Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hata Yanga hawakuitaka Mamelodi Sundowns

Yanga Vs Mamelodi Hata Yanga hawakuitaka Mamelodi Sundowns

Sun, 17 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kuna nyakati huwa unaona kama dunia imekuangukia. Ni kama nyakati hizi ambazo Yanga imepangwa kucheza na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini katika mechi za robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ni mzigo mzito kwa Yanga. Hakuna timu yoyote Afrika kwa sasa inatamani kukutana na Mamelodi. Wapo kwenye ubora wa juu sana. Wanacheza soka safi na la kikatili. Sio Al Ahly ya Misri, Esperance de Tunis ya Tunisia wala Wydad Casabalanca ya Morocco inayotamani kukutana na Mamelodi kwa sasa. Ni timu iliyoundwa vyema na wachezaji mahiri. Ndio timu ya pili kwa matumizi makubwa ya fedha Afrika. Wanazidiwa na Al Ahly tu.

Kocha Rhulani Mokoena ameifanya Mamelodi kuwa timu ya kutisha uwanjani. Hawana uwanja wa nyumbani wala ugenini. Wanakufunga sehemu yoyote.

Kwenye ukanda huu wa Kusini mwa Jangwa la Sahara katika zama hizi Mamelodi ndio timu pekee ambayo imemfunga Al Ahly mabao 5-0 kisha baada ya miaka michache ikamfunga tena 5-2. Unawezaje kuwafunga mabingwa wa Afrika mabao hayo? Ni ngumu sana. Ila kwa Mamelodi wala sio jambo gumu.

Kwa kifupi, Mamelodi ndiye mpinzani mgumu zaidi kwenye zile timu nane zilizofuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa. Hakuna timu iliyokuwa inatamani kukutana nao. Ila bahati mbaya imeangukia kwa Yanga. Wana kazi kubwa mbele.

Mamelodi ndio mabingwa wa African Football League (AFL). Walibeba ubingwa huo mwaka jana kwa kuzifunga Petro de Luanda, Al Ahly na Wydad Casablanca. Unaweza kuona aina ya wapinzani ambao Mamelodi alishindana nao kutwaa ubingwa huo.

Ni wapinzani wagumu. Ndio timu zilizotawala katika soka la Afrika kwa miaka mingi. Wydad mwaka jana waliitoa Mamelodi kwenye nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa kwa bao la ugenini. Hata hivyo, walipokutana kwenye African Football League waliyatimba.

Uzuri ni kwamba mashabiki wengi wa Yanga wanafahamu ukweli kuwa katika robo fainali wamekutana na kitu kizito. Wana kazi kubwa ya kufanya kushindana na Mamelodi. Kazi ni kubwa ndani na nje ya uwanja, Inahitajika hamasa kubwa kwenye mechi ya mkondo wa kwanza kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa. Inahitajika mipango thabiti uwanjani namna ya kucheza kwa nidhamu dhidi ya Mamelodi. Yanga inatakiwa kuiheshimu Mamelodi kama timu kubwa.

Wakiingia kucheza na Mamelodi kama wanacheza na timu ya kawaida wanaweza kukutana na dhahama kubwa. Ule mnara wa 5G ambao wamekuwa wakiusimika kwa wapinzani ndani ya Ligi Kuu na michuano mingine wanayoshiriki ikiwamo Ligi ya Mabingwa huenda safari ukasimikwa Jangwani kama hawataiheshimu Mamelodi.

Wanatakiwa kukaba kwa nidhamu kubwa na kutengeneza mashambulizi ya kushtukiza. Wanatakiwa kuwa fiti kwa dakika zote. Wanatakiwa kupunguza makosa hasa katika eneo la ulinzi. Kwenye kushambulia katika nafasi chache watakazotengeneza inabidi wazitumie vyema. Kwa timu kama Mamelodi haiwezi kukuacha utengeneze nafasi nyingi sana.

Pia Yanga inatakiwa kupambana katika mechi zote mbili. Kusema kwamba mechi itakwisha kwa Mkapa ni kujidanganya. Ili uweze kuitoa Mamelodi ni lazima umudu kucheza vizuri mechi zote mbili.

Mwaka jana mechi ya mkondo wa kwanza dhidi ya Wydad ilikwisha kwa sare ya bao 1-1 kule Morocco. Mechi ya marudiano ikamalizika kwa sare ya mabao 2-2 pale Afrika Kusini na Mwarabu akashinda kwa faida ya bao la ugenini. Hii ndio maana halisi ya kucheza vizuri mechi zote mbili.

Yanga ikiweka hesabu zote kwa Mkapa kisha mambo yasiende vizuri, watakwenda kukutana na kitu kizito kule Afrika Kusini. Yote kwa yote itakuwa mechi bora kati ya Mamelodi ya Mokoena na Yanga ya Miguel Gamondi. Hii inachagizwa na kiwango bora cha Yanga msimu huu. Wamecheza vizuri katika mechi kubwa ikiwemo dhidi ya Al Ahly.

Kwa upande wa Simba huu ni msimu ambao wanatakiwa kuonyesha utofauti mbele ya Al Ahly. Wamekutana nao katika miaka ya karibuni. Ila kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ndio mara ya kwanza wanakutana katika hatua ya mtoano.

Mwaka jana walikutana kwenye African Football League na Al Ahly akashinda kwa bao la ugenini. Simba ilikaribia kuiduwaza Al Ahly, lakini wakashindwa kukaba vyema baada ya kutangulia kwa bao moja pale Cairo. Mwaka jana, Simba ilikaribia kuwatoa washindi wa pili wa Ligi ya Mabingwa, Wydad, katika hatua ya robo fainali. Mechi iliamuliwa kwa mikwaju ya penalti. Walikaribia lakini hawakusonga mbele. Mwaka huu wanatakiwa kutuonyesha kitu cha tofauti.

Wanakutana na Al Ahly ambayo ina mabadiliko kadhaa ya wachezaji katika kikosi. Bado haijakaa sawa katika uchezaji wake. Tuliona mechi mbili dhidi ya CR Belouizdad walizidiwa. Hivyo ni mwaka wa Simba kufanya kitu. Hawana utetezi tena.

Kama ni uzoefu wanao wa kutosha. Kama ni Al Ahly wamekutana nayo vya kutosha. Kama ni kocha wanaye mwenye wasifu mkubwa. Kama ni timu wanayo ya ushindani. Kwanini wasisonge mbele? Itakuwa ni swali kubwa ambalo wanatakiwa kutujibu.

Chanzo: Mwanaspoti