Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hata wewe ungekuwa Nabi ungeondoka Yanga

Nasreddine Nabi 123 Nasreddine Nabi

Mon, 19 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ilianza kama tetesi na baadaye ikawa kweli. Ndoa ya Yanga na Mohamed Nabi ikavunjika rasmi katikati ya wiki. Ni huzuni kubwa sana.

Nabi ni Profesa wa mpira. Pamoja na jeuri ya pesa za GSM, Nabi amekuwa sehemu kubwa ya mafanikio ya Yanga kwa miaka hii miwili.

Alipotua Yanga aliikuta timu ikiwa kwenye hali mbali. Ilikuwa imetimiza miaka minne bila kushinda taji lolote la maana. Ni aibu kubwa.

Mambo yalikuwa ni magumu kwa Wananchi. Walipambana lakini Simba ilikuwa katika kilele cha ubora wake. Ilikuwa ni jambo gumu sana kuwashinda.

Jeuri ya fedha za Mohamed Dewji ziliifanya Simna iwe katika mafanikio ya hali ya juu sana. Ni katika zama hizi ambazo Yanga waliteseka.

Ujio wa Nabi miaka miwili nyuma ukaanza kuleta mabadiliko ya kiuchezaji. Akasuka timu imara taratibu. Ndio nyakati ambazo kina Fiston Mayele, Khalid Aucho, Yannick Bangala na wengineo walisajiliwa.

Yanga ikamaliza msimu uliofuata kibabe sana. Ikaurejesha ubingwa Jangwani tena kwa rekodi ya aina yake ya kutokupoteza mchezo wowote.

Ilikuwa ni ngumu sana kupata matokeo mbele ya Yanga ya Nabi. Walikuwa na safu ya ulinzi imara sana. Golini Djigui Diara alikuwa katika ubora wa hali ya juu. Ungewezaje kutoka mbele ya Yanga?

Mbali na Ligi Kuu Bara, Yanga walishinda pia Ngao ya Jamii na Kombe la Shirikisho la Azam katika msimu huo wa kwanza wa Nabi.

Bahati mbaya ni kwamba katika mashindano ya Kimataifa Nabi hakuingia na mguu mzuri. Alipoteza mechi zote mbili dhidi ya Rivers United na kuondoshwa kinyonge katika Ligi ya Mabingwa.

Hili ndio Lilikuwa deni kubwa la Nabi pale Yanga msimu huu. Yanga mbali na kurejesha Ufalme wao hapa ndani walitaka pia kuweka rekodi za kibabe huko Afrika.

Na hapa ndipo hoja yangu ya kuondoka Nabi inapopata mashiko. Yanga haikuwahi kufika fainali yoyote ya mashindano ya Afrika lakini wamefika chini ya Nabi.

Amewapeleka katika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika tena kwa rekodi za Kibabe. Amezifunga timu kubwa za Afrika nyumbani na ugenini.

Nani amesahau dhahama aliyofanyiwa TP Mazembe pale kwa Mkapa kisha akaenda kuaibisbwa Lubumbashi? Hii ndio Yanga ya Nabi. Ingekufanya chochote inachojisikia.

Mbali na rekodi hiyo ya Afrika, Nabi ametetea pia mataji ya ndani aliyoshinda mwaka jana. Ametetea Ngao ya Jamii, Ligi Kuu na FA. Mungu akupe nini tena.

Ukiachana na Yanga kuwa katika kilele cha mafanikio yake, Nabi pia ameweka rekodi bora katika maisha yake ya Soka. Angebaki Yanga kufanya nini tena?

Kazi kubwa kwa Nabi sasa ni kushinda ubingwa wa Afrika na hilo gumu sana kufanya ukiwa na Yanga. Imetokea kama bahati tu msimu huu. Ni wazi itachukua muda rekodi hii kujirudia.

Pili ni wazi kuwa mafanikio ya Nabi msimu huu yanatakiwa kumpeleka hatua kadhaa mbele katika kazi yake ya ukocha. Ni wakati wake kupata dili kubwa zaidi. Ni wakati wake kufundisha timu kubwa zaidi.

Ni wazi sasa timu nyingi za Afrika sasa zinatamani kuwa na kocha wa aina yake. Anaweza kupata kazi popote Afrika.

Changamoto inabaki kwa Yanga sasa kumpata mrithi sahihi wa Nabi. Ni nyakati ngumu kwao kuziba nafasi yake. Ila kwa fedha za GSM wanaweza kufanikiwa.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: