Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hao Azam FC jeuri ipo hapa

Azam FC VS MAPINDUZI Hao Azam FC jeuri ipo hapa

Sun, 5 Mar 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Azam FC hesabu za ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa sasa hazipo kutokana na kuyumba mwanzoni ikiacha vita kwa watani wa jadi, Simba na Yanga, hata hivyo, timu hiyo bado ina nafasi ya kumaliza msimu kwa heshima kama itaamua kukaza buti kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho (ASFC).

Kikosi hicho usiku wa leo kitafunga hesabu ya mechi za 16 Bora kwa kuikaribisha Mapinduzi ya Mwanza iliyopo Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL), itakayopigwa Uwanja wa Azam Complex, huku ikiwa na jeuri ya kujivunia rekodi zake kwenye michuano hiyo hasa kwa timu za madaraja ya chini.

Rekodi zinaonyesha tangu mwaka 2015, michuano hiyo iliyokuwa ikifahamika kama Kombe la FA kurejeshwa ikiwa na jina jipya la ASFC, Azam haijawahi kutolewa hatua ya 16 Bora kwani katika michezo yake saba iliyocheza ilishinda yote na kutinga robo fainali.

Februari 29, 2016 iliichapa Panone mabao 2-1 ikiwa ni msimu iliyofika hadi fainali na kupoteza kwa Yanga kwa mabao 3-1, kisha Februari 24, 2017 ilitinga tena na kuiondosha Mtibwa Sugar baada ya kuichapa kwa bao 1-0 kabla ya Februari 24, 2018 iliifunga KMC mabao 3-1.

Msimu wa 2018/19 iliichapa Rhino Rangers 3-0 na Februari 25, 2019 ukiwa ndio msimu iliyobeba taji la ASFC kwa kuinyoa Lipuli ya Iringa kwa bao 1-0 katika fainali na msimu wa 2020/2021 ikakutana na Ihefu na kuiondoa kwa penalti 5-4 baada ya timu hizo kutoka sare ndani ya dakika 90.

Azam iliendeleza moto wake tena ndani ya 16 Bora Aprili 29, 2021 ilipokutana na Polisi Tanzania ikaifunga kwa mabao 2-1 na mwaka jana Februari 12 iliifunga Baga Friends kwa mabao 6-0 japo iliishia nusu fainali kwa kutolewa na Coastal Union kwa matuta 6-5 baada ya suluhu ndani ya dakika zote 120 za mchezo huo.

Akizungumzia maandalizi yao kiujumla Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Dani Cadena alisema unapokuwa na rekodi zuri juu ya kitu fulani inakuongezea motisha kwenye utendaji wako ingawa jambo muhimu ni kujipanga vizuri.

Azam ilifuzu hatua hii baada ya kuifunga Dodoma Jiji kwa mabao 4-1 huku Mapinduzi ambao ni Mabingwa wa Mkoa wa Mwanza kwa misimu miwili mfululizo iliifunga Polisi Katavi kwa penalti 4-3 baada ya mchezo huo kuisha suluhu.

Mbali ya mechi hiyo ya Saa 1:00 usiku, mapema saa 10:00 jioni utapigwa mchezo mwingine wa michuano hiyo kwa kuzikutanisha Kagera Sugar itakayokuwa wenyeji wa Mbeya City kwenye Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba mkoani Kagera.

Hadi sasa jumla ya timu nne zimejihakikisha kucheza robo fainali (kabla ya mechi mbili za jana) ambazo ni Simba iliyotangulia mapema kwa kuinyoa African Sports kwa mabao 4-0, huku Yanga ikiing'oa Tanzania Prisons kwa mabao 4-1, Geita Gold kuitoa Green Warriors kwa 3-1 huku Singida Big Stars iliyoifunga JKT Tanzania.

Chanzo: Mwanaspoti