sh30 milioni.
Mwanaspoti linakuletea timu 12 zitakazochuana kwenye michuano hiyo ya inayopigwa kati ya Desemba 28, 2023 hadi Januari 13, 2024.
SIMBA
Simba ndio timu iliyocheza fainali nyingi za michuano hiyo, ikicheza mara nane na kutwaa ubingwa mara nne ikiwa ni ya pili kubeba mara nyingi nyuma ya Azam FC iliyobeba mara tano.
Taji la mwisho kwa Simba iliyopo chini ya Kocha Abdelahak Benchikha ni msimu wa 2022, ilipoinyoa Azam kwa bao 1-0 lililowekwa kimiani na aliyeibuka Mfungaji Bora, Meddie Kagere.
Mataji mengine iliyobeba timu hiyo ni mwaka 2008 ilipoinyoa Mtibwa Sugar kwa bao 1-0, ikanyakua tena 2011 kwa kuibutua Yanga mabao 2-1 na taji la tatu ililinyakua 2015 kwa kuifumua tena Mtibwa kwa penalti 4-3,
Simba inarudi kwa nguvu ikiwa na mastaa ambao wanaweza kuisaidia kurejesha taji akiwamo Willy Onana, Fabrice Ngoma, kipa Ayoub Lakred, Fondoh Che Malonde na wengine.
AZAM FC
Ndio vinara wa kubeba mara nyingi taji la michuano hiyo wakichukua mara tano na kufanikiwa kuingia fainali mara sita ikiwamo mara ya mwisho 2022 ilipofungwa na Simba kwa bao 1-0 kuonyesha kuwa wao na Kombe la Mapinduzi ni damdam.
Msimu huu wanatua visiwani na kukata utepe siku ya kwanza ya michuano hiyo dhidi ya Chipukizi ikiwa na mziki wa mastaa wanaopewa nafasi kubwa ya kuibeba taji hilo kwa mara ya sana akiwamo Zanzibar Finest, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Idris Mbombo, Kipre Junior, Gjibril Sillah na wengineo. Mabingwa hao wa kihistoria wa michuano hiyo walicheza fainali ya kwanza 2012 dhidi ya Jamhuri Pemba na kuibamiza mabao 3-1.
Kisha wakarudi tena msimu uliofuata kwa kuvaana na Tusker ya Kenya na kuinyoa kwa mabao 2-1, 2017 iliitungua Simba kwa bao 1-0, Mwaka 2018 ilitetea tena taji kwa kuicharaza URA ya Uganda kwa penalti 4-3 baada ya dakika zao 90 kumalizika kwa suluhu na kuja kulibeba jumla mwaka 2019 kwa kuichapa tena Simba kwa mabao 2-1.
YANGA
Ndio waliokuwa mabingwa wa kwanza wa michuano hiyo ilipoasisiwa kwa mfumo unaotumika sasa kwa na kushiriki kwa misimu yote 16 iliyopita ikinyakua mara mbili mataji ya Mapinduzi.
Yanga iliyotemeshwa taji Januari 2022, ilibeba ubingwa wa kwanza 2007 kwa kuifunga Mtibwa Sugar mabao 2-1, pia walirudi tena msimu wa 2021 wakimfunga mtani wao kwa penati 4-3 baada ya suluhu ndani ya dakika 90.
Msimu huu wanarudi upya kushiriki mashindano hayo wakiwa na kikosi chao bora ambacho kimeweza kuongoza ligi kwa pointi 38 ligi kuu bara wakiongozwa na mastaa wake Fiston Mayele ambaye ameifungia timu yake mabao 10 na kiungo Mzanzibar Feisal Salum ambaye anarudi kwenye uwanja wake wa nyumbani akiwa ni mmoja wa mastaa wa kutumainiwa ndani ya Yanga.
Mbali na nyota hao lakini Yanga inatarajiwa kuwa na nyota wengine akiwamo Maxi Nzengeli, Clement Mzize, Farid Mussa, Hafiz Konkoni na nyota mpya kutoka JKU, Shekhan Ibrahim Khamis na wengine, japo huenda ikawa na sura nyingine mpya kutokana na wachezaji wake wengi kuitwa timu za taifa ikiwamo ya Tanzania inayojiandaa na Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika. Mashabiki wanaweza wasiwaone Pacome Zouzoua, Stephane Aziz KI, Diarra Djigui na Kennedy Musonda walioitwa timu za taifa za Ivory Coast, Burkina Faso, Mali na Zambia zinazojiandaa na michuano ya Afcon 2023 itakayoanza Januari 13 mwakani huko Ivory Coast.
SINGIDA FOUNTAIN GATE
Inashiriki kwa msimu wa pili kwenye mashindano hayo baada ya msimu uliopita kushiriki kwa mara ya kwanza kama Singida Big Stars na kufanya maajabu ya kupenya hadi fainali na kukutana na Mlandege iliyobeba taji, lakini ikiacha heshima ya kutoa Mfungaji Bora, Francis Kazadi aliyefunga mabao sita. Safari hii inarejea tena ikiwa na sura za mastaa kibao kutoka nje ya nchi, huku ikitarajiwa kumtambulisha rasmi nyota mpya kutoka FC Lupopo, Manu Labola Bola aliyekuwa anawindwa na Yanga na kutua timu hiyo.
Pia kuna wakali wengine kama Meddie Kagere anayerejea tena visiwani humo na timu hiyo, Kazadi, Elvis Rupia, Bruno Gomes na wakali wengine .
JAMUS FC
Wakali hao kutoka Sudan Kusini inashiriki mashindano haya kwa mara ya kwanza kwa timu kutoka nje ya Tanzania ushiriki wake utaongeza chachu ya ushindani kwenye mashindano hayo, inakuja ikiwa imetoka kubeba ubingwa wa FA ya nchini huko kutoka Juba kwa kuifunga Malakia. Jamus inatarajiwa kutoa upinzani kutokana na kuundwa na wachezaji wenye vipaji na kiu ya mafanikio, hivyo kuongeza utamu wa michuano ya Mapinduzi itkapoanza kutupa karata za kwa mara ya kwanza visiwani Zanzibar.
MLANDEGE
Ndio watetezi wa taji hilo na mabingwa mara saba wa Ligi Kuu Zanzibar wakishika nafasi ya pili nyuma ya KMKM, iliyotwaa 1996, 1997, 1998, 1999, 2001, 2002, na 2019/2020. Wanaingia kwenye mashindano hayo ikiwa nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi baada ya kukusanya pointi 19 katika mechi 15 za duru la kwanza, lakini wakiwa na kazi ya kutetea taji ililotwaa msimu uliopita kwa kuifunga Singida Fountain Gate kwa mabao 2-1. Timu inaingia kwenye michuano hiyo ikiwategemea nyota wake kadhaa akiwamo Bizimana Valentin Nestory, Oscar Sikah, Bakar Nassor Bakar na Abdallah Said aliyeitwa hivi sasa katika kikosi cha timu ya taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’ kilicchovaana an Kilimanjaro Stars ya Tanzania Bara kuzindua Uwanja wa Amaan.
KVZ
Inashika nafasi ya nne katika Ligi Kuu ya visiwani humo iliyomaliza duru la kwanza ikikusanya pointi 27 na kufunga mabao 20.
Ni timu inayoonekana kuwa imara zaidi kwenye eneo la ushambuliaji, kwani straika wao, Suleiman Mwalim Abdallah anashika nafasi ya pili kwa mabao mengi akifunga manane hadi sasa katika Ligi ya Zanzibar, nyuma ya kinara Ibrahim Hamad ‘Hilika’ mwenye mabao 10.
VITAL’O
Wakali hao kutoka Burundi itashiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza na inatarajiwa kutoa upinzani kama ndugu zao Aigle Noir iliyoshiriki msimu uliopita na kutolewa nusu fainali na Mlandege.
Kikosi hicho kinatarajiwa kuja na majembe ya maana kama kipa Omar Biha, mabeki Alain Ndizeye, Nassor Niyonkuru, Issa Hubert Nsabumana, Iddy Djumapili, Fataki Kiza na D’Amour Nkurunziza.
Wengine Sutche Wambo, Fidele Nimubona, Trésor Akimana, Leopold Nkurikiye, Henry Mbazumutima, Fuadi Ndayisenga na mastraika Fuadi Ndayisenga na Déo Ndayishimiye.
JKU
Hawa ndio vinara wa Ligi Kuu ya Zanzibar, imeingia kwenye michuano hiyo baada ya kuongezwa dakika za mwisho sambamba na Jamus ya Sudan Kusini baada ya URA na Bandari kujitoa.
Timu hiyo itakuwa na kazi ya kuthibitisha kuwa wanastahili kuongoza mzimamo wa ZPL na kuingizwa kwao michuano kutawapa fursa ya kuandika rekodi ya kubeba taji hilo kwa mara ya kwanza kama ilivyotokea msimu uliopita kwa Mlandege waliyovikomboa visiwani hivyo kwenye Mapinduzi kubeba taji.
Kabla ya Mlandege, timu za Zanzibar zilikuwa wasindikizaji wakati za Bara na zile za nje ya nchi au Mtibwa zikipishana kubeba taji la michuano hiyo. Timu hiyo itaingia kwenye michuano hiyo ikijivunia straika wa mabao Gamba Idd Matiko na Saleh Kalabaka Kikuya wanajua kucheka na nyavu mbali na wakali wengine kama kipa Yacoub Suleiman na Swedi Juma waliopo Zanzibar Heroes pamoja na Mudrik Abdi Shehe ili kuzitetemesha timu nyingine kwenye michuano hiyo.
JAMHURI
Timu hiyo kongwe kutoka Pemba, inashiriki kwa mara nyingine michuano hiyo ikiwa na rekodi ya kucheza fainali mwaka 2012 mbele ya Azam na kupoteza kwa mabao 3-1. Licha ya kuwa na hali mbaya kwenye Ligi Kuu ya Zanzibar ikishika nafasi ya 14 kati ya timu 16 ikikusanya pointi 15 tu katika mechi 15, Jamhuri ni moja ya timu yenye uzoefu wa michuano hiyo na inatarajiwa kutoa upinzani kwenye msimu huu wa 18.
Timu hiyo inatarajiwa kuendelea kuwategemea nyota wake kadhaa akiwamo Hussein Abubakar Ahmas, Abdulrahmana Salum Omari, Abdillah Ramadhan Salim na Suleiman Masoud wanaotamba ZPL.
CHIPUKIZI
Wakali wengine kutoka Pemba wanaoshiriki michuano hiyo wakiiwakilisha Zanzibar, sio ya kubezwa kwani ni timu inayoundwa na vijana wanaojua mpira.
Inashiriki michuano hiyo ikiwa ndio kwanza imetoka kurejea kucheza Ligi Kuu ya Zanzibar baada ya kusota kwa muda tangu iliposhuka daraja, lakini ikionekana kuwa na moto ikiwa inashika nafasi ya nane, ikikusanya pointi 19 baada ya mechi 15, ikifunga mabao 10 na kufungwa 12.
Itaendelea kuwategemea nyota wanaotamba ZPL kama Faki Mwalimu Sharif, Ahmed Khamis Ali, Haji Salum Haji, Ibrahim Kombo, Khalfan Abdalla Saleh, Abdulmahfoudh Ali, Zubeiry Yahya na wengineo.
APR
Hawa ni mabingwa wa mara nne mfululizo wa Ligi Kuu ya Rwanda na ujio wake kwenye michuano hiyo ni wazi itaongeza chachu na ushindani kwa timu nyingine shiriki, kwani sio timu nyepesi ikiwa inamilikiwa na Jeshi la Rwanda.
Ni timu yenye soka la chini na pasi nyingine na kushambulia mwanzo mwisho, kitu kinachoweza kuzipa wakati mgumu wapinzani na sio ajabu kuiona ikiondoka na taji hilo kurudi kwao. Timu hiyo inayonolewa na Kocha Mfaransa, Thierry Froger ina nyota tishio wenye uzoefu wa michuano hiyo kama Taddeo Lwanga na Sharaf Eldin Shiboub waliowahi kucheza Simba, Yannick Bizimana, Ramadha Niyibizi, Victor Mbaoma, Ndikumaa Danny, Niyonshuti Hakim, Gilbert Mugisha, Innocent Nshuti na Alain Kwitonda.
Wengine ni; Ilshade Nsengiyumva, Jean Bosco Ruboneka, Bemol Apam Assongwe, Ismail Nshimirimana, Fitina Omborenga, Christian Ishimwe, Banga Bindjeme na Yunusu Nshimiyimana.