Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hapa usibeti, utaliwa!

Stephen Aziz Ki Goals Stephen Aziz Ki

Sun, 1 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Msimu wa 17 wa michuano ya Kombe la Mapinduzi unatarajiwa kuanza kesho Jumapili kwa timu 12 kuchuana kuwania ubingwa wa michuano hiyo inayofanyika kati ya Januari 1-13, 2023.

Kama ilivyokuwa michuano iliyopita, safari hii itafanyika kwenye Uwanja wa Amaan, mjini Unguja, huku timu hizo 12 zikiwa zimepangwa katika makundi manne tofauti.

Kila kundi lina timu tatu na kwa mujibu wa Kamati ya Mashindano ya Mapinduzi ni kwamba mshindi wa kwanza wa kundi husika atafuzu moja kwa moja hadi nusu fainali.

Kundi A safari hii lina timu za Azam ambao ni mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo, sambamba na Malindi na Jamhuri, huku Kundi B, likiwa na Yanga, Singida Big Stars na KMKM, wakati Kundi C lina watetezi Simba, KVZ na Mlandege huku Namungo, Chipukizi na Aigle Noir kutoka Burundi ziko Kundi D.

Kwa mujibu wa ratiba mechi za makundi zitaanza kuchezwa kati ya Januari 1-6 kisha kuwa na mapumziko ya siku moja kabla ya timu zilizofuzu nusu fainali kuanza kuumana kati ya Januari 8-9 na kuwepo kwa mapumziko ya siku tatu kisha ndipo ije ipigwe mechi ya fainali Januari 13.

Tayari timu shiriki za michuano hiyo zimeanza maandalizi na nyingine kuanza kwenda visiwani humo kwa ajili ya kuwasha moto ambao huwapa burudani mashabiki wa soka nchini.

Mwanaspoti linakuletea baadhi ya mambo yanayoifanya michuano hiyo iliyoasisiwa kwa mtindo unaotumika sasa mwaka 2007 kuwa migumu kutabiriwa mapema, yaani kama kuna wanaotaka kubeti wajue mapema wakizubaa wanaliwa kweupe. Kivipi? Endelea...!

VITA YA UFUNGAJI

Kwa misimu ya karibuni michuano hiyo imekuwa migumu kutabiri vita ya ufungaji mabao, kwani idadi ya mechi na ugumu wa michuano imekuwa ikiwakatili baadhi ya mastaa wanaosifika kwa kutupia mipira nyavuni.

Utabisha nini wakati kwa misimu mitatu mfululizo hakuna mchezaji aliyewahi kufikisha angalau mabao matano.

Msimu uliopita Meddie Kagere aliyekuwa Simba na safari hii anashuka katika michuano hiyo akiwa na Singida Big Stars, aliibuka mfungaji bora akiwa na mabao mawili tu, likiwamo lile la fainali alilolifunga kwa mkwaju wa penalti.

Hivyo hata msimu huu kwa idadi ya mechi za michuano hiyo (nne tu, mbili za hatua ya makundi, moja nusu fainali na nyingine ya fainali) zinatoa nafasi finyu kwa wachezaji kufunga idadi kubwa ya mabao, labda kama mtu atafunga hat-trick ambayo kwa siku za karibu zimekuwa adimu katika michuano hiyo.

Timu zote 12 zina majembe tishio wa kucheka na nyavu, lakini bado ni ngumu kwa mtu kubeti nani atakayeibuka mbabe katika michuano hiyo, hivyo lolote linaweza kutokea lakini haitabiriki mapema.

BINGWA KUTOKA ZENJI

Wazee wa kubeti wasitesti kabisa kuweka mzigo kwa timu za visiwani Zanzibar, japo soka huwa lina matokeo ya kustaajabisha.

Rekodi zinaonyesha tangu mwaka 2012, pale Jamhuri Pemba ilipofika fainali na kufungwa na Azam, hakuna timu yoyote ya visiwani Zanzibar iliyowahi kutimba hatua hiyo, mbali na kubeba ubingwa wa Mapinduzi tangu Miembeni ilipofanya hivyo kwa kuifumua KMKM mabao 2-0, mwaka 2009.

Timu nyingine ya Zanzibar iliyowahi kufika fainali ni Ocean View iliyofanya hivyo mwaka 2010 na kukubali kipigo cha bao 1-0 mbele ya Mtibwa Sugar, ndipo ikafuata Jamhuri 2012 na baada ya hapo timu za visiwa hivyo zimekuwa kama wasindikizaji kwenye michuano hiyo ya Kombe la Mapinduzi.

Kwa msimu huu licha ya Zanzibar kuwakilishwa na timu sita, wakiwamo mabingwa wa Ligi Kuu ya visiwani humo, KMKM, vinara wa sasa wa ZPL, KVZ inayonolewa na kocha Amri Said ‘Jaap Stam’, Malindi na Mlandege zote za visiwani Unguja pamoja na Jamhuri na Chipukizi za visiwa vya Pemba, bado ni ngumu kuweka karata na kuzitabiria kufanya maajabu mbele ya timu nyingine shiriki.

Hata hivyo, bado kama wawakilishi hao wa Zanzibar wataamua kulitupa joho la unyonge mbele ya wapinzani wao kwenye msimu huu wa Mapinduzi wanaweza kuwashangaza wengi, ila usibeti kwa sasa!

WAGENI KUBEBA NDOO

Baada ya misimu michache iliyopita ya kuwekwa kando kwa timu waalikwa kutoka nje ya mipaka ya Tanzania, hatimaye msimu huu Aigle Noir kutoka Burundi imepata fursa ya kuwasha moto sambamba na timu nyingine 11 kutoka Tanzania.

Timu hii ni ngeni kwenye michuano hiyo, kwani kwa miaka mingi zilizoeleka klabu kutoka Kenya na Uganda kuja kushiriki na kuleta upinzani mkali ikiwamo kufika fainali na hata kubeba ndoo kibabe.

Tusker ya Kenya ilishafika fainali za mwaka 2013 na kupasuka mbele ya Azam kwa mabao 2-1, lakini KCCA na URA zilifika fainali tatu tofauti za mwaka 2014, 2016 na 2018 na mara mbili kati ya hizo ziliondoka na ubingwa kwa kuzifunga Simba na Mtibwa na moja kukwama mbele ya Azam.

KCCA ilikuwa timu ya kwanza ya kigeni kubeba Kombe la Mapinduzi mwaka 2014 baada ya kuizidi akili Simba na kuichapa bao 1-0, kisha 2016 ikawa zamu ya URA iliyoinyoa Mtibwa kwa mabao 3-1 na 2018 URA tena ikafika fainali na kulala mbele ya Azam kwa mikwaju ya penalti 4-3 baada ya dakika 120 kumalizika kwa sare ya 0-0.

Ugeni iliyonayo kwenye michuano hiyo na aina ya vikosi vya timu wenyeji wa michuano hiyo kwa maana ya vigogo, Simba, Yanga, Azam, Singida Big Stars, Namungo na zile sita za visiwani, Aigle Noir ina nafasi finyu ya kuondoka na ubingwa, hata kama mpira unadunda.

Ili ifanikishe ndoto hizo za kuondoka na ubingwa ni lazima Warundi hao wakaze kweli kweli na kwanza kuhakikisha inatoboa mbele ya Chipukizi na Namungo ili itinge nusu fainali kisha ndipo ianze kufikiria fainali ambayo haijui itacheza na timu ipi na hapo ndipo pana ugumu wa kuibetia mapema.

NYOTA WATAKAONG’ARA

Kama ilivyo ngumu kutabiri timu ipi itakayoweza kubeba ubingwa wa msimu huu wa michuano hiyo ya Kombe la Mapinduzi 2023, ndivyo ilivyo kwa kubeti wachezaji gani wa klabu 12 zinazoshiriki michuano hiyo watakaong’ara.

Hii ni kutokana na ukweli michuano ya Mapinduzi huwa haitabiriki kwa mastaa wenye majina, pale watu wakiamini watauwasha moto huishia kuwa wa kawaida na kuibuka wachezaji wengine wasiotarajiwa, hivyo kufanya hata msimu huu mambo kuwa magumu.

Kinachozidi kutoa ugumu wa kutabiri ni mfumo wa michuano hiyo kuruhusu klabu kuwatumia wachezaji hata wale wasiokuwa kwenye usajili wa kudumu wanaotumika kwenye mechi za ligi na michuano inayotambulika kimataifa, imechangia kuleta ugumu kwa baadhi ya mastaa kutabirika.

Tayari baadhi ya makocha akiwamo wa Yanga, Nasreddine Nabi wameweka bayana kutaka kupumzisha nyota wa kikosi cha kwanza kutokana na timu zao kuwa na michuano migumu mbele yao ikiwamo ile ya CAF sambamba na nyota hao kutumika kwa muda mrefu bila kupumzika.

Chanzo: Mwanaspoti