Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hatihati Euro 2024 inawezekana wakaikosa

Haaland Norway Erling Haaland

Sat, 18 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

MECHI za kufuzu michuano ya Euro 2024 zinaendelea barani Ulaya na baadhi ya nchi zimefanikiwa kufuzu kushiriki michuano hiyo, huku zingine zikiendelea kupapatuana kwani hazina uhakika wa kupenya.

Katika upande wa timu ambazo hazina uhakika wa kushiriki mashindano hayo makubwa kabisa kwa ngazi ya nchi katika soka arani humo, zimebeba mastaa kibao ambao wameonekana kufanya vizuri kwenye klabu tangu kuanza kwa msimu huu.

Mastaa hawa ni tegemeo kwenye timu zao, lakini mataifa yao yapo kwenye hatihati ya kushiriki fainali hizo na mengine yameangukia kwenye hatua ya mtoano ili kufuzu. Hawa hapa ni baadhi ya nyota ambao huenda wakakosekana kwenye michuano hiyo ifikapo mwakani.

Erling Haaland, Martin Odegaard (Norway)

Mwaka jana hawakuwapo kwenye michuano ya Kombe la Dunia licha ya kwamba walionyesha viwango bora wakiwa na klabu zao.

Haaland msimu uliopita akiwa na Manchester City alitwaa tuzo ya Gerd Muller kwa kuwa mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi barani Ulaya ndani ya msimu mmoja.

Kwa upande wa Odegaard ni miongoni mwa mastaa waliofanikiwa kuiwezesha Arsenal kufanya vizuri msimu uliopita kwenye upande wa Ligi Kuu England.

Nyota hao na Norway yao hawataweza kufuzu moja kwa moja, lakini wanaweza kufuzu kupitia hatua ya mtoano.

Gianluigi Donnarumma, Destiny Udogie (Italia)

Mbali ya kushinda taji la michuano ya Euro 2021 walishindwa kufuzu kucheza Kombe la Dunia mwaka uliofuatia.

Donnarumma kwa sasa anatajwa kuwa mmoja kati ya makipa bora Ulaya kutokana na kiwango alichoonyesha akiwa na AC Milan na PSG.

Pia ndiye aliyesimama langoni wakati Italia inachukua taji la Euro kwa changamoto ya mikwaju ya penalti dhidi ya England katika Uwanja wa Wembley.

Kwa upande wa Udogie, hakuwa mmoja kati ya wachezaji waliounda kikosi cha Euro 2021, lakini kwa sasa ni mmoja kati ya mastaa tegemeo wa kikosi cha kocha Ange Postecoglou akiwa na Tottenham Hotspur na ubora wake umemfanya kuitwa timu ya taifa.

Italia inashika nafasi ya tatu katika kundi lake na imejihakikishia kucheza hatua ya mtoano ili kufuzu, lakini haina uhakika wa kufuzu moja kwa moja.

Luka Modric, Josko Gvardiol (Croatia)

Modric amekuwa mmoja kati ya wachezaji tegemeo ndani ya Real Madrid na hata timu ya taifa ya Croatia.

Hii ni sawa na ilivyo kwa Josko ambaye kwa sasa anatajwa kuwa mmoja kati ya mabeki bora barani Ulaya akiwa Man City.

Nyota hao waliisaidia Croatia kumaliza nafasi ya tatu kwenye michuano Kombe la Dunia 2022.

Kwa sasa Croatia inashika nafasi ya tatu kwenye kundi D na ili kufuzu Euro 2024 kwa kumaliza nafasi mbili za juu itatakiwa kushinda mechi mbili za mwisho dhidi ya Latvia na Armenia na ikishindikana itaangukia kwenye mechi za mtoano.

Alexander Isak, Dejan Kulusevski (Sweden)

Hakuna ubishi juu ya kiwango bora cha Alexander Isak ambaye ameendelea kuonyesha makali tangu ajiunge na Newcastle United akitokea Real Sociedad.

Supastaa mwingine kwenye kikosi hicho cha Sweden ni Dejan Kulusevski ambaye anafanya vizuri akiwa na Tottenham Hotspur. Ili kuonekana kwenye Euro 2024 wanatakiwa kuisaidia Sweden kufuzu kupitia hatua ya mtoano baada ya kushindwa kupenya moja kwa moja.

Robert Lewandowski (Poland)

Hakuna ubishi juu ya uwezo wa Lewandowski kufunga mabao kwani keshaonyesha akiwa na timu mbalimbali ikiwa pamoja na Borussia Dortmund, Bayern Munich na sasa Barcelona. Straika huyo raia wa Poland mwenye umri wa miaka 35, nchi yake italazimika kushinda mechi ya mwisho na kuziombea mabaya Albania na Jamhuri ya Czech kufanya vibaya mechi za mwisho. Ikishindikana itatakiwa kuangukia kwenye hatua ya mtoano.

Evan Ferguson (Ireland)

Huwezi kuyataja majina ya wachezaji vijana wanaofanya vizuri kwenye Ligi Kuu England ukaacha jina lake. Ferguson, 19, ni miongoni mwa wachezaji tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Brighton and Hove Albion.

Nchi yake, Ireland ina wakati mgumu wa kufuzu kucheza Euro 2024 ikiwa inashika nafasi ya nne kwenye kundi B na namna pekee ambayo inaweza kuwafanya wafuzu ni kucheza hatua ya mtoano ambapo bado haina uhakika wa asilimia, hiyo itategemea na matokeo ya mwisho ya timu nyingine.

Chanzo: Mwanaspoti