Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Harambee yaanza kuipeleka Pamba Jiji Ligi Kuu

Pamba Jiji Mwanza Harambee yaanza kuipeleka Pamba Jiji Ligi Kuu

Mon, 12 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla amewaongoza viongozi wa taasisi za umma, viongozi wa Serikali, wafanyabiashara na wadau mbalimbali wa soka mkoani humo katika harambee maalum ya kukusanya fedha za kuipeleka timu ya Pamba Jiji Ligi Kuu msimu huu, ambapo katika hafla hiyo jumla Sh milioni 177 zimepatikana.

Harambee hiyo imefanyika leo jijini humo kuanzia saa 12 jioni katika ukumbi wa Mwanza Hotel. Miongoni mwa waliochangia harambee hiyo ni mfanyabiashara Christopher Gachuma Sh milioni 35, Evarist Hagila na wenzake Sh 7 milioni, Katibu wa Itikadi na Uenezi Chama Cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda Sh milioni 10, Waziri wa Ulinzi, Stagomena Tax Sh milioni 5 na Mbunge wa Nyamagana, Stanslaus Mabula sh milioni 5.

Wengine ni Naibu Waziri Mkuu, Dotto Biteko ambaye amechangia Sh milioni 10 na klabu ya Yanga kupitia kwa Rais wake, Hersi Said Sh milioni 2 na mjumbe wa kamati tendaji ya timu hiyo, Yanga Makaga Sh milioni 2.

Akielezea harambee hiyo, Makalla amesema katika Sh milioni 177 zilizokusanywa Sh milioni 18.9 ni fedha taslimu, Sh milioni 48 miamala ya benki na Sh milioni 109 ambazo ni ahadi zilizoahidiwa kutolewa ndani ya wiki mbili.

Amewaahidi wachangiaji kwamba fedha hizo zitakuwa salama na zitatumika kwa matumizi yaliyokusudiwa ya kuipandisha timu ya Pamba kwenda Ligi Kuu, ambapo pamoja na mambo mengine zitafanya kazi ya kuhakikisha wachezaji wanapata motisha nzuri, kuishi sehemu nzuri, usafiri mzuri na mengineyo ili wafanye vyema katika michezo tisa iliyosalia ya Ligi ya Championship.

“Chochote mlichotoa kina thamani sana Kila aliyetoa sisi tunamuona ni mtu muhimu katika safari ya mafanikio, siku nyingine tukiwaita tutakuja kutoa hesabu ya kile tulichokitoa leo, kwahiyo tuna nyenzo tuachieni kazi Sh milioni 177 tunazo tunawaambia pisheni njia tunakuja,” amesema Makalla

Mfanyabiashara na mjumbe wa bodi ya timu hiyo, Christopher Gachuma, amesema kupatikana kwa fedha hizo siyo kwamba kila kitu kimeisha, kwani wanapaswa kuendelea kuhamasisha kwa kuwa kazi ndiyo kwanza kuhakikisha malengo waliyojiwekea yanatimia.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live