Kwa mara ya kwanza kwenye historia yake, Tanzania Prisons inakwenda kuwa na mchezaji wa kigeni msimu huu 2023/24 ambaye wanamuita Messi Roland
Mchezaji huyo kutoka nchini Cameroon anacheza nafasi ya Ushambuliaji, alijizolea umaarufu kwenye michuano ya Mbeya Pre Season, huenda akamalizana na Tanzania Prisons baada ya kocha mkuu, Fred Felix ‘Minziro’ kukubali kiwango chake.
Timu hiyo imekuwa na utamaduni wa kutumia wachezaji wazawa sikuzote kama njia ya kukuza vipaji lakini kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.
Nyota huyo mrefu na mwenye mwili mkubwa, alikuwa kivutio kwenye michuano hiyo iliyomalizika juzi Jumatano (Agosti 02) wilayani Kyela mkoani hapa kutokana na kimo na uchezaji wake wa chenga za maudhi.
Minziro amesema licha ya baadhi ya mechi kucheza chini ya kiwango kutokana na uchovu wa michezo ya mfululizo na majeraha aliyokuwa nayo, lakini alionesha uhai uwanjani hadi kuisadia timu kutwaa ubingwa wa michuano hiyo.
“Sitaki kumzungumzia zaidi, lakini naamini kila mmoja amemuona alichofanya, binafsi naweza kusema msimu ujao wa Ligi Kuu ataichezea Tanzania Prisons, niwapongeze wachezaji wote kwa kufanya vizuri na kutwaa ubingwa,” amesema Minziro.
Kwa upande wake nyota huyo amesema ikiwa ni mara yake ya kwanza kutua nchini, uwezo anao japokuwa hatma yake ipo kwa kocha ambaye ataamua kuwa naye au kumtosa.
“Nafikiri wameona nilichokifanya na nimefurahishwa na mashabiki walivyonishangilia uwanjani huenda wameona kitu tofauti hivyo nasubiri uamuzi wa kocha kama ataridhia kuwapo kikosini,” amesema nyota huyo.