Wakala wa Mshambuliaji kutoka England na Klabu ya Tottenham Hotspur Harry Kane amekutana na mabosi wa Paris Saint-Germain kujadili uwezekano mchezaji wake kuenda jijini Paris kwa msimu ujao 2023/24.
Mshambuliaji Kane anapigiwa hesabu za kuachana na Tottenham Hotspur kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi, huku mkataba wake utakitarajia kufikia tamati mwakani.
Klabu ya Manchester United imekuwa ikiripotiwa kuhitaji saini Kane, lakini Mshambuliaji huyo anazivutia pia timu za nje ya England.
PSG inaaminika kuweka kipaumbele kwenye usajili wa mshambuliaji wa kati kwenye dirisha lijalo na wanamtaka Kane baada ya kumkosa Robert Lewandowski.
Kwa mujibu wa Foot Mercato, PSG tayari imeshaanza mazungumzo na mawakala wa Kane.
Mkurugenzi wa michezo wa PSG Luis Campos alikutana na wawakilishi wa Kane hivi karibuni kwa ajili ya kwenda kukipiga Parc des Princes inaaminika.
Lakini shughuli ya kumshawishi Kane aondoke England ni ngumu kwa sababu mshambuliaji huyo dhamira yake ni kuvunja rekodi ya Alan Shearer ya mabao kwenye Ligi Kuu.
Shearer amefunga mabao 260, wakati Kane kwa sasa anashika namba mbili akiwa amefunga mabao 210 kwenye historia ya Ligi Kuu England.
Spurs hawatakuwa tayari kumuuza kama hakutakuwa na mkwanja unaoanzia Pauni 100 milioni mezani.
Man United wao walimwambia Kane kama atajiunda kwao basi watamlipa mshabara wa Pauni 300,000 kwa juma.