Wakati Ligi ya Championship ikiwa imesalia michezo mitatu ili kufikia tamati mambo yamekuwa magumu kwa Ndanda baada ya uongozi kueleza kujitoa kwenye ligi hiyo.
Ndanda imekuwa haifanyia vizuri kwenye ligi hiyo kuanzia mwanzoni na sasa inaonekana kuamua kuachia ngazi rasmi.
Katibu wa timu hiyo, Seleman Kachele alisema moja ya sababu iliyowafanya kutoendelea na ligi ni ukata wa fedha na wameshindwa kuiendesha timu hiyo maarufu nchini Tanzania.
Alisema walifanya juhudi kubwa kwa kushirikisha wadau namna ya kupambania timu iweze kumaliza ligi lakini imekuwa ngumu.
Jana timu hiyo ilikuwa icheze dhidi ya Copco katika Uwanja wa Nyamagana, Mwanza lakini Ndanda haikufanikiwa kusafiri kwa kukosa fedha.
"Kweli suala hilo lipo na tayari tumeruhusu wachezaji kuondoka sababu mambo yamekuwa magumu kwetu na tunaangalia namna nyingine kwa wachezaji waliobaki.
"Hadi kufikia uamuzi huo basi ujue hali imekuwa sio nzuri kwetu na tumejitahidi kufika hapa tulipo lakini sasa hatuna namna ya kufanya," alisema Kachele.
Ndanda inafikia hatua hiyo ikiwa imesalia michezo mitatu dhidi ya Biashara United, Pan African yote ugenini huku mchezo mmoja dhidi ya Transit Camp ingekuwa nyumbani katika mchezo wa mwisho wa ligi.
Ndanda inajitoa kwenye Ligi ya Championship ikiwa inashika nafasi ya 15 baada ya kuvuna alama 15 ambayo inaifanya kushuka daraja moja kwa moja.
Ikumbukwe Gwambina nayo ilijitoa kwenye ligi hiyo ikiwa mzunguko wa kwanza unaelekea ukingoni kwa madai ya kuonewa kila wakati na mamlaka ya soka nchini.
Huu umekuwa msimu wenye matatizo mengi kwa timu kujitoa kwani Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) Mbinga United ilijitoa, First League Njombe Mji ilijitoa na Ligi ya Championship sasa timu mbili zinakuwa zimejitoa.