Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hashim: Huyu Kibu ni balaa, Kaseja si mchezo

Kibu Fgh Kibu Denis

Tue, 19 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Haikuwa rahisi kwa familia yake kukubaliana na kipaji chake. Anasema wazazi wake waliamini katika kusoma na hawakuwa na habari na kipaji chake cha soka.

Huyu si mwingine bali ni Hashim Mussa, kipa wa timu ya soka ya Mashujaa FC inayoshiriki Ligi Kuu Bara anayesema ni wazazi wachache wanaotoa sapoti wanapogundua vijana wao wana vipaji vya michezo.

"Wengi huwa wanaamini katika kusoma tu. Ni kama ilivyokuwa kwangu nilipoingia kwenye soka ilikuwa ni ngumu. Familia yangu iliamini zaidi katika kusoma, japo halikuwa jambo baya sababu ile ni future (faida ya kesho) lakini kumbe hata kipaji kina umuhimu wake," anasema.

"Wazazi wangu walikuwa wanaamini katika masomo zaidi bila kutazama kipaji changu, lakini sasa wao ndio wananishangilia baada ya soka kuniwezesha kuendesha maisha yangu bila ya kuwategemea na muda mwingine nimekuwa nikiwasaidia.

"Mwanzo hawakutaka kuhusika na chochote kinachohusu soka lakini sasa baada ya kuona naweza kujisimamia na kuendesha maisha yangu wameanza kunisapoti na kunishangilia."

ALIVYOANZA SOKA

Katika soka kuna msemo usemao washambuliaji wanashinda mechi, lakini mabeki wanashinda mataji. Kwani unahitaji kuwa na washambuliaji makini ili kufunga mabao ili timu kushinda mechi, lakini utahitaji mabeki makini kulinda ushindi  uliopatikana na matokeo ya jambo hilo timu husika itakuwa imeshinda ubingwa unaoshindaniwa.

Hapo kwenye kulinda ushindi uliopatikana kuna mtu mmoja ni muhimu sana na huyo ni kipa. Kwenye soka unaambiwa unahitaji kuwa na kipa mahiri kurahisisha kazi ya kubeba mataji.

Hashim ni zao la kituo cha Emima ambacho kilikuwa Dar es Salaam baada ya hapo aliuzwa Tesema ambayo sasa ni KMC.

Mchezaji huyo anafunguka kuwa licha ya kupita timu nne, lakini Mbao FC ya Mwanza ndio ilimpa maisha na kumtambulisha kwenye soka.

"Usajili wangu Mbao msimu wa 2019/2020 mbali na kunipa fedha ambayo niliiwekeza kwenye biashara ya bodaboda ni timu ambayo ilinipa jina na kunifanya niweze kujulikana," anasema kipa huyo aliyepita pia Mwadui FC, Majimaji na sasa Mashujaa.

"Biashara yangu ya bodaboda haikuweza kukua kutokana na kukosa msimamizi mzuri. Niliamua kuuza na kuendelea na maisha yangu ya mpira hadi sasa, lakini bado ndoto yangu ni kuwa mfanyabiashara mkubwa hapo baadae."

KASEJA AMPA UJANJA

Wakati mastaa wengi wakilia kubadilishwa namba kutokana na makocha kubaini wana vitu tofauti ikiwa ni pamoja na vimo, Hashim anaweka wazi kuwa tangu ameanza soka ametimiza ndoto ya kukaa langoni na hajawahi kucheza nafasi nyingine tofauti.

"Tangu nikiwa na umri mdogo nilikuwa navutiwa na Juma Kaseja ambaye hakuna asiyetambua ubora wake miaka ya nyuma kabla hajaamua kutundika daruga.

"Nimeanza kucheza nafasi ya kipa tangu nikiwa na timu za mtaani hadi sasa nacheza Ligi Kuu. Nafurahia hilo kwani kimo changu pia kilikuwa kinanibeba kila mwalimu niliyepita chini yake aliamini katika nafasi ninayocheza," anasema.

Hashim anasema anafurahi alipata 'mautundu' ya Kaseja kabla ya kustaafu kwani alishapata nafasi ya kukutana naye na kumwambia kuwa yeye ndiye aliyemfanya aingie kwenye soka, ndipo alipompa nguvu na imani kuwa anaweza kufika mbali.

"Nimepata nafasi ya kukutana na Kaseja na kuzungumza naye mambo mbalimbali kuhusu soka. Kanipa mbinu nyingi na kuniambia nini niongeze ili niwe bora jambo ambalo naweza kukiri kuwa imeongeza kitu kwenye taaluma yangu," anasema.

AMKUBALI KIBU

Aliyekuwa kocha wa Simba, Roberto Oliveira maarufu kama Robertinho kabla ya kuondoka nchini aliweka wazi ubora wa mshambuliaji Kibu Denis ambaye licha ya Simba kuonekana kuwa na upungufu, ubora wake unaonekana na hilo pia limethibitishwa na Hashim.

"Ukiniamsha hata usingizini ukiniambia nikutajie mshambuliaji msumbufu na mwenye jicho la goli atakutajia Kibu. Ni mchezaji ambaye ana kila kitu, ana kasi, nguvu na jicho la kuona nyavu.

"Ukiangalia Simba kwa sasa ni mchezaji ambaye anapambana zaidi kuliko wachezaji wengine wote. Ubora wake hakuna asiyeona. Hazungumzwi sana lakini ni mchezaji ambaye anaipa Simba vitu vingi uwanjani," anasena Hashim.

MASHUJAA NI SUALA LA MUDA

Kipa huyo anakiri timu ya Mashujaa inapitia changamoto kutokana na matokeo mabaya kwa sasa, lakini hilo ni suala la muda na hali kama hiyo hutokea kwa timu nyingi duniani.

Mchezaji huyo anaamini wana nafasi ya kufanya vizuri na hawawezi kurudi walikotoka yaani Ligi ya Champioship ambako walitoka msimu huu.

"Timu yetu ambayo ilikuwa inasifiwa kuanza vizuri mechi tano za kwanza ndio hii iliyopo sasa kwenye nyakati ngumu. Huu ni upepo mbaya tu tupo imara na tutarudi kwenye ushindani," anasema.

"Kufungwa na sare tutazozipata hazitufanyi tukakubali kurudi nyuma na kuamini kuwa ndio mwisho wetu. Tuna timu nzuri na tuna imani ya kufikia malengo ya kucheza tena Ligi Kuu msimu ujao kwani mechi tulizocheza ni chache kuliko zilizobaki. Tuna nafasi ya kujitafakari na kuwa bora."

Chanzo: www.tanzaniaweb.live