Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hawa hapa wabaya wa Diarra Bongo

Kibu X Dubeeee Hawa hapa wabaya wa Diarra Bongo

Mon, 12 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kikosi cha Yanga kimezidi kuimarika baada ya kurejea kwa nyota wa timu hiyo waliokuwa kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 zilizomalizika wikiendi iliyopita kule Ivory Coast.

Stephane Aziz KI na kipa Diarra Djigui ndio pekee waliokuwa hawapo na kikosi hicho kutokana na timu za taifa za nchi zao, Burkina Faso na Mali kuendelea kusalia michuanoni, huku nyota wengine waliokuwa wa timu za Tanzania na Zambia kutolewa mapema katika hatua ya makundi.

Diarra akiwa na Mali waliishia robo fainali, wakati Aziz KI akiichezea Burkina Faso walikwamia hatua ya 16 Bora wakipoteza mbele ya Mali, ambayo nao walishindwa kuvuka mbele ya wenyeji Ivory Coast baada ya kufungwa kwa mabao 2-1 katika pambano lililochezwa kwa muda wa dakika 120.

Kipa huyo anarudi kwenye Ligi Kuu Bara akiwa na kumbukumbu ya kutunguliwa jumla ya mabao sita katika mechi nne kati ya tisa ambazo alikaa langoni tangu msimu ulipoanza Agosti 15, 2023.

Kipa huyo kwa msimu huu ameikosa michezo sita, ukiwamo ule kwanza dhidi ya KMC ambapo langoni alisimama Metacha Mnata wakati Yanga ikishinda mabao 5-0, dhidi ya Coastal Union ambapo Abuutwalib Mshery alikaa langoni, pia ameikosa michezo mingine mitatu wakati akiwa Afcon 2023 ukiwamo dhidi ya Kagera Sugar aliokaa langoni Metacha Mnata na kuisha kwa suluhu, huku zile za Dodoma Jiji na Mashujaa, kocha Miguel Gamondi alimpanga Mshery na timu hiyo kushinda zote na jana Metacha alianza kwenye pambano dhidi ya Tanzania Prisons, huku Mshery akiwa benchi.

Diarra aliyejiandikia rekodi tamu Afcon 2023 kwa kucheza kwa dakika 480 za mechi zote tano za Mali, ukiwamo ule wa robo fainali dhidi ya wenyeji uliopigwa kwa dakik 120, huku akiruhusu mabao manne pekee, huku akipata clean sheet mbili mbele ya Afrika Kusini na Namibia, katika Ligi Kuu ya msimu huu ameruhusu mabao sita pekee katika mechi nne, huku michezo saba aki.

Kumbuka Diarra ndiye Kipa Bora wa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa pili mfululizo akiiwezesha pia Yanga kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita na timu hiyo kulikosa taji kwa kanuni ya bao la ugenini, kwani matokeo ya mechi mbili dhidi ya USM Alger ya Algeria ilikuwa 2-2.

Licha ya kuwa na sifa ya kutofungika kirahisi, lakini kuna wanaume sita waliotumia nafasi walizopata mbele ya Diarra katika msimu huu kufunga, huku ni mchezo mmoja tu, Yanga ilipoteza huku langoni akisimama kipa hiyo maarufu kama Screen Protector.

Hapa chini ni wakali hao sita waliofanikiwa kumtungua Diarra msimu huu katika mechi nne za Ligi Kuu, huku hakuna hata mmoja aliyethubutu kumfunga mara mbili katika mechi moja, lakini kipa huyo akipata Clean Sheet kwenye michezo mitano aliosimama langoni msimu huu.

LENNY KISSU (IHEFU)

Nahodha na beki huyu wa kati wa Ihefu ndiye aliyekuwa mchezaji wa kwanza kumtungua Diarra katika Ligi Kuu kwa msimu huu wakati watetezi hao wakilala 2-1 kwenye mechi iliyopigwa Oktoba 4, 2023 kwenye Uwanja wa Highland Estate, uliopo Mbarali, jijini Mbeya.

Beki huyo alifunga bao hilo lililokuwa la kusawazisha katika dakika ya 40, ikiwa ni mara ya pili kwake kumtungua Diarra kwani katika mechi ya msimu uliopita, alifunga bao la ushindi kw Ihefu iliyoifyatua watetezi hao kwa mabao 2-1.

Mechi hiyo ya msimu uliopita ilipigwa Novemba 29, 2022 ndio iliyovunja mwiko na kutibua rekodi ya Yanga ya kuendelea kucheza mechi mfululizo bila kuonja kipigo, kwani tayari ilikuwa imeshacheza michezo 49 bila kupoteza, lakini bao la Lenny likaharibu rekodi yao katika mechi hiyo ya 50.

CHARLES ILANFYA (IHEFU)

Huyu ndiye aliyekuwa mchezaji wa pili aliyemfanya Diarra kufungwa mabao mawili ktika mchezo mmoja kwa mara ya kwanza msimu huu, baada ya kufunga bao la ushindi lililoizamisha Yanga kikiwa kipigo cha kwanza pia katika ligi hiyo.

Ilanfya ambaye kwa sasa amerejea Mtibwa Sugar kupitia dirisha dogo, alifunga bao hilo dakika ya 67, likitofautiana kwa dakika tano na lile la ushindi la Lenny la msimu uliopita ambalo lilifungwa dakika ya 62, licha ya mechi zote Yanga kutangulia kupata bao dakik za mapema.

Katika mechi ya msimu uliopita, Yanga ilitangulia kwa bao la dakika ya nane kupitia Yannick Bangala aliyepo Azam FC kwa sasa kisha Never Tigere kusawazisha dakika 38, na katika mechi ya msimu huu Pacome Zouzoua alifunga dakika ya nne tu kabla ya Lenny kusawazisha na Ilanfya kuongeza la pili la ushindi lililowatibulia Yanga kwa mara ya pili mfululizo ikiwa ugenini.

JIBRIL SILLAH (AZAM FC)

Nyota huyu kutoka Gambia alikuwa ni mchezaji wa kwanza wa kigeni na watatu kumtungia Diarra katika Ligi Kuu Bara kwa msimu huu wakati Azam FC ikilala mabao 3-2 kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Katika mechi hiyo iliyopigwa Oktoba 23, 2023, Sillah alifunga bao lililokuwa la kusawazisha akimalizia kazi nzuri ya Feisal Salum 'Fei Toto' katika dakika ya 19 baada ya Stephane Aziz KI kuitanguliza Yanga dakika ya tisa tu ya mchezo huo. Aziz KI alifunga mabao mengine ya Yanga na kuandika hat-trick yake ya kwanza msimu huu.

PRINCE DUBE (AZAM FC)

Mwana Mfalme kutoka Zimbabwe, Prince Dubu ndiye aliyekuwa mchezaji wa nne kutungua Diarra msimu huu katika mechi ya Oktioba 23, alipofunga bao lililokuwa la pili kw Azam na kwa mchezo huo kwa mkwaju wa penalti dakika ya 62.

Dube alikuwa ni mchezaji wa pili wa kigeni kumtungua kipa Bora huyo kwa Ligi Kuu kwa msimu wa pili mfululizo, kiasi cha kuwapa matumaini Wanalambalamba kuamini wangejivua joho la unyonge mbele ya Yanga, lakini bao hilo lilichomolewa na Aziz KI dakika saba baadae kisha kiungo nyota huyo kutoka Burkina Faso kuongeza jingine dakika ya 70 lililoipa Yanga ushindi wa mabao 3-2.

KIBU DENIS (SIMBA)

Mshambuliaji huyu mahiri wa Simba, ndiye aliyekuwa mchezaji wa tano msimu huu kumtungua Diarra, wakati alipotupia bao lililokuwa la kusawazisha kwa Wekundu wa Msimbazi waliofumuliwa na Yanga kwa kipigo cha mabao 5-1.

Katika mechi hiyo ya kwanza kwa msimu huu ya Kariakoo Derby, Kibu alifunga bao dakika ya tisa na kufanya ubao usomeke 1-1 baada ya awali Kennedy Musonda kuitanguliza Yanga kwa bao la dakika ya tatu tu ya mchezo huo mkali uliopigwa Novemba 5, 2023 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Hilo lilikuwa ni bao la pili mfululizo kwa Kibu kumtungua Diarra katika mechi ya Kariakoo Derby, kwani kwenye pambano la maarudiano la msimu uliopita, pia alifunga wakati Simba aikishinda 2-0, bao la kwanza lilifunguwa na beki Mkongoman, Henock Inonga dakika za mapema.

Hata hivyo, licha ya Kibu kuisawazishia Simba, haikuzuia Wekundu kupata aibu baada ya Maxi Nzengeli kufunga mabao mbili, Aziz KI na penalti ya Pacome kuwanyamizisha Wana Msimbazi.

SEIF KARIHE (MTIBWA SUGAR)

Huyu ndiye aliyekuwa mchezaji wa mwisho kumtungia Diarra kabla ya kipa huyo kwenda fainali z Afcon 2023 kule Ivory Coast.

Mshambuliaji hiyo wa Mtibwa Sugar alifunga bao hilo dakika ya 90+5 na kuipa timu hiyo ya Manungu bao la kufutia machozi kwenye kipigo cha mabao 4-1 ilichopewa kwenye mchezo huo uliopigwa Desemba 16, 2023.

Karihe alifunga bao hilo akiuwahi mpira ambao ulionekana wazi beki Ibrahim Bacca aliyechezew madhambi wakati akijiandaa kuuokoa, kisha mfungaji huyo akaupiga kwa shuti la mbali lililomshinda nguvu kupa Diarra aliyekuwa amesogea mbele la lango.

Hata hivyo, bao hilo halikuisaidia kwani tayari Aziz KI alifunga mara mbili dakika ya 45+1 na 65, huku Kennedy Musonda alifunga dakika ya 76 na Skudu Makudubela alitumia dakika ya 83.

CLEAN SHEET

Diarra licha ya kuruhusu nyavu za Yanga kuguswa kwenye mechi nne kati ya tisa alizosimama langoni, lakini mwamba huyo kuna mechi tano alikomaa na kutoruhusu bao lolote na kuifanya Yanga hadi sasa kuwa timu iliyoruhusu mabao machache zaidi na kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi.

Kipa huyo hakuruhusu bao kwenye mechi yake ya kwanza msimu huu katika Ligi dhidi ya JKT Tanzania ambayo ilipasuliwa mabao 5-0, kisha akakomaa dhidi ya Namungo iliyoisha kwa Yanga kushinda 1-0, halafu akafanya mambo dhidi ya Geita Gold iliyonyukwa mabao 3-0 jijini Mwanza.

Pia Diarra alisimama imara katika pambano la nyumbani dhidi ya Singida Fountain Gate iliyonyukwa 2-0 na ile ya mwisho ya ugenini dhidi ya Tabora United iliyopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma na Yanga kushinda bao 1-0 kisha kwenda zake Afcon 2023.

POINTI 24 MECHI 9

Rekodi zinaonyesha katika mechi 15 za duru la kwanza ilizocheza Yanga hadi jana na kukusanya jumla ya pointi 40 ikitokana na kushinda michezo 13 na kutoka sare mara moja na kupoteza pia mchezo mmoja.

Katika pointi hizo 40, kipa Diarra amechangia kuipa Yanga jumla ya pointi 24 kupitia mechi tisa alizocheza, akishinda michezo minane na kupoteza mmoja, huku kipa huyo akiwa hajawahi kukaa langoni kisha Yanga ikatoka sare yoyote, kuonyesha ana mchango mkubwa kiasi gani kikosini.

Pointi 16 nyingine za Yanga zimechangiwa na makipa Metacha Mnata aliyedaka kwenye mechi tatu ambapo moja iliisha kwa suluhu na Kagera, mbili zikiisha na ushindi wa 5-0 dhidi ya KMC kisha jana kukaa langoni kabla ya kupewa kadi nyekundu huku timu hiyo ikiwa inaoongoza kwa mabao 2-0.

Hii ikiwa na maana Metacha amechangia pointi sita, wakati Mshery katika mechi tatu alizocheza pia Yanga imeshinda zote, ikiwamo ile ya 1-0 dhidi ya Coastal Union, 1-0 ya Dodoma Jiji na 2-1 dhidi ya Mashujaa, kabla ya jana kuingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Metacha aliyelimwa kadi nyekundu wakati Yanga ikiwa mbele kwa mabao 2-0, kisha kuruhusu bao moja mechi ikiisha kwa 2-1.

Chanzo: Mwanaspoti