Kulikuwa na fununu zinatambaa chini kwa chini kwamba, Kocha wa Yanga, Nasrudinne Nabi anatakiwa kukabidhiwa mikoba ya kuinoa Timu ya Taifa ya Tanzania, ‘Taifa Stars’.
Binafsi sijui ni nani aliyezusha hili au nani aliyevujisha habari hizi kabla ya Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) halijatangaza rasmi kuhusu kutaka kumpa mikoba hiyo Nabi.
Kwa kuwasikiliza baadhi ya mashabiki wa Yanga, wanataka jambo hili lipite mbali. Hawataki kocha wao, Nabi aifundishe Stars. Nadhani wanadhani atatoka katika reli kutokana na timu yao kuwa na mwendelezo mzuri katika kipindi hiki.
Lakini hili linaweza kuwa geni kwa baadhi ya watu, miaka ya nyuma jambo hili lilikuwa la kawaida sana, tena Yanga imenufaika sana na makocha wa Timu ya Taifa ya Tanzania.
Ingawaje hivi karibuni Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) liliwahi kuwachukua makocha wa klabu za KMC na Namungo na kuwafanya kuwa makocha wa Stars kwa muda.
Kocha wa KMC Mrundi, Ettiene Ndairagije ambaye alienda na timu hiyo katika mashindano ya Chan baada ya kufanikiwa kufuzu akiwa na timu hiyo. Pia, katika hatua ya kufuzu mashindano hayohayo ya Chan dhidi ya Uganda msimu ulioisha, TFF ilimchukua Kocha wa Namungo, Mzambia, Hanour Janza kujaribu kuokoa jahazi lililozama.
Makocha hawa hawazungumzwi sana kwa kuwa hawakutoka katika timu zenye wapenzi wengi sana.
MAKOCHA WA SERIKALI
Miaka ya nyuma serikali mbali na kuajiri makocha kutoka nje, ilikuwa na makocha wake ambao walipelekwa nje kwenda kujifunza mbinu mbalimbali za soka.
Makocha wengi wa Tanzania walipelekwa Ujerumani Mashariki ambayo ilikuwa inafuata sera za ujamaa kama ilivyokuwa Tanzania.
Makocha wa Kitanzania waliopelekwa kusoma Ujerumani baadhi yao ni Joel Nkya Bendera, Shabani Marijani ‘Maji Moto’ au Maji Mengi na Paul West Gwivah.
Wengine ni Mbwana Abushiri, Ray Gama na Elijah Kategile (baba yake mchezaji wa zamani wa Kagera Sugar na Simba, Alfred Kategile). Chama cha Soka Tanzania (FAT) kiliwahi kumteua Kocha Ray Gama wa Yanga kuionoa Stars. Baadaye Gama aliinoa Majimaji ya Songea.
Kategile naye alikuwa kocha wa Pamba ya Mwanza alichaguliwa kuwa kocha namba tatu wa Timu ya Taifa ya Tanzania 1981 akiwa nyuma ya Mjerumani, Rud Gultendouf na Mohammed Msomali kuinoa Stars.
Kocha Bendera naye alikuwamo kwenye jopo hilo la makocha akitokea serikalini akiwa mtumishiwa wa Wizara ya Michezo na Utamaduni.
Pia, Kocha Mohammed Msomali aliyekuwa akiinoa Tumbaku ya Morogoro mara kadhaa alipewa jukumu la kuiongoza Taifa Stars.
SIMBA ILINUFAIKA
Simba ilinufaika na Kocha wa Serikali, Bendera mwaka 1979 baada ya kufungwa na Mufulira Wonderers 4-0 nyumbani aliiongoza kwenda kushinda 5-0 ugenini, kocha alikuwa Bendera ambaye mbali na kuwa mtumishi wa serikali pia alikuwa shabiki mkubwa wa Yanga.
Pia, Gwivah alikuwa pia mtumishi wa serikali aliutumia muda wake mwingi kuinoa Simba.
Yanga kwa nyakati tofauti imewahi kuwachukua makocha wa nje ambao waliomaliza majukumu yao ya kuionoa Taifa Stars.
Baadhi ya makocha hao ni Mjerumani, Rudolf ‘Rudi’ Gutendorf na Mwingereza, Jeff Hudson. Bendera aliisaidia Yanga dhidi ya Al Ahly jijini Dar es Salaam mechi uliyoisha kwa sare. Pia aliongeza nguvu kwa Coastal Unioni mwaka 1989 akiwa na Zakharia Kinanda kule Kenya katika Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati dhidi ya Kenya Bweweries.
RUD ALISUKA UKUTA
Baada ya kufungwa na katika fainali ya Challenge na Kenya ‘Harambee Stars’ bao 1-0. Baada ya mchezo huo, Rud aliachana na Stars na kuujinga na Yanga.
Kocha huyo Mjerumani aliikuta Yanga ikiwa haiko vizuri sana katika safu yake ya ulinzi, hivyo akaamua kuisuka na kujenga ulioitwa ‘Ukuta wa Berlini.’
Rud alimhamisha beki namba mbili, Athuman Juma ‘Chama’ kutoka beki wa kulia na kumweka katikati sambamba na Allan Shomari.
Akamhamisha Ahmed Amasha ‘Mathematics’ kutoka kiungo wa kukaba na kumpa ubavu wa kushoto alikokuwa akicheza Hussein Mmakonde.
Beki mbili akaja kucheza Yussuf Ismaili Bana. Hapo ukuta ukawa umekamilika golini alikaa Hamis Kinye. Rud alienda na Yanga katika michuano ya klabu bingwa Afrika Mashariki na kati mwaka 1982 nchini Kenya na Hudson naye alikwenda na timu hiyo kwenye Kisumu nchini Kenya mwaka 1988. Mwaka 2014. Yanga ilimwajiri Kocha Marcio Maximo aliyewahi kuinoa Taifa Stars.