Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hatima ya Vipers mikononi mwa Robertinho

Robertinho Dubai 1 Robertinho

Fri, 24 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kikosi cha Simba kilicholazimisha sare ya 1-1 na Azam FC juzi, kimeondoka jana kwenda Uganda kwa mchezo wa tatu wa Kundi C wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Vipers, huku kocha wa timu hiyo ya Msimbazi, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amesema amelipanga jeshi lake kuhakikisha wanazichukua pointi zote sita.

Simba ililazimisha sare kwa kukomboa bao katika dakika ya 90 kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara ikiwa ni siku chache tangu ifumuliwe mabao 3-0 na Raja Casablanca ya Morocco katika mechi ya CAF, lakini kocha huyo amesema wamesahau kila kitu na akili zao sasa zipo kwa Vipers anayoijua kwani ameitumikia kabla ya kuja Simba.

Kocha huyo alisema anajua huenda wapinzani wao hao wakawa na mabadiliko tofauti na alivyoiacha, lakini wamepania kukomba pointi sita za mechi zao mbili zinazofuatana kwani ndizo zilizoshikilia hatma yao kundini kwa ajili ya kutinga robo fainali ya michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Robertinho alisema anawashukuru mashabiki zao ambao wameendelea kuwapa sapoti katika kipindi chote licha ya kutopata kile ambacho walikikusudia tangu mwanzoni.

“Tulitengeneza nafasi nyingi na kama tungekuwa makini kwenye kuzitumia basi tungekuwa na nafasi kubwa ya kushinda, nawashukuru wachezaji kwa jitihada zao hivyo tunaangalia mchezo wetu ujao,” alisema na kuongeza;

“Ni kweli katika michezo mitatu tumekuwa na matokeo yasiyoridhisha na kila mmoja wetu ameumia ingawa hatutakiwi kuendelea kuangalia nyuma bali tufanye linalowezekana kuhakikisha tunapata ushindi na Vipers.”

Alisema mechi mbili dhidi ya Vipers ndizo zenye kutoa dira kwa Simba kwenda robo fainali, hivyo wanaenda wakiwa wamejipanga kuhakikisha wanapata ushindi ugenini wikiendi hii kabla ya kurudi nyumbani kumalizana nayo na kuisubiri Horoya AC ya Guinea kwa mechi ya wiki ijayo.

“Naifahamu Vipers vizuri kwa sababu nimewahi kuifundisha lakini ni mechi nyingine ngumu kutokana na wao pia wana kocha mzuri, hivyo naamini inaweza kuwa bato ya mbinu zaidi tofauti na matarajio ya wengi wanavyoiona,” alisema Robertinho.

Pia kocha huyo alifafanua kwanini hakuwatumia wachezaji wake wote katika mchezo na Azam kwani wengi wao hawakupata muda mzuri wa kupumzika baada ya mechi yao iliyopita ya hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Raja Casablanca.

“Tulikuwa na kipindi kifupi sana cha maandalizi kutoka mchezo mmoja hadi mwingine na tunatambua nguvu kubwa iliyotumika hivyo wachezaji wetu wengine waliokosekana tuwategemee katika mchezo ujao ili kuongeza morali ya timu,” alisema.

Sare na Azam inaifanya Simba kucheza michezo mitatu mfululizo bila ya ushindi baada ya awali kupoteza mechi mbili za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Horoya kwa bao 1-0 na 3-0 na Raja Casablanca.

Robertinho kabla ya kujiunga na Simba Januari 3, mwaka huu alikuwa na Vipers ambayo aliiwezesha kufuzu hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza katika historia tangu ilipoanzishwa 1969.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live