Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Harry Kane, miaka 14 ya ukame, mateso

Kane Matajiiii Harry Kane, miaka 14 ya ukame, mateso

Tue, 16 Jul 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Julai Mosi, mwaka huu mshambuliaji wa Bayern Munich na England, Harry Kane alikuwa anatimiza miaka 14 ya kucheza soka la kulipwa tangu alipopandishwa kwa mara ya kwanza katika timu ya wakubwa ya Tottenham Hotspur, Julai 2010.

Kwa miaka yota hiyo Kane amecheza mechi 545 za michuano yote na kufunga mabao 340, lakini hajafanikiwa kuchukua taji hata moja.

Mara ya mwisho kwa supastaa huyo kuvaa medali ya ubingwa wa taji lolote la mashindano ilikuwa 2010 alipokuwa na timu ya taifa ya England yenye umri chini ya miaka 17 walipochukua Kombe la 1X Torneio International Algarve.

Tangu hapo Kane amecheza fainali saba za michuano mbalimbali akiwa na Spurs na Bayern Munich, lakini kote ameangukia pua.

Akiwa na Spurs alifanikiwa kuifikisha timu hiyo katika hatua ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya 2019 walipokutana na Liverpool na kupoteza kwa mabao 2-0.

Vilvile 2021 walipoteza fainali ya Carabao dhidi Manchester City taji ambalo alilipoteza hapo awali katika fainali mbele ya Chelsea 2019. Wakati huu akiwa anaichezea Spurs.

Mwaka 2020 aliangukia pua katika fainali ya Euro dhidi ya Italia katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja Wembley na

msimu uliopita akiwa na Bayern Munich wakati watu wana matumaini kwamba huenda angeondoa gundu, aliishia kula kwa macho kwani timu hiyo ilipoteza ubingwa wa Ligi kuu Ujerumani (Bundesliga) kwa mara ya kwanza baada ya miaka 11 mbele ya Bayer Leverkusen.

Haikuishia hapo, Kane na Bayern wakapoteza pia fainali ya Kombe la Shirikisho (DFB-Supercup). Katika fainali zote hizo Kane hakubahatika kufunga hata bao moja.

Wikiendi iliyopita kulikuwa na matumaini kwamba staa huyo huenda angezaliwa upya kwa kuvaa medali ya ubingwa wa Euro mbele ya Hispania, lakini ilishindikana.

Mbaya zaidi ni kwamba katika fainali saba alizocheza mbali ya kuondoka kapa bila ya taji, Kane pia hajafunga bao hata moja.

Moja kati ya vitu vinavyomfanya aongelewe zaidi kwa kukosa kwake mataji supastaa huyo wa kimataifa wa England ni uwezo wake wa kufunga unaomfanya aibuke mfungaji bora katika michuano mbalimbali licha ya kukosa makombe.

Msimu uliopita tu katika Bundesliga aliibuka kinara wa ufungaji mabao akiwa nayo 36. Pia alikuwa ndiye mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mabao manane aliyofunga.

Katika michuano ya Euro mwaka huu pia ameondoka na tuzo ya mfungaji bora. Kwa upande wa Ligi Kuu England alichukua tuzo ya mfungaji bora kwa misimu mitatu tofauti.

Ukiondoa Euro, pia Kane aliwahi kushinda tuzo ya kiatu cha dhahabu kwa kuwa mfungaji bora wa Kombe la Dunia 2018.

Chanzo: Mwanaspoti