Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hata uwanja wa CCM Kirumba unaweza kuwa kama New Amaan

Uwanja Wa CCM Kirumba 1140x640 CCM Kirumba

Fri, 29 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Juzi Jumatano, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hussein Ali Mwinyi alizindua Uwanja wa Amaan. Uwanja huo umefanyiwa ukarabati na kuwa bora zaidi kuliko ulivyokuwa awali.

Serikali ya Mapinduzi imeufanya uwanja huo kuingia kwenye viwanja bora ambavyo vinaweza kutumika kwa mechi za kimataifa zinazosimamiwa na Shirikisho la Soka la Afrika (Caf).

Uwanja huo ambao sasa unaitwa New Amaan Complex umekuwa bora zaidi kuliko viwanja vyote vya Tanzania Bara, ukiondoa Uwanja wa Benjamin Mkapa ambavyo navyo vinaweza kuboreshwa na kuwa na hadhi ya kimataifa.

Mwanaspoti tunasema hivyo kwasababu, Tanzania Bara kwa sasa inategemea viwanja vya Benjamin Mkapa na wakati mwingine Azam Complex kwa ajili ya mechi za kimataifa.

Juzi Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) liliufungia Uwanja wa Uhuru kutokana na kukosa sifa. Baada ya tukio hilo, Serikali ya Tanzania Bara chini ya Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo ikaufungia pia Uwanja wa Benjamin Mkapa. Kitendo hicho kilichozua taharuki kwa timu za Simba, Yanga na Al Hilal ya Sudan ambazo zimekuwa zikiutumia Uwanja wa Mkapa kwa ajili ya mechi za kimataifa. Pia, taharuki ilikuwa kwa timu za Ligi Kuu zilizokuwa zikiutumia Uwanja wa Uhuru kwa ajili ya mechi za nyumbani.

Tofauti na Zanzibar, Tanzania Bara ina viwanja vingi  vinavyoweza kufanyiwa ukarabati na kuondoa taharuki zisizokuwa na msingi na kuliwezesha taifa siku za usoni kuandaa Afcon bila ya kuomba ushirikiano na nchi za majirani za Kenya na Uganda.

Viwanja vingi vinavyotumiwa kwenye Afcon havichukui watazamaji wengi, vingi vina sifa ya kubeba watazamaji ishirini elfu na si zaidi sana na hapo. Uwanja wa Amaan kabla ya ukarabati ulikuwa na uwezo wa kuchukua watazamaji kumi na mbili elfu tu lakini sasa una uwezo wa kuchukua watazamaji kumi na tano elfu.

Ukija Tanzania Bara Uwanja wa CCM Kirumba uliopo Mwanza una uwezo wa kuchukua watazamaji Ishirini elfu unaweza kufanyiwa ukarabati na kuwa wa kisasa na kuongeza idadi ya watazamaji wa kwa wakati mmoja. Pia, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Kaluta uliopo Arusha, Viwanja vya Jamhuri Dodoma na Morogoro pia vinaweza kufanywa kuwa vya kisasa.

Kama haitoshi Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi uliopo Tabora ambao inadaiwa ujenzi wake hajawahi kuisha tangu ulipoanza kujengwa unaweza kuboreshwa na kuwa mmoja kati ya viwanja bora  Afrika Mashariki. 

Rais Samia Suluhu Hassan alivizungumzia viwanja vinavyomilikiwa na CCM kufanyiwa ukarabati na kuwekewa nyasi bandia. Hatufahamu zoezi hilo hadi sasa limeishia wapi.

Tunaamini kama viwanja hivyo vilivyotajwa hapo juu kama vitafanyiwa ukarabati kama ule wa Amaan, Tanzania itapiga hatua kubwa kwenye sekta ya michezo.

Pia, tunaweza kuupumzisha Uwanja wa Benjamin Mkapa ambao umekuwa ukiombwa kutumiwa na timu za taifa na klabu za nchi jirani kwa ajili ya mechi za kimataifa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live