Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hata Kibadeni anaishangaa hat-trick yake

Kibaden Abdallah 'king' Kibaden

Mon, 17 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kama utani imetimia miaka 45 sasa tangu mchezaji mmoja alipofanikiwa kufunga magoli matatu ‘hat-trick’ kwenye Dabi ya Kariakoo.

Ilifungwa na Abdallah ‘King’ Kibadeni mwaka 1977. Ni miaka mingi sana. Kibadeni alifunga mabao hayo matatu wakati Simba ikiichapa Yanga 6-0. Nakumbuka enzi hizo nilikuwa bado mtoto mdogo kabisa. Rekodi zinaonyesha mechi ilipigwa Jumanne ya Julai 19, 1977 miezi michache tangu Tanu na Afro Shiraz Party vilipoungana na kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi (CCM). Insshangaza kidogo.

Ni kitambo sana. Enzi hizo kina Juma Kaseja, Mrisho Ngassa, Nadir Cannavaro, Kelvin Yondani na wengineo bado hawajazaliwa. Wamekuwa na wamecheza Simba na Yanga hadi kustaafu lakini bado rekodi ya Kibadeni inadumu.

Ni kweli kwamba kufunga mabao matatu kwenye Dabi ya Kariakoo imekuwa kazi ngumu kiasi hicho? Inafikirisha sana.

Simba na Yanga zimepitia nyakati ngumu tangu zamani. Kuna wakati timu moja inakuwa imara na nyingine dhaifu. Lakini pamoja na hayo hakuna mchezaji aliyeweza kufunga mabao matatu kwenye Dabi. Nchi imepata mastraika wengi wakubwa lakini hakuna aliyeweza kuvunja rekodi hiyo ya Kibadeni.

Wamepita kina Said Sued 'Scud' , Zamoyoni Mogela, Makumbi Juma 'Homa ya Jiji' a.k.a Bonga Bonga, Zubery Magoha, Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ na Joseph Kaniki 'Golota', Emmanuel Gabriel 'Batgol', Jerry Tegete, Mussa Hassan Mgosi, Mrisho Ngassa, Meddie Kagere na wengineo lakini bado rekodi ya Kibadeni inadumu mpaka leo.

Nini kinachangia mechi za Dabi ya Kariakoo kukosa hat trick kwa miaka zaidi ya 40 sasa? Ni swali gumu sana kuweza kulielezea.

Kwanini wachezaji wanaweza kufunga mabao matatu kwenye Dabi ya Afrika Kusini, Misri, Morocco, Jamhuri ya Kongo na nyinginezo na siyo ile ya Kariakoo? Ni swali gumu sana.

Pengine Watani hawa wa Kariakoo wanakamiana sana. Kila wanapoingia katika mechi wanawaza zaidi kuwakaba wapinzani kuliko kufikiria wao kufunga.

Pengine hili ndio limechangia kuwepo na ukame kwenye mechi hizi. Yaani mfano sasa Yanga wanawaza zaidi kumzuia Baleke asifunge kuliko kumsaidia Mayele afunge hat trick. Vivyo hivyo kwa Simba wanawaza kuhusu Mayele kuliko Baleke wao.

Bahati mbaya katika nyakati hizi wamepita makocha wengi wazuri lakini bado mechi hizi za Dabi ya Kariakoo hutawaliwa zaidi na viongozi kuliko benchi la ufundi.

Mfano nyakati fulani Emmanuel Okwi hata asingefanya mazoezi bado angepangwa katika Dabi ya Kariakoo. Nani angemuweka benchi? Ingekuwa ni vita kubwa kati ya benchi la ufundi na viongozi.

Ni kama wakati fulani Morrison alipokuwa pale Yanga. Angeweza akapangwa kwenye Dabi hata kama hakuwa sehemu ya timu kwa muda mrefu. Ni ajabu kweli.

Mechi za Dabi siku hizi zimebadilika sana. Wachezaji wanapewa ahadi kubwa ambazo zinapelekea mechi kuwa ngumu sana. Uwanjani wachezaji wanakamiana sana kama hakuna kesho.

Unaweza kusikia wachezaji wa Yanga wameahidiwa Sh100 milioni kama wataifunga Simba. Pia unaweza kusikia Mohamed Dewji amewaahidi mastaa wa Simba mamilioni endapo wataifunga Yanga.

Katika mazingira kama hayo unadhani mchezaji gani ataweza kufunga mabao matatu peke yake? Ni ngumu kuliko ugumu wenyewe.

Wapo wachezaji kama Okwi, Hamis Kiiza, Tegete, Mayele na wengineo wamewahi kufunga mabao mawili katika mechi moja ya Dabi, lakini bado hawakuweza kuifikia rekodi hii ya Kibadeni.

Huenda rekodi hii ikachukua miaka mingi zaidi ya tunavyotegemea. Ugumu wa Dabi hizi unaongezeka kila siku.

Licha ya timu kuendelea kusajili wachezaji mahiri, bado kuna mambo mengi yanazunguka Dabi ya Kariakoo ambayo huwezi kuyakuta katika nchi nyingine.

Mfano nje ya uwanja utakuta kuna mambo mengi ya kishirikina huwa yanaendelea katika mechi hizi. Watu wapo bize kwa Waganga.

Ubaya ni kwamba mambo haya wala hayafanyiki kwa kificho. Utayaona kuanzia kambini hadi ndani ya uwanja. Watu wanafanya bila aibu.

Ila yote kwa yote, bado tuna Dabi bora zaidi Afrika Mashariki na Kati. Tumewazidi wengi kwa kuwa na mechi yenye msisimko mkubwa ndani na nje ya uwanja.

Tuendelee kufurahia tulichonacho kwa sasa na kuongeza msisimko wa Dabi hizi zaidi na zaidi. Hata hivyo tumuache Kibadeni aendelee kufurahia rekodi yake kwa miaka mingi zaidi.

Chanzo: Mwanaspoti