Katika timu ngumu kuzitetea hapa Tanzania, nadhani Azam FC inaongoza.
Kila inapoanza msimu inakupa matumaini kama itashindania vilivyo ubingwa wa ligi na mashindano mengine ambayo hushiriki.
Utaona inafanya usajili wa wachezaji ambao wanaonekana mahiri kwenye timu zao ambao huaminisha wengi kuwa watawasha moto vilivyo kwenye msimu husika. Watafanya maandalizi kabambe ya kabla ya msimu (pre-season) nje na ndani ya nchi na yanaweza kukuaminisha kuwa Simba na Yanga zitakutana na ushindani mkali katika mbio za ubingwa za mashindano tofauti.
Hata hivyo, msimu ukishaanza Azam inageuka timu ya kukamia mechi mojamoja na nyingi hucheza pasipo kuonyesha kama timu kubwa ambayo ina kiu na hamu ya kutwaa mataji.
Mfano mzuri ni msimu huu, wakati ulipoanza, kila mmoja aliamini kuwa watatoa ushindani mkali katika Ligi Kuu kutokana na usajili waliofanya lakini hadi sasa, wameshatoka katika mbio za ubingwa huku zikiwa zimebaki raundi tano kabla ya ligi kumalizika.
Badala yake leo hii imebakia kuwania nafasi ya tatu dhidi ya Singida Big Stars ambayo ndio kwanza inashiriki kwa mara ya kwanza kwenye Ligi Kuu msimu huu.
Yaani kama hadi ligi imebakiza raundi tano kumalizika, Azam haina uhakika hata wa kumaliza katika nafasi ya tatu, unapata wapi nguvu za kusimamia na kuitetea pale watu wanapoikosoa?