Nchi ina Rais mmoja tu. Ni Samia Suluhu Hassan. Ndiye mwakilishi wa muumba wa ulimwengu hapa Tanzania. Tunamuombea maisha marefu.
Ni Rais wa kwanza Mwanamke kuwahi kutokea nchini hakuna aliyewahi kuwaza kama tungepata Rais Mwanamke katika zama hizi, lakini Samia ameweka historia.
Ukiachana na mambo mengi makubwa anayofanya katika sekta nyingine, kuna simulizi nzuri ya kusisimua kuhusu Rais Samia katika michezo.
Ni kama vile ameingia na nyota ya mafanikio ndani ya muda mfupi tu madarakani, sekta ya michezo imekua na mafanikio makubwa sana.
Ni katika wakati wake timu ya Tanzania imecheza Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya miaka 30. Yanga wameweka rekodi hiyo mwaka huu na kabla ya hapo ni Simba ilicheza fainali ya CAF 1993.
Uzuri ni kwamba katika mashindano ya CAF mwaka huu serikali imekuwa na mchango mkubwa sana. Kwanza, imeweka mazingira mazuri ya timu kucheza kwa ushindani.
Pili, Rais Samia akaweka zawadi ya mabao yatakayofungwa katika mechi zao, zawadi hii iliongezeka kadri timu ilivyosonga mbele. Yanga wakavuna zaidi.
Mwisho wa siku akamalizia kwa kutoa Ndege ya kuwapeleka Yanga kwenye mechi ya marudiano nchini Algeria. Ni historia.
Ni katika wakati wa Rais Samia timu ya Taifa ya Wanawake chini ya Umri wa Miaka 17 ilifika robo fainali ya Kombe la Dunia pale India.
Kwanza iliweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kutoka Tanzania kufuzu Kombe la Dunia. Pili katika michuano yenyewe ikafika hatua ya Robo Fainali. Ni historia ya kukumbukwa.
Ni katika wakati wake pia timu ya Taifa ya Wanawake ilibeba ubingwa wa COSAFA, timu ya Taifa ya Walemavu ikafuzu Kombe la Dunia. Ni historia nyingine.
Jambo la kusisimua zaidi ni hiki ambacho kimetokea majuzi. Rais Samia amemaliza sakata la Feisal Salum 'Fei Toto' ndani ya siku tatu tu. Ni wazi kuwa hata Fei haamini kilichotokea.
Sakata la Fei lilikuwa gumzo nchi nzima kila mtu alikuwa akizungumza lake, lakini ukweli mchungu ni kwamba ni miezi sita sasa nyota huyo yupo nje ya uwanja.
Hiki ndicho kilichokuwa kinamuumiza mchezaji mwenyewe na wapenda soka wote. Kipaji cha Fei kilikuwa rehani wengi tulimuona alipoitwa Stars mwezi Machi.
Hakuwa kwenye ubora wake.
Mchezaji mzuri ni yule anayecheza kila siku. Tena awe anacheza mechi nyingi za ushindani. Hiki ni kitu ambacho Fei amekikosa kwa miezi sita sasa.
Katika miezi hii sita Fei amefanya jitihada zote lakini hazikuzaa matunda.
Alianza kwa kuandika barua ya kuvunja mkataba na Yanga kisha kuwapa kiasi cha fedha kilichoandikwa katika mkataba endapo upande wowote ungetaka kufanya hivyo. Ila mambo yakaenda mrama. Kamati ya TFF ikasema Fei hakuwa na mamlaka ya kufanya hivyo.
Akaomba marejeo ya hukumu hiyo lakini bado mambo yakagonga mwamba. Akakata Rufaa lakini hakukuwa na jipya.
Mwisho wa siku akaomba Watanzania wamsaidie kumchangia fedha ili akakate Rufaa kwenye Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS). Huku ndiko kulikuwa tegemeo lake la mwisho.
Hata hivyo kasi ya michango ilikuwa ya kusuasua. Hakuwa na matarajio ya kumaliza sakata hilo mapema kabla ya msimu mpya kuanza.
Lakini Rais Samia amerahisisha kila kitu. Aliwaomba Yanga wakae mezani na kumaliza sakata hilo na Feisal. Msimamo wa mchezaji ulikuwa wazi. Alisema hataki tena kurejea Yanga. Ilikuwa wazi kabisa.
Yanga wakakubali ombi la Rais Samia na kulifanyia kazi mara moja. Wakamalizana na mchezaji. Wakamaliza tofauti zao. Kisha wakamuuza kwenda Azam FC. Kiroho safi kabisa.
Sakata limekwisha ndani ya siku tatu. Hata Fei mwenyewe hakutarajia mambo yangeweza kuwa mepesi namna hii.