Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hatimaye Simba yafanikiwa kumbakisha Ayoub, lakini Inonga ....!

Ayoub Lakred Asepa Simba yafanikiwa kumbakisha Ayoub Lakred

Wed, 15 May 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Katika kuhakikisha inakuwa na kikosi imara kwenye msimu ujao, uongozi wa Simba umeanza mchakato wa kuhakikisha inambakisha kipa wake chaguo la kwanza, Ayoub Lakred, kwa kumpa mkataba mpya wa miaka miwili ya kuendelea kuitumikia klabu hiyo ya Msimbazi.

Mbali na Lakred, taarifa kutoka Simba zinasema mabosi wa timu hiyo pia wameweka wazi hakuna ofa rasmi kutoka katika timu yoyote kwa ajili ya kuhitaji huduma ya beki wao Mkongomani, Henock Inonga.

Lakred, nyota raia wa Morocco, alisaini mkataba wa mwaka mmoja ambao unafikia tamati mwisho wa msimu huu.

Taarifa zilizopatikana jana zinasema  viongozi wamekamilisha mazungumzo na kipa huyo ataendelea kusalia Msimbazi baada ya kukubali kuongeza mkataba wa miaka miwili.

"Mambo yameenda vizuri kwa upande wa Lakred, viongozi wamefanya mazungumzo naye na ameridhia kubakia Simba, atasaini mkataba mpya wa miaka miwili wa kuitumikia klabu yetu," kilisema chanzo chetu.

Kuhusu Inonga, chanzo chetu kilisema bado beki huyo ataendelea kusalia Wekundu wa Msimbazi kwa sababu hakuna ofa iliyopelekwa ikihitaji huduma ya Mkongomani huyo.

“Kuna baadhi ya wachezaji ambao mikataba ilifikia tamati wameongezewa, akiwamo Kibu (Dennis) na Israel Mwenda tayari wameshasaini mkataba wa miaka miwili kila mmoja ili kuendelea kusalia ndani ya Simba.

Kuhusu Chama (Clatous), bado amewekewa ofa mezani jukumu iliyobakia ni mchezaji mwenyewe kama ama atasaini au kama akiona haina maslahi kwake amepewa baraka zote za kwenda kupata changamoto nyingine huko aendako,” kiliongeza chanzo hicho.

Kilisema pia usajili mpya wamekamilisha kuwapa mkataba wa miaka miwili, beki wa Coastal Union, Lameck Lawi huku safari ya kwaheri ikinukia kwa kiungo mshambuliaji, Saido Ntibazonkiza.

Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amekiri kufanya mazungumzo na baadhi ya wachezaji waliomaliza mkataba akiwamo Lakred.

“Kuhusu wachezaji waliomaliza mikataba yao, tunaendelea na mazungumzo ili kuhakikisha tunawabakiza, suala la kocha mchakato unaendelea kwa kufuata mapendekezo yetu ni aina gani ya mwalimu tunayemhitaji,” alisema Ahmed. 

Simba kwa sasa iko chini ya Juma Mgunda baada ya aliyekuwa Kocha Mkuu, Abdelhak Benchikha, kurejea kwao kutokana na matatizo ya kifamilia.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live