Uongozi wa Geita Gold leo utaanza kufanya tathmini ya msimu ulivyokuwa katika kikao ambacho kinaweza kutoa uamuzi wa hatma ya Kocha Felix Minziro na msaidizi wake, Mathias Wandiba.
Minziro na Wandiba walisimamishwa hivi karibuni kwa sababu ambazo hazikuwekwa wazi huku tetesi zikidai kuwa ni kutokana na kufanya vibaya kwa timu hiyo katika mechi mbili zilizopita dhidi ya Mbeya City na Tanzania Prisons.
Hilo limetokea wakati mikataba ya wawili hao kuinoa Geita Gold ikikaribia ukingoni ambapo itafikia tamati baada ya kumalizika msimu huu.
Mwenyekiti wa Geita Gold, Leonard Bugomola amesema watajadiliana suala la benchi la ufundi na hadi kufikia mwisho wa msimu Juni 9, watakuwa wamejua mwelekezo.
“Tutaanza kukutana leo kuhusu suala hilo ila niwatoe hofu mashabiki wetu kwani timu bado iko mikono salama, malengo yetu ni kuhakikisha tunafanya vizuri katika michezo yetu yote miwili iliyobaki,” amesema
Kocha msaidizi wa timu hiyo, Mathias Wandiba amesema bado ni mfanyakazi wa Geita Gold hadi mwisho wa msimu.
Kupoteza mechi dhidi ya Prisons na Mbeya City, kuliifanya Geita Gold kuporomoka kutoka nafasi ya tano hadi sita kwenye msimamo wa ligi.