Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hashim afunguka kuvunjwa rekodi kadi za njano Dabi

Mwamuzi Kadi Za Njano Hashim afunguka kuvunjwa rekodi kadi za njano Dabi

Wed, 26 Oct 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Mei 6, 2012 kwenye Uwanja wa Mkapa, Mwamuzi wa Mechi ya Watani wa Jadi, Hashim Abdallah alitoa kadi saba za njano pamoja na penalti tatu upande wa Simba rekodi ambayo haikuvunjwa upande wa kadi hizo hadi juzi ilipovunjwa na kutamka kwamba bado penalti.

Ukiwa ni msimu wa 10 tangu rekodi hiyo iweke, juzi Jumapili kwenye uwanja huo huo, watani Simba na Yanga wakicheza mechi ya Ligi Kuu Bara, Mwamuzi Ramadhan Kayoko alivunja rekodi ya kadi za njano iliyokuwa inashikiriwa na Hashim akitoa jumla ya kadi tisa za njano, mechi iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1.

Akizungumza Hashim alisema huwa inatokea kwa mwamuzi kutoa kadi nyingi kwenye mechi moja na hiyo inatokana na presha ya mechi inavyokuwa hasa hizi za dabi.

Hashim aliyetoa kadi hizo katika mechi ya ligi, Yanga ikifungwa mabao 5-0, na baada ya mechi hiyo mwamuzi huyo alistaafu fani hiyo huku akieleza kuwa ndoto yake kubwa kwenye uamuzi ilikuwa ni kuchezesha dabi ndipo astaafu.

“Kayoko amevunja rekodi yangu ya kadi, ametoa kadi tisa kwenye mechi ya watani, hii inatokana na ‘tension’ kubwa ya mchezo inavyokuwa, alitaka kuumudu mchezo kwa kutoa kadi za njano ili wachezaji wawe makini kwani ukirudia kosa linalofanana na hilo unapewa kadi nyekundu.

“Kila mwamuzi anapoingia uwanjani anakuwa na mbinu yake namna ya kuumudu mchezo,” alisema Hashim ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Kitengo cha Usalama TFF.

Katika mchezo huo, Simba ilipata kadi tano za njano zilizokwenda kwa Israel Mwenda, Mohamed Hussein, Mzamiru Yassin, Habibu Kyombo na Okrah wakati nne za Yanga zilikuwa za Djuma Shaban, Aziz Ki, Khalid Aucho na Feisal Salum ‘Fei Toto’.

Hashim aliweka rekodi hiyo ya watani tangu wakutane kwenye mechi za Ligi Kuu Bara mwaka 1965 huku Kayoko akiivunja ikiwa ni mechi ya 109 kuchezwa kwa timu hizo.

Mwaka 2005, aliyekuwa mwamuzi Othman Kazi alitoa kadi saba za njano kwa Simba na Yanga pamoja na nyekundu moja hivyo kuwa na jumla ya kadi nane katika mchezo mmoja. Kazi alitoa kadi hizo katika fainali ya Kombe la Tusker ikiwa ni mchezo wa fainali uliochezwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza. Mkurugenzi wa Sheria, Habari na Masoko, Boniface Wambura, alisema endapo timu inapata kadi za njano zaidi ya tano basi hupewa adhabu kwa mujibu wa kanuni.

Chanzo: Mwanaspoti