Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Harry Kane anavyoishi kishua Ujerumani

Harry Kane Germany Harry Kane anavyoishi kishua Ujerumani

Sun, 8 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Nahodha wa timu ya taifa la England na mshambuliaji wa Bayern Munich, Harry Kane ameripotiwa kuishi kishua huko Ujerumani kwenye jumba la kifahari la Pauni 29 milioni katika kitongoji cha Munich kinachojulikana kama “Hollywood ya Ujerumani”.

Mshambuliaji huyo alijiunga na Bayern Munich majira ya joto akitokea Tottenham Hotspur anavuta kitita cha Pauni 400,000 kwa wiki.

Mkwanja huo anaokusanya kwa wiki umeripotiwa kumsaidia nahodha huyo kupanga kwenye mjengo huo wa kifahari huko Grunwald, ambako kunajulikana kama “Bavarian Beverley Hills”.

Mke wa Kane, Katie Goodland aliripotiwa mapema mwaka huu kuhusika na mchakato wa kutafuta nyumba huko Ujerumani kabla ya kufichuka kuwa nyota huyo wa zamani wa Tottenham Hotspur ameuchukua mjengo huo wa kifahari wenye vyumba 12.

Kulingana na mawakala wa mali isiyohamishika, nyumba hiyo imetajwa kuwa na mabwawa ya kuogelea ndani na ya nje yenye uwezo wa kuyafanya maji kuwa na moto au bardi, kuna sehemu ya vinywaji tu, ukumbi maalumu wa sinema na eneo la kupozi tu. Mjengo huo una vyumba tofauti kwa ajili ya wageni pia upo ndani ya fensi yenye nafasi ya kutosha, inaelezwa humo ndani kuna zaidi ya mita za mraba 400.

Kane, mwenye umri wa miaka 30, anadaiwa kukodisha nyumba hiyo kwa Pauni 70,000 kwa mwezi badala ya kuinunua moja kwa moja kulingana na mtandao wa Bild.

Grunwald, inayomaanisha “msitu wa kijani kibichi” ni eneo lenye utulivu wa kutosha na kama unapenda uoto wa asili unaweza kufurahia mandhari hayo lakini pia kuna uwanja wa kipekee wa gofu na migahawa mingi ya kifahari.

Pia ni sehemu inayopendwa zaidi na baadhi ya wachezaji wenzake wapya wa Harry huko Bayern Munich, na pia watu mashuhuri.

Wanaoishi kati ya wakazi 11,000 wa eneo hilo ni nyota wa Bayern kina Alphonso Davies, Matthijs de Ligt, Eric Maxim Choupo-Moting, Benjamin Pavard na Leroy Sane.

Kane anaungana na wachezaji wenzake kuishi kishua huko Grunwald pamoja na mkewe Katie na watoto wao wanne Ivy (6), Vivienne (5), Louis (2) na Henry ambaye alizaliwa muda mfupi baada ya kuhamia Ujerumani.

Wasichana hao wanaweza kuhudhuria Shule ya Kimataifa ya Munich ambayo ina ada ya Euro 7,500 kwa mwaka.

Grunwald pia ina migahawa ya hali ya juu ikiwa ni pamoja na Pan Asian Chang Chang, ambapo sahani za ‘sushi’ moja ya chakula maarufu inagharimu karibu Euro 100.

Kane ambaye anafurahia maisha yake ya soka Ujerumani, alizaliwa Julai 28, 1993 huko Walthamstow, London, kwa Kim (nee Hogg).

Mshambuliaji huyo ana asili ya Ireland kupitia baba’ke ambaye anatoka Galway.

Familia yake ilihamia Chingford ambapo Kane alihudhuria Chuo cha Larkswood hadi 2004, ikifuatiwa na Shule ya Msingi ya Chingford (ambayo pia ilihudhuriwa na David Beckham). Alicheza soka tangu akiwa mdogo akijiunga na klabu ya ndani, Ridgeway Rovers kabla ya kwenda Watford na Tottenham ambako alijizolea umaarufu.

Chanzo: Mwanaspoti