Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hausung: Yanga ni kubwa ila tunayo ASFC

Hausung Hausung: Yanga ni kubwa ila tunayo ASFC

Fri, 8 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) hatua ya 64 ikitarajia kuendelea kati ya Desemba 15-17, Hausung inasubiri mchezo dhidi ya Yanga kwa hamu kubwa ili kuionesha maajabu Tanzania.

Hausung inashiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza baada ya kufanya vizuri hatua ya awali ilipoichapa Mgololo FC 2-0, katika Uwanja wa Samora mkoani Iringa.

Timu hiyo yenye makazi yake katika Kata ya Ihanga huko Igomini nje ya Mji wa Njombe, ndio mabingwa wa mkoa huo ilipoilaza Michael Jackson mabao 2-0 kwenye fainali ya Ligi Daraja la Tatu.

Kwa sasa Njombe haina timu inayoshiriki ligi za ushindani tangu Njombe Mji iliyowahi kucheza Ligi Kuu na kushuka daraja na kupotea kwenye mashindano misimu miwili.

Wadau na mashabiki wengi wa soka mkoani Njombe, matarajio yao makubwa yapo kwa Hausung wakiamini inaweza kufanya kweli na kurejesha burudani.

HAINA HISTORIA

Timu hii ilisajiliwa 2021 na kushiriki Ligi ya Wilaya hadi Mkoa na ilitwaa ubingwa na kushiriki ASFC ikiwa ni mara ya kwanza na itakuwa rekodi ya kwanza kucheza dhidi ya Yanga inayotetea taji hilo.

PACOME, AZIZ KI WATAJWA

Kocha wa timu hiyo, Shangwe Michael anasema licha ya furaha kwa benchi la ufundi na wachezaji kupangwa na Yanga, lakini anajua shughuli haitakuwa nyepesi.

Anasema anavyoiona Yanga msimu huu wamekuwa wakicheza soka la ushindani na mara kadhaa huwa wakali kwa mashambulizi ya pembeni na muda mwingine kutumia viungo.

Anasema kwa kikosi cha bingwa huyo mtetezi wa Ligi Kuu na ASFC, anamuona Pacome Zouzoua ndiye atakuwa msumbufu hivyo watahakikisha wanamdhibiti.

“Naifuatilia sana Yanga, mashambulizi yao zaidi ni pembeni kwa mawinga na eneo la katikati kwa viungo, lakini nitawaelekeza vijana wangu kuwa makini na Pacome, yule bila kumdhibiti madhara yake ni makubwa.

“Kuna hata Aziz Ki kwa mipira ya faulo na mashuti ya kushtukiza, lakini huyo hatupi ugumu kwakuwa tunajua tutambana vipi hasa kwenye mguu wa kushoto ambao ndio wenye hatari,” anasema Michael.

Kocha huyo anaongeza mchezo huo utakuwa muhimu sana kwao kwani nchi nzima itafuatilia, hivyo lazima waingie uwanjani kwa kujiamini na kuonesha uwezo na vipaji walivyonavyo.

Anasema mchezo huo ni kipimo kwa maandalizi yao ya kwenda Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) hivyo itawapa mwanga kubaini udhaifu wao.

“Ukicheza na Yanga ni fursa kubwa kujitangaza, hatutegemei kuwa dhaifu bali tutapambana ikiwa ni njia ya kujipima kuelekea RCL, ninao vijana wenye uwezo japo uzoefu hatuna,” anasema kocha huyo.

STAA WAO ATULIZA

Nahodha wa timu hiyo, Henry William anasema licha ya kukutana na timu kubwa lakini kwao ni furaha kwani ndio wanaenda kuonesha uwezo na kujitangaza zaidi.

Anasema hawakutarajia kukutana na vigogo hao, lakini kutokana na matokeo waliyopata walijiandaa kumkabili na timu yoyote watakayepangwa nayo hivyo hata Yanga watavaana nao.

“Sisi tunaendelea kujiandaa kwa kufanya mazoezi na kufuata maelekezo ya kocha ili siku ya mechi tuingie kupambana kutafuta ushindi, mashabiki wawe na matumaini tutashinda,” anatamba nyota huyo.

UONGOZI VIPI

Mwenyekiti wa timu hiyo, Erasto Haule anasema hawana hofu kukutana na Yanga kwani waliopanga ratiba wanafahamu uwezo wao kucheza na timu yoyote na hawataingia uwanjani kinyonge.

“Hatuna hofu kucheza na Yanga, hatuendi kushiriki bali kushindana ili kwenda hatua nyingine, tulicheza na Ihefu iliyoifunga Yanga mechi ya kirafiki hatukufungana, hivyo tunajiamini,” anatamba Haule.

Kiongozi huyo anaongeza iwapo mechi hiyo Yanga watahitaji kumchukua nyota wao yeyote atakayewavutia, hawatamzuia kwani mpira ni fursa, biashara na ajira.

“Kwa upande wetu hatuna mpango wa kusajili wachezaji kutoka Yanga, ila wao wakitaka hatuna shida, tutaweka dau kwa wachezaji kuhakikisha wanacheza na kushinda mechi hiyo,” alisema kigogo huyo.

MKOA NAO WAPANIA

Katibu mkuu wa Chama cha Soka Mkoa wa Njombe (Njorefa), Lucas Ndifwa anasema kukutana na Yanga ni furaha kwao kutangaza Mkoa na vijana kujiweka sokoni kwani hata dirisha dogo linakaribia.

Chanzo: Mwanaspoti