Mchambuzi mkongwe wa masuala ya soka nchini, Ibrahim Maestro amesema kuwa kikosi cha Timu ya Yanga ambacho kimechukua ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC msimu huu kina uwezo mkubwa wa kuchukua tena ubingwa huo msimu ujao iwapo hakutatokea changamoto zozote ndani ya kikosi.
Maestro amesema kuwa uongozi wa yanga ndio umekuwa mhimili mkubwa wa matokeo chanya ndani ya timu na ndiyo maana imekuwa rahisi kwa wachezaji, benchi la ufundi na watendaji wote wa klabu kuyaishi maono ya klabu ya kutaka mafanikio.
“Kama Simba aliweza kuchukua ubingwa mara nne mfufulizo, Yanga hashindwi kufanya hivyo. Unaweza kufanya kitu kizuri lakini kuendelea kufanya vilevile au zaidi ndiyo ikawa kazi ngumu. Ni jukumu la viongozi kusimamia hayo na kuhakikisha klabu inabaki kwenye ubora wake.
“Wana kazi ya kubakisha ubingwa wa ligi, ubingwa wa kombe la Shirikisho la CRDB na kufanya vizuri zaidi kimataifa kwa kuongeza vitu viache na kuyafanyia kazi mapungufu yao waliyoyaona msimu huu.
“Timu hii hii inaweza kucheza ligi kuu msimu ujao na ikachukua ubingwa tena kwa sababu ya timu jinsi ilikuvyo. Wengine matatizo yao yalikuwa yanajitokeza nje ya uwanja tumeyasikia kuna hiki mara kile, yalikuwa yanaingilia matokeo ndani ya uwanja.
“Siamini kama Yanga hawakuwa na matatizo ya ndani, ninaamini yalikuwepo lakini wakija uwanjani huoni wanakuja nayo uwanjani, wanafanya kile wanachotakiwa na mwisho wa siku wanapata ubingwa.
“Viongozi wao wamefanya kazi kubwa sana, wasingekuwa wao inamaana haya yote tusingeyaona. Tumewaona Rais wa yanga (Eng. Hersi Said) na Makamu wake (Arafati haji) kila mechi wamekuwepo kuwapa nguvu vijana wao,” amesema Maestro.