Baada ya juhudi za kumshawishi kuendelea kuitumikia timu yao kukwama, uongozi wa Klabu ya Yanga, umefikia makubaliano ya pamoja kumweka sokoni Mshambuliaji wao kutoka DR Congo Fiston Mayele, imefahamika.
Mayele ambaye amebakiza mkataba wa mwaka mmoja, alikuwa kwenye mvutano na uongozi wa klabu yake kwa kufanya vikao kadhaa kabla ya juzi Jumatatu (Julai 10) kufanyika cha mwisho, lakini mshambuliaji huyo raia wa DR Congo akashilia msimamo wake wakuiomba Yanga kumuuza kwa moja kati ya klabu zinazomhitaji huduma yake.
Uongozi wa klabu ya Yanga umeendelea kusisitiza hautaongeza ofa tena kwani ofa waliyompatia Mayele ni kubwa mnoo.
Pia, uongozi wa klabu ya Yanga SC wamewapa siku tano wanaomsimamia Mayele kuamua hatma yake ndani ya klabu ya Yanga SC na wamewapa machaguo mawili, kusaini mkataba mpya kwa ofa ile ile au kumuuza nje ya nchi kwa dau lisilopungua dola 900,000 (zaidi ya bilioni 2 za Kitanzania).
Ingawa uongozi wa Yanga haukuwa tayari kuweka hilo bayana, chanzo chetu ndani ya kamati yao ya utendaji, kimeeleza kuwa wamefikia uamuzi wa kumuuza kutokana na msimamo wake.
Aidha, kimesema kwamba mbali na Klabu ya Zamalek, Pyramids (za Misri) na Esperance Sportive de Tunis kuonyesha nia ya kumsajili, pia kuna klabu moja ya Saudi Arabia ipo tayari kutoa Sh. bilioni mbili za Tanzania ili kuinasa saini ya nyota huyo aliyeongoza kwa ufungaji Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho Afrika.
“Ni kweli Mayele alikutana na viongozi juu ya mustakabali wake wa kuendelea kwa msimu ujao na makubaliano yaliyofikiwa ni nyota huyo kuuzwa,” kimeeleza chanzo hicho.
Hivi karibuni Mayele aliweka wazi kuwa atakuwa na mkutano wa mwisho na uongozi wa Young Africans na juzi Jumatatu (Julai 10), walikutana na kufikia maamuzi hayo.