Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hatma ya Sven ipo kwa mo

95095 Sven+pic Hatma ya Sven ipo kwa mo

Mon, 10 Feb 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

SIMBA inajiandaa kwenda Morogoro kwa ajili ya mchezo wao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Mtibwa Sugar, huku Kocha Mkuu wake, Sven Vanderbroeck akiwa kwenye wakati mgumu baada ya juzi kujikuta akizomewa na mashabiki kutokana na kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa JKT Tanzania.

Tayari kumekuwa na taarifa za chini chini kocha huyo Mbelgiji hana muda mrefu kabla ya kutupiwa virago kwani mabosi wake hawataki kuona timu yao inapata matokeo mabaya zaidi, huku Mtendaji Mkuu waSimba, Senzo Mazingisa akifichua hatma ya kocha huyo ipo chini ya Bodi ya Wakurugenzi ya Simba inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Mohammed ‘Mo’ Dewji.

Akizungumza na Mwanaspoti kwa muda wa dakika 30, Senzo alifichua hawatakuwa tayari kupokea tena matokeo mabaya kama waliyopata dhidi ya JKT, lakini hata kiwango kinachooneshwa na timu hakiwaridhishi kabisa.

Hata hivyo, alisema yeye hawezi kuwa na maamuzi yoyote dhidi ya kocha huyo na suala lake analiacha kwa Bodi ya Wakurugenzi chini ya MO Dewji kama itasema atimuliwe hatakuwa na neno.

Senzo alisema awali kwa jinsi timu ilivyo, walitaka kukaa na kocha kwa muda mrefu, kwani hitaji lao maendeleo zaidi na sio kubadilisha makocha kila mara, kwa vile wamegundua badiliko la kocha kila mara limekuwa likiwayumbisha.

Hata hivyo, alisema kwa namna timu inavyocheza na kutoridhishwa na viwango vya wachezaji inamweka pabaya kocha huyo, lakini akasisitiza;

Pia Soma

Advertisement
“Kuhusu suala la kuondoka kwake (Sven) baada ya matokeo haya, kwangu limenizidi ila naenda, nitazungumza na Bodi ya Wakurugenzi na kama wataridhia kumtimua sitaweza kupinga.”

“Bodi ndio kila kitu, mimi ni mtendaji tu, ila nimeona hapa timu inacheza lakini ikiwa haina kiwango cha kuvutia kwa mechi kadhaa sasa na kama wataridhia atimuliwe itakuwa sawa tu, kwani kazi yangu ni kutenda,” aliongeza Senzo anayetajwa ndiye aliyependekeza kuletwa kwa Sven.

“Kimsingi matokeo haya na hata timu inavyocheza, naamini hata bodi hairidhishwi nayo kwa maana siwezi kueleza lolote, maamuzi ya mwisho juu ya Sven yapo kwao na lolote linaweza kutokea kwa namna hali ilivyo kwa sasa,” alisema Senzo.

Hata hivyo, alipododoswa kama atatimuliwa hivi karibuni alisema; “Tuache kuzungumza maneno mengi kuhusu Sven, wakati huu mpaka hapo bodi ambavyo itaamua, lakini kwa jumla matokeo ya kufungwa na JKT kila mtu imemuuma na tunatakiwa kulaumiwa wote kila mmoja kwa nafasi yake.”

Pia aliwataka wanachama na mashabiki wa Simba watulie na kuacha kuongea maneno makali kwani haivutii na kudai viongozi wanafanyia kazi ili kuona timu inafika mbali na kufikia mafanikio yenye furaha.

Aidha alifichua kwa namna wachezaji wanavyocheza kwa siku za karibuni, watakaa nao na kuwaeleza umuhimu wa kuitambua thamani ya jezi za klabu hiyo na kujituma kuwapa furaha mashabiki, pia kuipaisha timu ambayo ina uwekezaji mkubwa uliofanywa na MO Dewji.

“Jambo tunaloenda kulifanya wakati huu tutawaeleza wachezaji wetu kama viongozi, wale wenye kuonyesha kucheza chini ya kiwango mara kwa mara haturidhishwi nao na kama hawatajirekebisha tunaweza kufanya maamuzi dhidi yao,” alisema Senzo.

“Maamuzi ni yale ambayo yanamtaka mchezaji kuwajibika na kusikia uchungu wa klabu kwani hayatakuwa mazuri kwa upande wao,” alisema Senzo ambaye alionekana mwenye hasira kwa kufungwa na maafande hao.

Chanzo: mwananchi.co.tz