Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hatimaye Simba wamlipa Matola kila kitu

MATOLA MISRI Selemani Matola

Mon, 6 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Jana tuliona jinsi ambavyo Matola alianza maisha yake ya soka kwao Kigoma akiwa kwenye timu ya mtaani,Tukaona jinsi alivyoondoka na kujiunga na Kagera Stars, leo tunaangalia namna alivyopewa fedha za nauli na Simba akaenda nazo kwao badala ya kwenda Dar kusaini mkataba, kuna mambo mengi kabla hajasaini mkataba. Unajua nini kilitokea alipokutana na Kassim Dewji, shuka nayo....

SIMBA WATANGAZA KWENYE SPIKA KUMTAFUTA MATOLA

Matola anasema walisafiri kwa treni kwenda Tabora na muda mwingi alikuwa amesinzia ndani ya treni, lakini jambo la tofauti linatokea baada ya kufika kwenye kituo cha mwisho wakati wanashuka.

“Tukiwa tunashuka nikasikia tangazo kutoka kwenye spika za pale kituoni kuwa mgeni anayeitwa Suleiman Matola mwenyeji wake anamsubiri ofisini, kocha akaniuliza kama nina mgeni nikamwambia hapana, akasema twende wote, tukaenda nilipofika nilimkuta meneja ya Breweries wa kipindi hicho pale Tabora, akaniomba niende ofisini kwake kocha akaniruhusu, nikampa mabegi yangu nikaenda.

“Tulipofika ofisini kwake akaniambia amepigiwa simu na kiongozi wa Simba Khalfan Matumla, amemwambia natakiwa kwenda Dar es Salaam baada ya kumaliza mechi nikasaini mkataba, nikamwambia sawa hakuna shida akanipa laki moja kwa ajili ya nauli, nikachukua hela nikaweka mfukoni na kuondoka zangu.

AGOMA KWENDA DAR, ATIMKIA KIGOMA

“Baada ya mechi, sikwenda Dar na ukumbuke Yanga walisema watamtuma mtu kunifuata, sikumuona mtu wao, baada ya mechi nikapanda treni kwa kutumia nauli ya Simba na kuondoka, sikwenda Dar, nilienda zangu Kigoma kumsalimia mama yangu.

“Baada ya wiki mbili nikampigia simu yule kiongozi wa Simba na kumsalimia, aliongea maneno kumi kwa wakati mmoja, mwisho akaniambia mbona tunakusubiri sana, nikamwaambia baada ya siku mbili naenda Dar wakaniambia watakuja kunipokea nikifika niwaambie.

“Nikamuaga mama na kuondoka kwenda Dar na hapo ndiyo maisha ya soka yakaanza kubadilika, najua utauliza mbona nilikuwa siagi kutoka timu moja kwenda nyingine, wakati ule mkataba ulikuwa ni mwaka mmoja tu msimu ukiisha nanyi mmemalizana, maisha yanaendelea.

KASSIM DEWJI AMCHUNIA

Matola anaendelea kusema kuwa maisha ya soka yana mambo mengi sana, anasema alitua Dar na kwenda kwa babu yake Ilala baadaye akamtafuta yule kiongozi wa Simba ambaye anamkumbuka kwa jina la Matumla akamwambia aende kesho yake.

Alipokwenda alitakiwa kwenda kwenye ofisi ya Kassim Dewji ambaye ndiye alikuwa anasimamia usajili wa Simba wakati huo, ofisi yake ilikuwa pale Posta kwenye Mgahawa wa Food World.

“Nilienda pale mara ya kwanza Dewji akaniambia niende kesho yake, nikaenda tena nikamkuta na mtu anayeitwa Suleiman Mathew ofisini kwake akaniambia niende kesho yake, kesho zikawa nyingi sana baada ya kuchoka kwenda nikaghairi sikwenda tena.

“Ukapita muda nikakutana na yule kiongozi wa Simba nikamweleza kila kitu kilivyotokea, akasema lazima nitacheza Simba kwa kuwa Kassim anasajili tu lakini mwisho wa siku lazima zile fomu zitafika kwake, nikauliza na kuelezwa kuwa Simba wakati huo walikuwa wanasajili kwa kitita cha shilingi milioni tatu zilikuwa hel nyingi sana kwangu kumbuka huko nyuma hela ya mpira niliyokuwa nashika ilikuwa laki na laki na nusu, basi siku moja nikiwa naangalia mechi ya Kombe la Mapinduzi, nakumbuka Yanga ndiyo walikuwa wanacheza na timu moja kutoka Zanzibar, baada ya mechi nikatoka nje, mara nyingi wakati wa mechi zilizokuwa zinapigwa Uwanja wa Uhuru, pale nje watu walikuwa wanakaa kidogo kabla hawajaenda majumbani kwao, nilipotoka hapo nikakutana na Mathew akanimbia Dewji ananitafuta yupo ndani uwanjani tumsubiri.

“Akaingia ndani akamwita na kumwambia kuwa nipo nje, akaja akaniambia asubuhi niende ofisini kwake, nikaenda nilipofika akaniambia alikuwa hanifahamu sana lakini amenifuatilia na ameshagundua kuwa ni mchezaji mzuri baada ya kuulizia, akaniuliuza kama nipo tayari, nikamjibu ndiyo.”

ASAJILIWA SIMBA KWA LAKI MOJA

Matola anakumbuka, akiwa na Kassim ambaye alikuwa anasajiliwa watu wake ili baadaye agombee ukatibu kwenye timu hiyo, kilitokea kizuizi kingine, baada ya bosi huyo kumwambia kuwa hela ya usajili kwa muda huo hakuna.

“Nikiwa pale Kassim akatoa sh laki moja na kuniwekea mezani, akaniambia wameshasajili wachezaji wengi sana na fedha zimeisha, hela iliyopo kwake kwa wakati huo ni sh laki moja tu kama nipo tayari kusaini basi nifanye hivyo, huwezi kuamini nilikuwa nina shida kweli lakini ingekuwa ngumu kwangu kusaini kwa laki, kwa kuwa nilikuwa nafahamu Mohammed Dewji ndiye alikuwa ameanza kazi ya ufadhili Simba na alikuwa anatoa fedha nyingi sana za usajili.

“Nikagoma, nikamjibu kuwa ngoja nienda nikajifikirie kwanza halafu nitarudi tena kwake, nikiwa nashuka chini nikakutana mzee mmoja tunafahamiana anaitwa Adam Mgoyi, huyu mzee kwa sasa ndiye mdhamini wa mali za Simba, akaniuliza mbona nimepooza sana, nikamweleza kila kitu kichotokea, akaniambia hapa ni mjini, nirudi kwa Kassim nikasaini kama riziki ni yangu nitaipata tu.

Anasema baada ya kuelezwa na yule mzee alirudi juu kwa Kassim na kumweleza kuwa amekubali akasaini mkataba wa miaka miwili na kupewa shilingi laki moja na mpira akaondoka.

“Sikumbuki kama kila mtu alikuwa anapewa mpira, lakini nakumbuka baada ya kusaini Kassim alinipa laki moja na mpira mzuri tu, nikauchukua na hela yangu nikaweka mfukoni nikaondoka zangu, nikafika Ilala, kesho yake nikaenda Kigoma kwa kuwa muda wa ligi ulikuwa bado.

AKUTANA NA SAID MAULID KAMBINI

Matola anasema baadaye alipigiwa simu kuwa muda kwa kuingia kambini umefika hiyo ilikuwa mwaka 2000, akaaga kwao Kigoma na kurudi Dar ambapo alitakiwa kwenda kambini, lakini wachezaji wote wageni walikuwa wanakaa kwenye Lodge ya kiongozi mmoja wa Simba wakati huo inaitwa Saanan Lodge.

“Nilipofika Dar nilipokelewa na viongozi wa Simba na kupelekwa moja kwa moja Lodge ambapo nilimkuta pia Said Maulid ambaye alitokea timu moja ya mkoani Kigoma angalau nikawa na mtu wa kupiga naye stori.

“Simba wakati huo ilikuwa na wachezaji wengi sana mastaa, nakumbuka wakati naingia Simba ilimuajiri kocha kwa sasa ni marehemu, alikuwa anaitwa Nziyosaba Tauzany wakati huo alikuwa anatokea Majimaji ya Songea ambapo alikuja na wachezaji wake kadhaa, akiwemo Amri Said, Willy Martin, Ally Moparwa, Patrick Betwel na Jemini Kiiza.

“Baada ya siku tatu kambini, tulitakiwa kwenda mazoezini, Simba ilikuwa na uwanja pale Jangwani wakati huo ndiyo sehemu ambayo tulifanya mazoezi, tukachukuliwa na kwenda mazoezini ambapo timu ilikuwa na mastaa wengi sana wakubwa, tukafanya mazoezi pale lakini niliona tofauti kubwa sana ya kule nilipokuwa na Simba kwani mazoezini tu mashabiki walikuwa wengi kuliko hata wale ambao walikuwa wanaingia kwenye mechi zetu kule mikoani.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live